Muislamu! Jifunze nyudhuru zinazomruhusu mtu kutofunga Ramadhaan:

1 – Maradhi

Imewekwa katika Shari´ah mgonjwa ambaye swawm inamtia uzito asifunge. Pale Allaah atakapomponya atalipa yale masiku yaliyo juu yake. Allaah (Subhaanah) amesema:

وَمَن كَانَ مَرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ

“Atakayekuwa mgonjwa au safarini basi atimize idadi katika siku nyinginezo.”[1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah anapenda zichukuliwe ruhusa Zake kama ambavyo anachukia kuasiwa.”[2]

Kwa sharti swawm iwe ni yenye kumdhuru mgonjwa. Iwapo itakuwa sio yenye kumdhuru haifai kwake akaacha kufunga kwa sababu hazingatiwi kuwa ni mwenye udhuru.

Ikiwa madaktari waaminifu watamjuza mgonjwa ya kwamba ana maradhi yasiyotarajiwa kupona itakuwa sio lazima kwake kufunga wala kulipa. Badala yake analazimika kumpa masikini chakula 1½ kg kwa kila siku moja ambayo hakufunga.

Inajuzu kutoa kafara yote mara moja sawa ikiwa itatolewa mwanzoni mwa Ramadhaan, mwishoni au katikati yake. Kafara hii anaweza kupewa fakiri mmoja au zaidi.

2 – Mimba na unyonyeshaji

Mjamzito na mnyonyeshaji wana hukumu moja kama mgonjwa. Iwapo swawm itakuwa ni yenye kuwadhuru imewekwa katika Shari´ah kuacha kufunga. Katika hali hii, ni kama mgonjwa, ni juu yao kulipa masiku waliyokula pindi wanapoweza. Baadhi ya wanachuoni wanasema inatosha kwa kila siku moja ambayo hawakufunga kumlisha masikini. Hata hivyo maoni haya ni dhaifu. Maoni sahihi ni kwamba ni wajibu kwao kuzilipa siku hizo kama msafiri na mgonjwa. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمَن كَانَ مَرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ

“Atakayekuwa mgonjwa au safarini.”[3]

Haya yanatolewa dalili na yale yaliyopokelewa na Anas bin Maalik al-Ka´biy kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliyesema:

“Allaah amemfanya msafiri kutofunga na kuswali swalah nusu na amemfanya mjamzito na mnyonyeshaji kuacha kufunga.”[4]

Wameipokea watano.

3 – Safari

Msafiri ana khiyari ya kufunga na kuacha kufunga. Udhahiri wa dalili za Kishari´ah zinaonyesha kuwa lililo bora ni kuacha kufunga hata kama swawm haitokuwa nzito kwake. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema:

وَمَن كَانَ مَرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ

“Atakayekuwa mgonjwa au safarini basi atimize idadi katika siku nyinginezo.”[5]

Kadhalika Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake walikuwa wakiacha kufunga safarini. Endapo vilevile atafunga ni sawa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa mara akifunga na mara akiacha kufunga safarini. Pindi Hamzah bin ´Amr al-Aslamiy alipomuuliza juu ya hilo akasema:

“Ukipenda funga na ukipenda acha kufunga.”[6]

Ni mamoja msafiri anasafiri kwa gari, ngamia, boti, meli au ndege. Zote hizo ni safari na kwa ajili hiyo wana haki ya kutendea kazi vile vyenye kuruhusiwa safarini.

Katika zama za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) Allaah (Subhaanah) aliwawekea waja Wake hukumu zinazohusiana na safari na ndani ya mji baada ya kufa kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mpaka siku ya Qiyaamah. Hakika Yeye (Subhaanah) anajua namna hali zitavyokuja kubadilika na kugeuka kwa vyombo vya usafiri. Lau hukumu ingebadilika basi (Subhaanah) angetuzindua kama Alivyosema katika Suurah “an-Nahl”:

وَنَزَّلْنَا عَلَيْكَ الْكِتَابَ تِبْيَانًا لِّكُلِّ شَيْءٍ وَهُدًى وَرَحْمَةً وَبُشْرَىٰ لِلْمُسْلِمِينَ

“Tumekuteremshia Kitabu chenye kubainisha kila kitu na ni mwongozo na Rahmah na bishara kwa waislamu.”[7]

وَالْخَيْلَ وَالْبِغَالَ وَالْحَمِيرَ لِتَرْكَبُوهَا وَزِينَةً ۚ وَيَخْلُقُ مَا لَا تَعْلَمُونَ

“[Ameumba vilevile] farasi na nyumbu na punda ili muwapande na wawe mapambo. Anaumba [pia] msivyovijua.”[8]

Muislamu akitambua kuwa endapo ataacha kufunga itakuwa uzito kuilipa siku hiyo aliyoacha kuifunga kwa sababu ya safari na hivyo akaamua kufunga siku hiyo, ni sawa na hakuna neno. Haijalishi kitu sawa chombo cha usafiri kikiwa ni chepesi au kizito kwa sababu dalili zimeachiwa.

