Swali 8: Je, mtu achanganyike na makundi mbalimbali au ayasuse?

Jibu: Ikiwa yule anayechanganyika nao yuko na elimu na utambuzi[1] na akachanganyika nao kwa lengo la kuwalingania katika Sunnah na kuacha kosa, ni jambo zuri. Ni katika aina ya kulingania katika dini ya Allaah. Lakini ikiwa mtu anachanganyika nao ili kufarijika nao na kuwa na kufanya urafiki nao bila ya kuwalingania na kuwabainishia, haijuzu.

Haijuzu kwa mtu kuchanganyika na wahalifu ikiwa hilo halileti faida inayokubalika kwa mujibu wa Shari´ah kama vile kuwalingania katika Uislamu sahihi na kuwabainishia haki ili waweze kujirejea[2]. Mfano wa hilo ni kama jinsi Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) alivoenda wazushi msikitini na kuwakemea kwa Bid´ah zao. Mfano mwingine ni Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) alivowaendea Khawaarij na kujadiliana nao na kuzivunja hoja zao tata. Kuna ambao walijirejea.

Ikiwa kuchanganyika nao ni kwa lengo hili ni sawa. Lakini wakiendelea kung´ang´ania upotevu wao ni wajibu kujiepusha nao na kupambana nao katika njia ya Allaah.

[1] Hili ni sahihi inapokuja kwa mtu mmojammoja. Ni jambo linalowezekana kuwalingania na kuwaathiri. Hata hivyo ni jambo lisilowezekana kwa jumla kubadilisha mfumo na viongozi wao. Bali wao ndio wanaoweza kumuathiri yule mwenye kuchanganyika nao bila ya wao kuathirika. Inapokuja katika ulinganizi wenyewe, kwa jumla mapote haya hayaachi mafundisho ya viongozi wao. Mfano wa mapote haya ni al-Ikhwaan al-Muslimuun na Jamaa´at-ut-Tabliygh. Ni nasaha ngapi wameshapata kutoka kwa watu wakweli! Ni mara ngapi kumeandikwa juu yao! Pamoja na yote haya bado wamesimama palepale. Hapa unayo dalili ya yale niyasemayo. Muasisi wa al-Ikhwaan al-Muslimuun Hasan al-Bannaa amesema chini ya kichwa cha khabari “Mawqiyfunaa min ad-Da´waat”:

“Msimamo wetu juu ya linganizi mbalimbali ni kwamba sisi tunazipima kwa mizani ya ulinganizi wetu; yale yanayoafikiana nayo tunayakaribisha na yale yasiyoafikiana nayo sisi ni wenye kujiweka nayo mbali.” (Majmuu´-ur-Rasaa-il, uk. 24)

Ee Allaah! Shuhudia ya kwamba mimi ni mwenye kujiweka mbali na ulinganizi wa al-Ikhwaan al-Muslimuun na mwanzilishi wake. Kwa sababu ni wenye kwenda kinyume na Qur-aan, Sunnah na mfumo wa Salaf.

Kutokana na haya wao hawakubali ulinganizi wa yeyote. Kwa sababu wao wanachotaka ni linganizi za wengine zifuate ulinganizi wao na ziwe chini yao – na Allaah ndiye anajua zaidi.

[2] Ikiwa mtu kweli amelazimika kuchanganyika nao ili kuwalingania katika mfumo wa Salaf, basi wanazuoni pekee au wanafunzi walio madhubuti katika ´Aqiydah sahihi, Sunnah na mfumo wa Salaf ndio wanaotakiwa kufanya hivo na si mwingine.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ajwibah al-Mufiydah ´an As-ilat-il-Manaahij al-Jadiydah, uk. 29-30
  • Imechapishwa: 18/02/2017