Suala la saba: Wakati wa nia katika funga na hukumu yake

Ni lazima kwa mfungaji anuie kufunga. Ni nguzo miongoni mwa nguzo zake, kama ilivyotangulia. Hilo ni kutokana na maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakika kila kitendo kinategemea na nia na kila mmoja atalipwa kwa kile alichonuia.”

Swawm ya wajibu ni lazima aweke nia wakati wa usiku. Mfano wa swawm hizo ni swawm ya Ramadhaan, swawm ya kafara, swawm ya kulipa na ya nadhiri. Ni lazima aweke nia ijapo dakika moja kabla ya kuingia kwa alfajiri. Hilo ni kutokana na maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Asiyelala na [nia ya] swawm kabla ya Fajr swawm yake haisihi.”[1]

Mwenye kunuia kufunga wakati wa mchana, licha ya kuwa hajatumia kitu, haisihi isipokuwa katika funga ya sunnah. Inafaa kwake kuweka nia mchana. Kwa sharti asiwe ametumia kitu katika chakula au kinywaji. Hilo ni kutokana na Hadiyth ya ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) aliyesema:

“Siku moja Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliingia nyumbani kwangu na akasema:

“Je, mna chochote?” Tukasema: “Hapana.” Akasema: “Basi mimi nimefunga.”[2]

Kuhusu swawm ya lazima nia haifunguki kwa kuwekwa mchana. Ni lazima kuweka nia wakati wa usiku.

Inatosha kuweka nia moja mwanzoni mwa Ramadhaan kwa ajili ya mwezi mzima. Imependekezwa kuiweka upya kila siku.

[1] at-Tirmidhiy (733), an-Nasaa´iy (04/196) na Ibn Maajah (1700) na tamko ni la an-Nasaa´iy. Ni Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy. Tazama ”Swahiyh-ut-Tirmidhiy” (583).

[2] Muslim (1154).

  • Mhusika: Nukhbatin minal-´Ulamaa´
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fiqh-ul-Muyassar, uk. 153
  • Imechapishwa: 16/04/2020