Joto likiwa jingi na ikawa kuna uzito mkubwa itakuwa kumekokotezwa kukata swawm. Katika hali hii itakuwa imechukizwa kwa msafiri kufunga. Wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipomuona mtu ambaye alikuwa msafiri na amefunga anakota kivuli kwa sababu ya joto jingi, alimwambia:

“Sio wema kufunga katika safari.”[9]

Imethibiti vilevile ya kwamba (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah anapenda zichukulie ruhusa Zake kama ambavyo anachukia kuasiwa.”[10]

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Allaah anapenda zichukuliwe ruhusa Zake kama ambavyo anapenda maamrisho Yake yatendewe kazi.”[11]

TANBIHI

Iwapo msafiri ataacha kufunga na akatua katika mji usiokuwa mji wake sio lazima kwake kuanza kufunga ikiwa hakupangilia kubaki hapo siku nne au chini ya hapo. Lakini hata hivyo haifai kwake kufanya mambo yanayoharibu swawm mbele ya watu wa mji ilihali hawajui hali yake. Anachotakiwa ni yeye ajifiche ili asije kutuhumiwa kufanya kitu alichoharamisha Allaah na ili asije kuwafanya wengine kuwa na ujasiri wa kumuiga.

Ama ikiwa msafiri ambaye hakufunga amepangilia kutua katika mji zaidi ya siku nne anatakiwa kujizuia na siku hiyo pale tu atapotua katika mji na atailipa siku hiyo. Anatakiwa kufunga iliyobaki, kwa sababu kwa nia ya kutua hapo zaidi ya siku nne wanachuoni wengi wanaonelea kuwa ana hukumu ya wakazi na sio ya wasafiri.

4 – Hedhi

Pindi mwanamke anapopata hedhi anaacha kuswali na kufunga. Atapotwaharika atalipa zile siku alizokula katika Ramadhaan na hatolipa swalah. al-Bukhaariy na wengine wamepokea kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema pindi alipokuwa akibainisha upungufu wa dini wa mwanamke:

“Pindi mmoja wenu anapopata hedhi si anaacha kuswali na kufunga?”[12]

Vilevile al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kutoka kwa Mu´aadhah ya kuwa alimuuliza  ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ni kwa nini mwanamke mwenye hedhi analipa swawm na halipi swalah. ´Aaishah akamuuliza:

“Je, wewe ni Haruuriyyah?”

Akasema:

“Mimi sio Haruuriyyah. Nauliza tu.”

Ndipo ´Aaishah akasema:

“Tulikuwa tukipata hedhi wakati wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Tulikuwa tukiamrishwa kulipa swawm na si swalah.”[13]

Ameipokea al-Bukhaariy, Muslim na wengineo.

Hii ni rehema na upole wa Allaah kwa mwanamke. Kwa kuwa swalah inakariri mchana na usiku mara tano na mara nyingi hedhi inatokea mara moja kwa mwezi ndipo Allaah akamfutia uwajibu wa kulipa swalah kutokana na uzito mkubwa unaopatikana katika kitendo hicho. Ilipokuwa swawm haikariri isipokuwa mara moja kwa mwaka ndipo Allaah akamuamrisha kuacha kufunga kipindi yuko na hedhi kwa kumuhurumia. Baada ya hapo ni lazima kwake kulipa masiku aliyokula kwa ajili ya kuhakikisha maslahi ya Kishari´ah.

5 – Nifasi

Nifasi ni damu inayotoka kwa sababu ya uzazi. Maadamu mwanamke anaona damu siku arubaini baada ya kuzaa asiswali wala kufunga. Katika kipindi hicho si halali kwa mumewe kumwingilia mpaka atwaharike au zikamilike siku arubaini.

