07. Jiandae kufa na kufinywa ndani ya kaburi

[11] Inatakiwa kuamini adhabu ya ndani ya kaburi na Munkar na Nakiyr. Allaah (Ta´ala) amesema:

فَإِنَّ لَهُ مَعِيشَةً ضَنكًا

“Basi hakika atapata maisha ya dhiki kabisa.”[1]

Wafasiri wa Qur-aan wamesema:

”Bi maana adhabu ya ndani ya kaburi.”

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema kumwambia ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh):

”Ee ´Umar! Hali ingelikuwa vipi endapo ungeliona fitina za Malaika wawili wa kaburi? Ni weusi na wana macho ya bluu na kama umeme na sauti yao ni kama radi. Wanaingia kwenye nywele zao na wanachimba kwa meno yao ya kuchimba. Mikononi mwao wana nyundo za vyuma. Lau wangeliwapiga watu na majini, basi wangelikufa.” ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) akasema: ”Siku hiyo nitakuwa na hali gani?” Akasema: ”Katika hali yako hiyohiyo ulionayo.” Akasema: ”Basi nitakutosheleza nao, ee Mtume wa Allaah!”[2]

Umm Khaalid (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesimulia:

”Nilimsikia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akiomba kinga dhidi ya adhabu ya kaburi.”[3]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Lau angelikuweko yoyote atakayeokoka na mbano wa kaburi, basi angeliokoka Sa´d bin Mu´aadh ambaye ´Arshi ya Mwingi wa rehema ilitikisika kwa ajili yake.”[4]

Halafu baada ya hapo mtu anatakiwa kuamini sauti ya parapanda kutoka kwa Israafiyl kwa ajili ya kufufuka kutoka ndani ya makaburi. Ulazimishe moyo kwamba utakufa na utabanwa ndani ya kaburi. Ni wajibu pia kuamini kuwa mtu atahojiwa ndani ya kaburi na atafufuliwa baada ya kufa. Mwenye kuyakanusha haya ni kafiri.

[1] 20:124

[2] al-Bayhaqiy katika ”Ithbaat ´Adhaab-il-Qabr” (116–117) na Ibn Abiy Daawuud katika ”al-Ba´th” (7).

[3] al-Bukhaariy (6364) na Muslim (584).

[4] Ahmad (6/55).

  • Mhusika: Imaam Abul-Husayn Muhammad bin Abiy Ya´laa al-Hanbaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-I´tiqaad, uk. 32
  • Imechapishwa: 25/02/2019