09. Mazingatio yanayopatikana katika kisa cha mbedui aliyekojoa msikitini

Hebu wacha tuchume mafunzo katika kisa hiki.

1- Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) walipanda juu na wakamfokea mbedui huyu. Hapo tunapata funzo ya kwamba haijuzu kukinyamazia kitendo kiovu. Bali ni wajibu kukimbilia kumkataza yule mtenda maovu. Lakini ikiwa kule kukimbilia kukataza uovu huo kunapelekea katika jambo kubwa zaidi, basi inatakiwa kuwa na hekima mpaka yaondoke kwanza madhara haya makubwa. Kwa ajili hii ndio maana Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwakataza. Sivyo tu bali kumkemea na kumfokea mbedui huyu.

2- Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliamrisha kumwaga ndoo ya maji juu ya ule mkojo. Hapa kuna mafunzo ambayo lililo bora ni kukimbilia kuondosha madhara. Kuchelewa kuyaondosha kuna madhara pia. Ilikuwa ni jambo linalowezekana kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuchelewesha kusafisha sehemu hii ya msikiti mpaka pale watu watapohitajia kupaswalia ndipo akapasafisha kwa ajili hiyo. Lakini lililo bora ni mtu akimbilie kuondosha madhara ili baadaye asije kushindwa au akasahau. Hii ni nukta muhimu sana. Mtu anatakiwa kukimbilia kuondosha madhara kwa kuchelea asije kushindwa kuyaondosha huko mbele.

Kwa mfano lau nguo ya mtu – sawa iwe nguo hiyo anaswali nayo au haswali nayo – itaingiwa na najisi. Lililo bora ni yeye kuharakisha kuiosha najisi hii na asicheleweshe. Anaweza kusahau huko mbeleni au akashindwa kuiondosha ima kwa kukosa maji au kwa sababu nyingine isiyokuwa hiyo.

Kwa ajili hii pindi alipokuja mvulana kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo akampakata na tahamaki mtoto yule akamkojolea. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaamrisha kuletwe maji na akayamwaga juu ya ule mkojo papo hapo. Hakuchelewesha kuosha nguo yake mpaka wakati wa swalah kutokana na yale tuloyasema hivi karibuni.

4- Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimweleza mbedui huyu shani ya msikiti huu na kwamba umejngwa kwa ajili ya swalah, kusoma Qur-aan na kumdhukuru Allaah. Au alisema maneno kama hayo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kwamba haisihili ndani yake kitu katika dhara na taka. Kwa hiyo shani ya msikiti ni kuutukuza, kuusafisha, kuutwahirisha na yasifanywe ndani yake isipokuwa swalah, kusoma Qur-aan, kumdhukuru Allaah na mfano wa hayo ambayo yanamridhisha Allaah (Ta´ala).

5- Mtu atapowalingania wengine kwa hekima, upole na ulaini basi yanafikiwa malengo makubwa kuliko atapotaka kukiondosha kitu kwa ukali. Mbedui huyu alikinaika kikamilifu kwa yale aliyomfunza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mpaka akasema maneno haya yanayojulikana:

“Ee Allaah! Nihurumie mimi na Muhammad na usimuhurumie kati yetu mwengine yeyote.”

Utaona kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitangamana na mtu huyu kwa ulaini na upole. Ni jambo lisilokuwa shaka ya kwamba alikuwa ni mjinga. Haiwezekani kwa ambaye anajua utukufu wa misikiti na uwajibu wa kuiheshimisha akasimama mbele za watu na kukojoa pembezoni mwake.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Dawr-ul-Mar´ah fiy Iswlaah-il-Mujtama´ https://www.sahab.net/home/?p=806
  • Imechapishwa: 02/02/2017