Iwapo damu itaendelea baada ya kutimiza siku arubaini aoge ile siku ya arubaini. Kwa sababu maoni sahihi ni kuwa nifasi haizidi siku arubaini. Kwa hiyo aoge na kuswali. Ni halali kwa mumewe kumwingilia. Atumie pamba na vitu vyenginevyo ili kuizuia damu isiguse nguo na mwili wake. Hukumu ya damu hii ni ya ugonjwa isiyomzuia na swalah, swawm na jimaa. Katika hali hii ni juu yake kutawadha kunapoingia wakati wa kila swalah.

Upande mwingine mwanamke akitwaharika kabla ya siku arubaini aoge, aswali na afunge. Mwanamke huyo atakuwa ni halali pia kwa mumewe hata kama kumepita tu siku chache. Endapo damu itarudi ndani ya siku arubaini ataacha kuswali na kufunga. Atakuwa pia si halali tena kwa mumewe mpaka ima atwaharike au akamilishe siku arubaini.

TANBIHI

Istihadha ni damu ya ugonjwa inayomtoka mwanamke ambayo si hedhi wala nifasi. Hukumu ya damu hii ni safi. Katika hali hii anatakiwa kufunga na kuswali na ni halali kwa mumewe kumwingilia pindi yuko na damu hii. Anatakiwa kutawadha wakati wa kila swalah kama ambaye yuko na hadathi yenye kuendelea. Ni juu yake kujihifadhi na damu kwa kutumia pamba au kitu kingine ili isichafue mwili wala nguo yake. Kitendo hichi kimesihi kupokelewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

6- Kushindwa kwa sababu ya utu-uzima

Ikiwa mwanaume na mwanamke ni watuwazima kiasi cha kwamba swawm ni nzito kwao waache kufunga na badala yake wamlishe masikini kwa kila siku moja ambayo hawakufunga. Ima wanaweza kuwaacha wakachangia chakula pamoja nao au wampe masikini 1½ kg ya tende, ngano au mchele kwa kila siku moja ambayo hakufunga. Ikiwa pamoja na hayo wanasumbuliwa na vidonda au maradhi mengine, hakika wanatakiwa kuacha kufunga. Wala itakuwa sio wajibu kwao kulisha kwa kuwa wameacha kufunga kwa sababu ya maradhi na sio kwa sababu ya utu-uzima. Wakipona watalipa zile siku ambazo hawakufunga.

Ikiwa hawawezi kulipa siku walizoacha kwa sababu ya utu-uzima watalisha kwa kila siku moja masikini kama ilivyotangulia kutajwa. Hivyo ndivyo alivyofutu Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) na wanachuoni wengine. Dalili ya hilo zinajulikana. Miongoni mwazo maneno ya Allaah (Ta´ala):

وَمَن كَانَ مَرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ

“Atakayekuwa mgonjwa au safarini basi atimize idadi katika siku nyinginezo.”[14]

Mtumzima ambaye si muweza hawezi kulipa. Kwa hiyo ni wajibu kwake kulisha chakula badala ya hilo. Pindi Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ´anh), mfanya kazi wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), alipokuwa mtumzima na swawm ikawa nzito kwake aliacha kufunga na badala yake akalisha chakula kwa kila siku moja ambayo hakufunga masikini. Ama ikiwa mtu akili imempotea haimlazimu si kulisha wala kitu kingine.

Ninamuomba Allaah (´Azza wa Jall) atutunuku sisi, nyinyi na waislamu wengine wote kuweza kuifahamu dini na kuwa na msimamo juu yake na atulinde sisi sote kutokamana na shari ya nafsi zetu na matendo yetu maovu. Hakika Yeye ni muweza juu ya hilo.

Swalah na amani zimwendee mja na Mtume Wake, Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah wake.

[1] 02:185

[2] Ahmad (5866), al-Bayhaqiy (5201) na wengine. Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Irwaa’-ul-Ghaliyl” (564).

[3] 02:185

[4] at-Tirmidhiy (715), an-Nasaa’iy (2275), Ibn Maajah (1667) na Ahmad (20341). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh Ibn Maajah” (1353).

[5] 02:185

[6] al-Bukhaariy (1943) na Muslim (1121).

[7] 16:89

[8] 16:08

[9] al-Bukhaariy (1946).

[10] Ahmad (5866), al-Bayhaqiy (5201) na wengine. Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Irwaa’-ul-Ghaliyl” (564).

[11] Ahmad (5866), al-Bayhaqiy (5201) na wengine. Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Irwaa’-ul-Ghaliyl” (564).

[12] al-Bukhaariy (304) na Muslim (80).

[13] al-Bukhaariy (321) na Muslim (335).

[14] 02:185

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Mufiyd fiy Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 31-35
  • Imechapishwa: 02/04/2022