07. Sababu ya nne: mwanaume kuisimamia familia yake

Miongoni mwa sababu familia kupata furaha ni mwanaume amsimamie mke wake na aichunge familia yake. Allaah (Subhanaahu wa Ta´ala) anasema katika Kitabu Chake kitukufu:

الرِّجَالُ قَوَّامُونَ عَلَى النِّسَاءِ بِمَا فَضَّلَ اللَّـهُ بَعْضَهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ وَبِمَا أَنفَقُوا مِنْ أَمْوَالِهِمْ

“Wanaume ni wasimamizi wa wanawake kwa kuwa Allaah amefadhilisha baadhi yao kuliko wengine na kwa sababu ya matumizi wanayotoa katika mali zao.” 04:34

Usimamizi huu ni katika mazuri ya Uislamu na ni katika utimilifu wa neema za Allaah (´Azza wa Jall) juu yetu. Kwa kuwa ndani yake kuna kheri kubwa na ni jambo linaafikiana na maumbile ya mume na mke. Usimamizi ina maana mume asimame na yale yatayotengeneza shani ya mke wake. Shaykh Ibn Sa´diy (Rahimahu Allaah) amesema:

“Allaah (Ta´ala) anaelezea kuwa wanaume ni wasimamizi wa wanawake. Bi maana ni wenye kuwasimamia kwa kuwalazimisha haki za Allaah (Ta´ala) katika kuzihifadhi faradhi Zake na kuwazuia na madhara. Ni juu ya wanaume kuwalazimisha hayo. Ni wasimamizi wao pia kwa kuwapa matumizi, mavazi na makazi.”[1]

´Abdullaah bin ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema: “Nimemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema: “Nyote ni wachunga na nyote mtaulizwa juu ya kile mlichokichunga. Mwanaume ni mchunga juu ya familia yake na yeye ataulizwa juu ya kile alichokichunga. Mwanamke ni mchunga nyumbani kwa mume wake na ataulizwa juu ya kile alichokichunga.” al-Bukhaariy (893) na Muslim (1829).

Mwanaume ni mchungaji wa familia. Ni wajibu kwake kusimamia yale yenye kuwatengeneza. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakuna mja yeyote Allaah atamchungisha wachungwa na akafa ilihali ni mwenye kuwaghushi wale wachungwa wake isipokuwa Allaah atamharamishia Pepo.” al-Bukhaariy (7151), (7150) na Muslim (142) na matamshi ni ya kwake.

Hakuna mja yeyote… – Anaingia kila mja.

Allaah atamchungisha wachungwa… – Wachungwa wowote hata kama atakuwa mchungwa mmoja tu.

akafa ilihali ni mwenye kuwaghushi wale wachungwa wake… – Bi maana hakuwapa nasaha.

isipokuwa Allaah atamharamishia Pepo – Haya yanafahamisha kuwa ni katika madhambi makubwa ambayo yanamkasirisha Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).

[1] Tafsiyr ya as-Sa´iyd, uk. 177.

  • Mhusika: Shaykh Sulaymaan bin Saliymillaah ar-Ruhayliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Asbaab sa´aadat-il-Usrah, uk. 27-29
  • Imechapishwa: 08/10/2016