10. Ni ipi hukumu ya swawm ya mwanamke mwenye hedhi na mwenye damu ya uzazi wakichelewesha kulipa mpaka katika Ramadhaan nyingine?

Swali 10: Ni ipi hukumu ya swawm ya mwanamke mwenye hedhi na mwenye damu ya uzazi wakichelewesha kulipa mpaka katika Ramadhaan nyingine? Ni kipi kinachowalazimu?

Jibu: Ni lazima kwa mwenye hedhi na nifasi kula wakati wa hedhi na nifasi. Haifai kwao kufunga wala kuswali wakati wa hedhi na nifasi. Si sawa kwao kufanya hivo. Ni lazimsa kwao kulipa swawm na si swalah kutokana na yale yaliyothibiti kutoka kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa):

“Aliulizwa kama mwanamke mwenye hedhi analazimika kulipa funga na swalah?” Akajibu: “Tulikuwa tukiamrishwa kulipa swawm na wala hatuamrishwi kulipa swalah.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Wanachuoni (Rahimahumu Allaah) wameafikiana juu ya yale yaliyotajwa na ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) kwamba ni wajibu kwa mwenye hedhi na mwanamke mwenye damu ya uzazi kulipa swawm na kutolipa swalah. Hii ni rehema na wepesi wa Allaah (Subhaanah) juu yao. Kwa sababu swalah ni kitu kinakariri kwa siku mara tano na hivyo kuzilipa kuna ugumu kwao. Kuhusu swawm ya Ramadhaan ni lazima kwa mwaka mara moja. Hivyo hakuna ugumu kwao juu ya kuilipa.

Mwenye kuchelewesha kulipa deni lake mpaka kukaingia Ramadhaan nyingine, pasi na kuwa na udhuru wa Kishari´ah, basi ni lazima kwake kutubu kwa Allaah juu ya kitendo hicho pamoja na kulipa na kulisha masikini kwa kila siku moja. Vivyo hivyo mgonjwa na msafiri wakichelewesha kulipa mpaka kukaingia Ramadhaan nyingine, pasi na kuwa na udhuru wa Kishari´ah, basi ni lazima kwao kulipa, kutubu na kulisha kwa kila siku moja masikini. Ama ikiwa ugonjwa au safari itaendelea mpaka Ramadhaan nyingine, basi ni lazima kwao kulipa peke yake pasi na kuhitajia kulisha. Hapa ni baada ya yeye kupona kutoka katika maradhi yake na kufika kutoka safarini mwake.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdllaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: As-ilah Muhimmah tata´alaqah bisw-Swiyaam, uk. 19-20
  • Imechapishwa: 19/04/2019