10. Mahimizo ya umoja ndani ya matendo ya Salaf


Kuhusu matendo ya Salaf hakika miongoni mwa misingi ya Ahl-us-Sunnah wal-Jmaa´ah juu ya masuala yenye tofauti muda wa kuwa tofauti hizo zinatokana na Ijtihaad na isitoshe ikawa inafaa kufanya Ijtihaad katika mambo hayo, basi baadhi wanawapa udhuru wengine kwa tofauti hizo. Hilo halipelekei baadhi kuwajengea wengine chuki, uadui wala bughudha. Bali wanaonelea kuwa wote ni ndugu ingawa kutatokea kati yao tofauti hii. Wakati mwingine hli inafikia kiasi cha kwamba baadhi yao huswali nyuma ya yule ambaye yeye anaonelea kuwa hana wudhuu´ lakini imamu yeye anaona kuwa yuko na wudhuu´. Mfano wa hilo ni kama kuswali nyuma ya mtu ambaye amekula nyama ya ngamia; imamu huyo yeye anaona kuwa nyama ya ngamia haichengui wudhuu´ lakini mswaliji nyuma yake yeye anaona kuwa inachengua wudhuu´. Hivyo anaona kuwa swalah nyuma yake inasihi ingawa yeye endapo ataswali peke yake basi ataona kuwa swalah yake haisihi. Yote haya ni kwa sababu wanaona kuwa tofauti ambayo inatokana na Ijtihaad katika yale mambo ambayo inafaa kufanya Ijtihaad ukweli wa mambo ni kwamba sio tofauti. Kwa sababu kila mmoja katika watu wawili hawa amefuata kile kinachomuwajibikia kwake kukifuata katika dalili ambayo haijuzu kwake kuiacha. Wao walikuwa wanaona kuwa ndugu yao akitofautiana nao katika kitendo ambacho hakufuata dalili ukweli wa mambo ni kwamba ameafikiana nao. Kwa sababu wao huita kufuata dalili popote ilipo. Akitofautina nao kutokana na dalili aliyoona yeye basi ukweli wa mambo ni kwamba amewafuata. Kwa sababu amefuata yale wanayolingania na kuyaongoza katika kuhukumiana kwa Qur-aan na Sunnah.

Kuhusu yale mambo ambayo haifai kufanya Ijtihaad ni yale ambayo yanatofautiana na yale waliyokuwemo Maswahabah na wanafunzi wa Maswahabah. Mfano wa hayo ni yale mambo ya ´Aqiydah ambayo wamepotea kwayo baadhi ya watu. Tofauti ilikuja kutokea katika mambo hayo baada ya kumalizika kwa zile karne bora. Kwa msemo mwingine tofauti haikuenea isipokuwa baada ya karne bora ingawa baadhi ya tofauti zilikuweko zama za Maswahabah. Lakini itambulike tunaposema “karne za Maswahabah” haina maana kwamba ni lazima afe kila Swahabah. Bali tunachokusudia ni ile karne ambayo wako asilimia kubwa ya watu wake. Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

“Kunasemwa kumalizika kwa karne pindi wanapomalizika wakazi wake wengi.”

Karne bora zilimalizika na hakukuweko hizi tofauti ambazo zilienea baada yao zinazohusu ´Aqiydah. Yule anayekwenda tofauti na yale waliyokuwemo Maswahabah na wanafunzi wa Maswahabah basi haikubaliwi tofauti yake.

Kuhusu masuala ambayo kulipatikana kwayo tofauti katika zama za Maswahabah na ikawa inafaa kufanya Ijtihaad yake basi ni lazima tofauti iendelee kuweko. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Akihukumu hakimu na akajitahidi ambapo akapatia basi anapata ujira mara mbili. Na akijitahidi na akakosea basi anapata ujira mara moja.”[1]

Hiki ndio kigezo.

Kwa hiyo ni lazima kwa waislamu wote wawe kitu moja na kusitokee baina yao tofauti na makundimakundi kwa njia ya kwamba wakachukiana baina yao kwa lugha za ndimi zao, wakafanyiana uadui na wakachukiana eti kwa sababu ya tofauti ambazo inafaa kufanya Ijtihaad. Kwa sababu ikiwa watatofautiana katika yale wanayotofautiana kutokana na vile yanavyopelekea maandiko kwa mujibu wa fahamu zao basi hilo ni jambo lenye wasaa na himdi zote anastahiki Allaah. Muhimu ni mioyo iungane na kupatikane umoja.

Hapana shaka kwamba maadui wa waislamu wanapenda wawaone waislamu wamefarikiana. Ni mamoja wale maadui ambao wanaonesha waziwazi uadui wao au maadui ambao wanajidhihirisha eti kuwapenda waislamu na Uislamu, ilihali ukweli wa mambo hawako hivo.

[1] al-Bukhaariy (7352) na Muslim (1716).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sittah, uk. 15-17
  • Imechapishwa: 27/06/2021