Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

“Miongoni mwa Sunnah hizo ni kuamini Qadar, kheri na shari yake na kusadikisha Hadiyth juu yake. Maswali kama “Kwa nini?” na “Vipi?” hayatakiwi kuulizwa.”

MAELEZO

Hapa kunabainishwa yale yote yaliyomo ndani ya Qur-aan na Sunnah Swahiyh Ahl-us-Sunnah wanaofuata njia ya Salaf wanayakubali. Wanatilia bidii kujifunza nayo na kuitendea kazi, ni mamoja inahusiana na ´Aqiydah au kitu kingine katika mambo ya kielimu. Miongoni mwa hayo ni imani juu ya Qadar.

Qadar ni makadirio ya Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) juu ya kila kitu. Ahl-us-Sunnah wanayaamini maandiko yote yanayohusiana na mada hii tukufu ambayo imefanya mapote mengi kuangamia. Baadhi ya maandiko hayo ni maneno ya Allaah (Tabaarak wa Ta´ala):

إِنَّا كُلَّ شَيْءٍ خَلَقْنَاهُ بِقَدَرٍ

”Hakika sisi Tumekiumba kila kitu kwa Qadar.”[1]

وَخَلَقَ كُلَّ شَيْءٍ فَقَدَّرَهُ تَقْدِيرًا

“Ameumba kila kitu akakikadiria kiwango cha sawasawa.”[2]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah amekadiria makadirio ya viumbe wote miaka elfu khamsini kabla ya kuumba mbingu na ardhi na ´Arshi Yake ilikuw juu ya maji.”[3]

“Kitu cha kwanza alichoumba ni kalamu. Akaiambia: “Andika.” Ndipo kukakadiriwa kila kitachotokea mpaka siku ya Qiyaamah.”[4]

Allaah amesema kuhusu hilo:

إِنَّا نَحْنُ نُحْيِي الْمَوْتَىٰ وَنَكْتُبُ مَا قَدَّمُوا وَآثَارَهُمْ ۚ وَكُلَّ شَيْءٍ أَحْصَيْنَاهُ فِي إِمَامٍ مُّبِينٍ

“Hakika Sisi tunahuisha wafu na tunaandika yale waliyoyatanguliza na athari zao na kila kitu tumekirekodi barabara katika daftari kinachobainisha.”[5]

Kalamu imeandika kila kitu kitachotokea mpaka Qiyaamah kitaposimama.

Kupitia tafiti za kisomi Qadar ina daraja zifuatazo:

1- Elimu. Allaah amekiumba kila kitu kwa uwezo Wake na amekizunguka kila kitu kwa elimu Yake. Kalamu imekiandika kila kitu kutokana na amri Yake, pasi na kuonegza wala kupunguza, si mapema wala si kwa kuchelewa.

2- Akayaandika kwenye Ubao uliohifadhiwa.

3- Matakwa ya kilimwengu. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

فَمَن يُرِدِ اللَّـهُ أَن يَهْدِيَهُ يَشْرَحْ صَدْرَهُ لِلْإِسْلَامِ ۖ وَمَن يُرِدْ أَن يُضِلَّهُ يَجْعَلْ صَدْرَهُ ضَيِّقًا حَرَجًا كَأَنَّمَا يَصَّعَّدُ فِي السَّمَاءِ

“Basi yule ambaye Allaah anataka kumwongoza, humfungulia kifua chake kwa Uislamu na yule ambaye anataka kumpotoa, basi hufanya kifua chake kuwa na dhiki chenye uzito kana kwamba anapanda kwa tabu mbinguni.”[6]

مَن يَشَإِ اللَّـهُ يُضْلِلْـهُ وَمَن يَشَأْ يَجْعَلْهُ عَلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ

“Allaah humpotoa amtakaye na humuweka amtakaye katika njia iliyonyooka.”[7]

4- Uumbaji. Allaah anakiumba kila kitu na kukipa uundaji wake. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

إِنَّا كُلَّ شَيْءٍ خَلَقْنَاهُ بِقَدَرٍ

”Hakika sisi Tumekiumba kila kitu kwa Qadar.”[8]

Hizi ndio ngazi za Qadar. Ni mambo yamethibitishwa kwa Qur-aan na Sunnah kama ulivyojionea mwenyewe.

[1] 54:49

[2] 25:02

[3] Muslim (2653).

[4] Abu Daawuud (4700) na at-Tirmidhî (2155). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh-ul-Jaami´” (2017).

[5] 36:12

[6] 06:125

[7] 06:39

[8] 54:49

  • Mhusika: ´Allaamah Zayd bin Muhammad al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Latwiyfah ´alaa Usuwl-is-Sunnah al-Muniyfah, uk. 58-59
  • Imechapishwa: 03/10/2019