10. Kusubiri wakati wa kulingania na kumfanya Mtume ni kiigizo katika hilo


Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Suala la nne: Kusubiri juu ya maudhi yatakayompata mtu ndani yake.

MAELEZO

Ni jambo linalojulikana kwamba yule anayewakataza watu maovu basi atafikwa na shari kutoka kwa watu waovu. Kwa sababu watu wengi hawataki kheri. Bali wanachotaka ni mambo ya matamanio, mambo ya haramu na matamanio ya batili. Hivyo anapokuja anayewalingania kwa Allaah na kuwazuia kutokamana na matamanio basi ni lazima wamkabili kwa maneno au kwa vitendo. Kwa hiyo ni lazima kwa yule mwenye kulingania kwa Allaah na anataka uso wa Allaah asubiri juu ya maudhi na asubiri juu ya kulingania kwa Allaah. Kiigizo chake katika hayo ni Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam). Mbora wao na wa mwisho wao ni Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam). Alifikwa na mangapi kutoka kwa watu? Ni maudhi mangapi ya kimaneno na kivitendo yalimfika? Walisema kuwa ni mchawi na mwongo. Wakasema kuwa ni mwendawazimu. Walisema maneno mengi yaliyotajwa na Allaah (´Azza wa Jall) ndani ya Qur-aan na wakamkabili kwa maudhi mbalimbali. Pindi alipowalingania kwa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) walimpiga mawe mpaka miguu yake ikatokwa na damu. Wakamuwekea matumbo ya ngamia juu ya mgongo wake wakati amesujudu kwenye Ka´bah. Wakamtishia kumuua na kumpa vitisho mbalimbali. Katika vita vya Uhud yalipitika kwake (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) na kwa Maswahabah wake yaliyopitika; waliyavunja magego yake na kumuumiza kichwani mwake (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) na akatumbukia shimoni ilihali ni Mtume wa Allaah. Yote haya ni maudhi wakati wa kulingania kwa Allaah (´Azza wa Jall). Lakini alifanya subira na akastahamili na yeye ndiye mbora wa viumbe (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam).

Kwa hiyo ni lazima kwa yule anayesimama kulingania ajiandae maudhui kwa kiasi cha imani yake na ulinganizi wake. Lakini ni lazima kwake kuvumilia. Muda wa kuwa yuko juu ya haki basi ni lazima kwake kusubiria na kustahamili. Yuko katika njia ya Allaah. Maudhi yanayomfika yatawekwa katika sahani la matendo yake mema na ujira kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 27-28
  • Imechapishwa: 24/11/2020