Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili ni maneno Yake (Ta´ala):

وَالْعَصْرِ إِنَّ الْإِنسَانَ لَفِي خُسْرٍ إِلَّا الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ وَتَوَاصَوْا بِالْحَقِّ وَتَوَاصَوْا بِالصَّبْرِ

 “Naapa kwa al-‘Aswr. Hakika ya mwanadamu bila shaka yumo katika khasara, isipokuwa wale walioamini na wakatenda mema na wakausiana kwa haki na wakausiana subira.” (al-´Aswr 103 : 01-03)

MAELEZO

Dalili – Bi maana dalili ya masuala haya manne ni maneno Yake (Ta´ala):

وَالْعَصْرِ

“Naapa kwa al-´Aswr”

Katika Suurah hii Allaah (´Azza wa Jall) ameapa kwa alasiri ambayo ni zama ambapo ndani yake kunatokea matukio ya kheri na shari. Allaah (´Azza wa Jall) ameapa kwa zama ya kwamba kila mwanadamu yumo katika khasara, isipokuwa wale wanaosifika na sifa hizi nne; imani, matendo mema, kuusiana kwa haki na kuusiana kwa subira. Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) amesema:

“Kupambana na nafsi na nafsi ni jambo lina ngazi nne;

1- Kupambana nayo juu ya kuifunza uongofu na dini ya haki ambayo ndio njia ya kufaulu na furaha duniani na Aakhirah.

2- Kupambana nayo juu ya kutenda kazi kwa mujibu wa elimu.

3- Kupambana nayo juu ya kulingania katika dini ya haki na kuwafundisha wale ambao ni wajinga.

4- Kupambana nayo juu ya kuwa na subira kwa ajili ya Allaah kwa yale mashaka na maudhi ya viumbe wakati anapolingana katika dini ya Allaah.

Sifa hizi nne zinapokusanyika kwa mtu, basi anakuwa katika wale wanaoishi kwa mfumo wa kiungu.”

Allaah (´Azza wa Jall) ameapa katika Suurah hii ya kwamba kila mtu yumo katika khasara pasi na kujali ni mali na watoto kiasi gani alionao na pasi na kujali ni cheo na heshima kiasi gani alionayo. Isipokuwa yule mtu ambaye anasifika kwa sifa hizi nne;

1- Imani. Kunaingia kila ´Aqiydah sahihi na elimu yenye manufaa inayomkurubisha mtu kwa Allaah (Ta´ala).

2- Matendo mema. Kunaingia kila neno na tendo ambalo linamkurubisha mtu kwa Allaah. Kwa sharti mtendaji awe amemtakasia nia Allaah na ni mwenye kumfuata Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

3- Kuusiana kwa haki. Nako ni kule mtu kuitana na kuhimizana katika matendo mema.

4- Kuusiana kuwa na subira kwa baadhi kuwausia wengine kuwa na subira ya kutekeleza maamrisho ya Allaah (Ta´ala), kujiepusha na makatazo ya Allaah na kuwa na subira ya makadirio ya Allaah.

Kuusiana kwa haki na kuusiana subira kunakusanya kuamrishana mema na kukatazana maovu, mawili ambayo ndio yenye kuifanya dini kusonga mbele na sababu ya mafanikio yake na nusura na kufikia heshima na utukufu:

كُنتُمْ خَيْرَ أُمَّةٍ أُخْرِجَتْ لِلنَّاسِ تَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَتَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ وَتُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ

“Mmekuwa Ummah bora kabisa ulioteuliwa kwa watu: mnaamrisha mema na mnakataza maovu na mnamwamini Allaah.” (Aal ´Imraan 03 : 110)

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 25-26
  • Imechapishwa: 16/05/2020