1. Familia salama zinachangia miji salama


Himdi zote ni Zake Allaah. Tunamhimidi Yeye na kumuomba msaada na msamaha. Tunaomba kinga kwa Allaah kutokamana na shari za nafsi zetu na matendo yetu maovu. Yule mwenye kuongozwa na Allaah, hakuna yeyote awezae kumpoteza, na yule mwenye kupotezwa na Allaah, hakuna yeyote awezae kumwongoza. Ninashuhudia ya kwamba hakuna yeyote mwenye haki ya kuabudiwa isipokuwa Allaah na nashuhudia ya kwamba Muhammad ni mja na ni Mtume Wake.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ حَقَّ تُقَاتِهِ وَلَا تَمُوتُنَّ إِلَّا وَأَنتُم مُّسْلِمُونَ

“Enyi mlioamini! Mcheni Allaah kama apasavyo kuogopwa na wala msife isipokuwa na nyinyi ni Waislamu.”[1]

يَا أَيُّهَا النَّاسُ اتَّقُوا رَبَّكُمُ الَّذِي خَلَقَكُم مِّن نَّفْسٍ وَاحِدَةٍ وَخَلَقَ مِنْهَا زَوْجَهَا وَبَثَّ مِنْهُمَا رِجَالًا كَثِيرًا وَنِسَاءً ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ الَّذِي تَسَاءَلُونَ بِهِ وَالْأَرْحَامَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلَيْكُمْ رَقِيبًا

“Enyi watu! Mcheni Mola wenu Ambaye Amekuumbeni kutokana na nafsi moja na Akaumba kutoka humo mke wake na Akaeneza kutoka hao wawili wanaume wengi na wanawake. Na mcheni Allaah Ambaye Kwake mnaombana na jamaa. Hakika Allaah Amekuwa juu yenu Mwenye kuchunga.”[2]

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ وَقُولُوا قَوْلًا سَدِيدًا يُصْلِحْ لَكُمْ أَعْمَالَكُمْ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ ۗ وَمَن يُطِعِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ فَازَ فَوْزًا عَظِيمًا

“Enyi mlaomini! Mcheni Allaah na semeni kauli ya kweli [ya sawasawa]. Atakutengenezeeni ‘amali zenu, na Atakusameheeni madhambi yenu; na anayemtii Allaah na Mtume Wake, basi kwa hakika amefanikiwa mafaniko makubwa.”[3]

Hakika maneno bora ni maneno ya Allaah na uongofu bora ni uongofu wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Shari ya mambo ya yenye kuzushwa. Kila chenye kuzushwa ni Bid´ah na kila Bid´ah ni upotevu na kila upotevu ni Motoni.

Tumekusanyika katika usiku huu, usiku wa Ijumaa, ambao ninamuomba Allaah Aubariki na wale walioko katika usiku huu na yale tunayoyasema ndani yake. Tumekusanyika juu ya jambo kubwa. Vipi lisiwe ni kubwa wakati linahusiana na familia ambayo katika jamii ina ngazi kama moyo kwenye mwili? Moyo ukiwa salama mwili mzima husalimika, na moyo ukiharibika mwili mzima huharibika. Vivyo hivyo huwa familia. Familia ikiwa salama mji mzima husalimika, na familia ikiharibika mji mzima huharibika. Vipi mada isiwe muhimu sana wakati inahusiana na utulivu wa mwanaadamu? Moyo wa mwanaadamu na uhai wake vikitulizana kadhalika ´ibaadah zake hutulizana. Humfanya akapata unyenyekevu katika Swalah zake na uchangamfu katika Swawm zake na njia za ´ibaadah zake hupata mwanga. Vipi mada isiwe ni ya sawa yenye kuzungumziwa na wanafunzi wakati inahusiana na mume na mke, mvulana na msichana, mtoto wa kiume na mtoto wa kike, wanandoa ambao wameshaoana na wale wanaopangilia kuoana? Kwa msemo mwingine inahusiana na jamii nzima na imethibitishwa katika Qur-aan na Sunnah.

Dini yetu ya Kiislamu ni rehema kwa walimwengu wote. Dini yetu ni yenye kheri, furaha, mafanikio na wema. Ujumbe wake ni wenye kuwanufaisha watu duniani na Aakhirah, kila siku na kila mahali. Mwanaadamu hawezi kupata furaha kokote isipokuwa katika dini ya mbora wa viumbe – dini ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Allaah (Ta´ala) Hakuamrisha kitu isipokuwa maamrisho hayo yana faida, manufaa na maslahi mengi. Allaah Hakukataza kitu isipokuwa makatazo hayo yana madhara na khasara nyingi.

Uislamu umetunza masuala yote ya maisha. Hakuna suala lolote katika maisha yako isipokuwa Uislamu umelibainisha na kuliweka wazi. Miongoni mwa hayo ni pamoja na Uislamu kutilia umuhimu wa kuitengeneza jamii na uwiano wake. Pale ilipokuwa ustawi wa jamii ni wenye kufuatana na ustawi wa familia, na pale ilipokuwa ustawi wa jamii ni matunda yanayopatikana katika ustawi wa familia, na pale ilipokuwa furaha ya familia imefungamana na ndoa, ndipo Uislamu ukawa umetilia umuhimu mkubwa juu ya ndoa. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) Ameamrisha ndoa katika Qur-aan na Kusema:

فَانكِحُوا مَا طَابَ لَكُم مِّنَ النِّسَاءِ مَثْنَىٰ وَثُلَاثَ وَرُبَاعَ ۖ فَإِنْ خِفْتُمْ أَلَّا تَعْدِلُوا فَوَاحِدَةً أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُكُمْ ۚ ذَٰلِكَ أَدْنَىٰ أَلَّا تَعُولُوا

“Basi oeni waliokupendezeni katika wanawake; wawili au watatu au wanne. Mkikhofu kuwa hamtoweza kufanya uadilifu, basi [oeni] mmoja au ambao mikono yenu ya kulia imewamiliki [masuriya]. Hivyo ni karibu zaidi kwamba hamtoelemea [kudhulumu].”[4]

Vilevile mwaminifu na mwenye kusadikishwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameamrisha hilo na kuwaambia vijana:

“Enyi vijana! Mwenye kuweza katika nyinyi kuoa basi na aoe. Hilo litamfanya aweze kushusha macho na ni utakaso wa tupu.”[5]

[1] 03:102

[2] 04:01

[3] 33:70-71

[4] 04:03

[5] al-Bukhaariy (5066) na Muslim (1400)

  • Mhusika: Shaykh Sulaymaan bin Saliym ar-Ruhayliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Haqq-uz-Zawjayn, uk. 6-8
  • Imechapishwa: 21/03/2017