1. Shirki ya kwanza kujitokeza ulimwenguni


Mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) ameweka mlango huu kwa sababu picha ni sababu inayopelekea katika shirki ambayo ni kinyume cha Tawhiyd. Hivyo ndivo ilivyokuwa kwa watu wa Nuuh wakati walipotengeneza picha za watu wao wema na wakazitundika kwenye vikao vyao. Mwishowe wakaanza kuwaabudu badala ya Allaah.

Shirki ya kwanza iliojitokeza ardhini ni kwa sababu ya picha na vinyago. Kadhalika Ummah wa Ibraahiym (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) waliabudu masanamu vinyago. Vivyo hivyo wana wa israaiyl walimwabudu ndama waliotengenezewa na Samiyriy. Haya yanafahamisha  kuwa picha ni sababu ya kujitokeza kwa shirki na inapelekea katika shirki. Zikitengenezwa picha za viongozi, waja wema na wanachuoni na zikatundikwa basi hatimaye mwishowe huadhimishwa. Kisha shaytwaan huwajia watu na kuwashawishi kwamba wanaweza kunufaisha na kudhuru ambapo wanaanza kuziadhimisha, kutafuta baraka kwazo, wakazichinjia na wakaziwekea nadhiri. Hatimaye yakawa ni masanamu yanayoabudiwa badala ya Allaah. Hii ndio sababu ya mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) kuweka mlango huu kwenye “Kitaab-ut-Tawhiyd”. Kwa sababu kitabu hiki kinabainisha Tawhiyd, shirki na njia zinazopelekea katika shirki. Miongoni mwa njia kubwa zinazopelekea katika shirki ni kutengeneza picha na kuzining´iniza.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: I´aanat-ul-Mustafiyd bi Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 602
  • Imechapishwa: 05/09/2019