07. Ushirikiano wa majina haupelekei kufanana

Vilevile ana sifa za kidhati kama mfano wa uso, mikono na sifa nyenginezo za ukamilifu. Tunamthibitishia Allaah yale aliyojisifia Mwenyewe na yale aliyojisifiwa na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ni mamoja katika sifa za kidhati na sifa za matendo. Hatuingizi akili zetu na maono na fikira zetu wenyewe na kusema kwamba majina na sifa hizi zinapatikana kwa watu na kwamba tukizithibitisha tutakuwa tunamfananisha na watu. Hivo ndivo wanavosema Mu´attwilah. Bali tunasema kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ana majina na sifa zinazolingana tu na utukufu Wake na viumbe wana majina na sifa zinazolingana nao. Ushirikiano wa majina na maana haupelekei ushirikiano katika uhakika. Kwa mfano Peponi kuna zabibu, mitende, makomamanga na vyenginevyo ambavyo majina yake yanafanana na vitu vilivyoko hapa duniani. Lakini vilivyoko Peponi havifanani kabisa na vilivyoko hapa duniani. Mitende ilioko Peponi haifanani na mitende ilioko duniani. Makomamanga ilioko Peponi haifanani na makomamanga ilioko duniani japokuwa ni vyenye kushirikiana katika majina. Hata hivyo uhakika na namna zake ni zenye kutofautiana. Kadhalika majina na sifa za Allaah japokuwa ni venye kushirikiana na majina ya viumbe; uhakika na namna zake ni zenye kutofautiana. Hakuna yeyote mwenye kuyajua isipokuwa Allaah pekee. Kwa hivyo hakuna kufanana kokote, kwa sababu hakuna yeyote anayefanana na Muumbaji (Subhaanah) kama alivosema:

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.”[1]

[1] 42:11

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: I´aanat-ul-Mustafiyd bi Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 24
  • Imechapishwa: 22/07/2019