10. Katika hali hii ndio kutaswaliwa ´iyd msikitini

Inawezekana mtu akasapoti sababu hiyo kutokana na yale aliyopokea al-Bayhaqiy katika “as-Sunan al-Kubraa” (03/310) kupitia kwa Muhammad bin ´Abdil-´Aziyz bin ´Abdir-Rahmaan, kutoka kwa ´Uthmaan bin ´Abdir-Rahmaan at-Taymiy ambaye amesema:

“Katika uongozi wa Abaan bin ´Uthmaan Madiynah, usiku wa kuamkia siku ya Fitwr kulinyesha mvua kubwa. Akawakusanya watu msikitini na hakutoka kwenda mahali pa uwanja ambapo kulikuwa kukiswaliwa Fitwr na Adhwhaa.” Kisha akasema kumwambia ´Abdullaah bin ´Aamir bin Rabiy´ah: “Simama na uwaeleze watu yale nimetoka kukueleza punde.” ´Abdullaah bin ´Aamir akasema: “Wakati wa ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) kulinyesha mvua kiasi cha kwamba watu hawakuweza kwenda mahali pa uwanja. Hivyo basi ´Umar akawakusanya watu msikitini na akawaswalisha. Halafu akasimama juu ya mimbari na kusema: “Enyi watu! Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiwatoa watu kwenda mahali pa uwanja akiwaswalisha huko. Kwa sababu hivyo ndio kuzuri na kwenye wasaa na kwa kuwa msikiti haukuwa na nafasi yenye kuwatosha. Akasema: ”Kukinyesha mvua, basi bora ni kuswali msikitini.”[1]

Upokezi huu ni dhaifu sana. Muhammad bin ´Abdil-´Aziyz ndiye Muhammad bin ´Abdil-´Aziyz bin ´Umar bin ´Abdir-Rahmaan bin ´Awf al-Qaadhwiy. al-Bukhaariy amesema:

“Husimulia Hadiyth munkari.”

an-Nasaa´iy amesema:

“Ni mwenye kuachwa.”

Vilevile ash-Shaafi´iy ameipokea katika “al-Umm” (01/207) kupitia njia nyingine kutoka kwa Abaan bila ya Hadiyth kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kadhalika sababu hiyo imetokana na Swahabah na wakati huohuo mlolongo wa wapokezi wake ni dhaifu mno kwa sababu imetoka kwa mwalimu wa ash-Shaafi´iy ambaye ni Ibraahiym bin Muhammad bin Abiy Yahyaa al-Aslamiy alikuwa mwongo. Maalik amesema:

“Hakuwa ni mwaminifu katika Hadiyth wala katika dini yake.”

Ndio maana Haafidhw amesema:

”Ni mwenye kuachwa.”[2]

Kwa hivyo kusema kwamba sababu ilikuwa ni kutokana na ufinyu wa msikiti. Sambamba na hilo maoni ya wanachuoni yenye kusema kuwa Sunnah na jambo lililowekwa katika Shari´ah ni kuswali mahali pa uwanja katika kila zama na kila pahali, isipokuwa tu kukiwepo dharurah, yanabaki kuwa na nguvu. Simjui mwanachuoni yeyote ambaye elimu yake inategemewa aliyepingana na hili. Ibn Hazm amesema:

“Sunnah katika swalah za ´Iyd ni wakazi wa kijiji na mji watoke wende sehemu ya uwanja ilio wazi, katika pande za nje ya miji yao, asubuhi pale ambapo jua ni jeupe na inajuzu kuswali swalah za Sunnah.”[3]

Halafu akasema:

“Ikiwa watapata uzito wa kutoka na kwenda mahali pa uwanja, basi waswali katika msikitini mkubwa.”[4]

Kisha akasema:

“Imesimuliwa kwetu ya kwamba ´Umar na ´Uthmaan (Radhiya Allaahu ´anhumaa) waliwaongoza watu swalah ya ´Iyd msikitini kutokana na mvua iliyonyesha siku ya ´Iyd. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akitoka na kwenda mahali pa uwanja kwa ajili ya kuswali swalah ya ´Iyd, jambo ambalo ndio bora zaidi. Hata hivyo mtu anapewa ujira kwa jengine pia, kwa sababu inahusiana na kitendo na sio maamrisho.”[5]

[1] as-Sunan al-Kubraa (3/310).

[2] at-Taqriyb.

[3] al-Muhallaa (05/81).

[4] al-Muhallaa (05/86).

[5] al-Muhallaa (05/87).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swalaat-ul-´Iydayn, uk. 26-28
  • Imechapishwa: 13/05/2020