Kuhusiana na matendo ni lazima kuzitendea kazi Sunnah ambazo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameziwajibisha, kama ambavyo ni lazima kuitendea kazi Qur-aan katika yale ambayo Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amewajibisha. Vivyo hivyo kuhusiana na makatazo na hukumu zengine zilizobaki.

Ni lazikam kuitakidi kwa kukata ya kwamba Sunnah ni Wahy kama Qur-aan tukufu na kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakusema jambo lolote la kidini kutoka kichwani mwake mwenyewe; alikuwa ni mwenye kusubiri ateremshiwe na Allaah ili aweze kufikisha. Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amemsifu katika Aayah nyingi kukiwemo:

وَالنَّجْمِ إِذَا هَوَىٰ مَا ضَلَّ صَاحِبُكُمْ وَمَا غَوَىٰ وَمَا يَنطِقُ عَنِ الْهَوَىٰ إِنْ هُوَ إِلَّا وَحْيٌ يُوحَىٰ

“Naapa kwa nyota zinapotua. Hakupotoka swahibu wenu na wala hakukosea. Wala hatamki kwa matamanio yake. Hayo si chochote isipokuwa ni Wahy unaofunuliwa.”[1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema wakati alipokuwa akibainisha nafasi na kiwango cha Sunnah:

“Hakika mimi nimepewa Qur-aan na kitu kingine mfano wake.”

Bi maana Qur-aan tukufu.

Hata kama Qur-aan ina sifa zake maalum na za kipekee, lakini vyote viwili Qur-aan na Sunnah ni Wahy kutoka kwa Allaah (Tabaarak wa Ta´ala). Kadhalika ni wajibu kutendea kazi mambo yake ya wajibu, ni mamoja yamo ndani ya Qur-aan au ndani ya Sunnah. Utumiaji wa dalili wa Sunnah ni kama utumiaji wa dalili wa Qur-aan. Huu ndio mfumo wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Hawako kama wale ambao shaytwaan amechezea akili zao ambao wanatendea kazi tu yale yaliyomo ndani ya Qur-aan. Ni kama vile wanaona kuwa hawana haja ya Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Huu ni upotevu wa wazi kwa sababu Sunnah inahitajika vikubwa kama inavyohitajika Qur-aan. Qur-aan tukufu imeelekeza kuitendea kazi na kuitilia umuhimu Sunnah. Amesema (´Azza wa Jall):

وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا

”Kile alichokupeni Mtume basi kichukueni na kile alichokukatazeni basi kiacheni.”[2]

Upande mwingine Allaah ametahadharisha kumuasi mja na Mtume Wake Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika yale aliyofikisha kutoka katika Qur-aan na Sunnah. Amesema (Subhaanah):

فَلْيَحْذَرِ الَّذِينَ يُخَالِفُونَ عَنْ أَمْرِهِ أَن تُصِيبَهُمْ فِتْنَةٌ أَوْ يُصِيبَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ

“Basi watahadhari wale wanaokhalifu amri yake; isije kuwapata fitina au ikawapata adhabu iumizayo.”[3]

Kwa haya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah siku zote wameona kuwa Sunnah ni Wahy wa pili.

Sehemu ya Sunnah inaibainisha Qur-aan kama tulivyotangulia kusema. Sunnah yote ni bora, timilifu na imekokotezwa; kisomo chake, hukumu na matendo. Kadhalika Qur-aan tukufu inaokokoteza Sunnah, inaamrisha iweze kufuatwa na kuwashaji´isha watu kwayo. Ni jambo lisilowezekana mtu akajitosheleza na Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Haijuzu kubishana nayo. Haijuzu kuamini kwamba mtu anaweza kujitosheleza nayo. Ni wajibu Sunnah ikatambuliwa, ikatendewa kazi na kusomwa.

Hatumjui mtu yeyote kutoka katika Ahl-us-Sunnah ambaye anaichukulia wepesi Sunnah au kuipuuza. Bali wanaizingatia kuwa Sunnah ni Wahy kutoka kwa Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) ambayo ni wajibu kuiadhibisha na kuiheshimu na kutendea kazi hukumu zake kama zinavyotendewa kazi hukumu za Qur-aan. Zipo Hadiyth nyingi zinazoonyesha namna ambavyo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anauamrisha Ummah kuonyesha shukurani juu ya Qur-aan na Sunnah. Katika hayo amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mimi nakuachieni yale ambayo midhali mtashikamana nayo barabara basi hamtopotea; Kitabu cha Allaah na Sunnah zangu.”[4]

Huu ndio mfumo waliokuwa nao Salaf na wafuasi wao, katika kila zama na mahali.

[1] 53:1-4

[2] 59:07

[3] 24:63

[4] Maalik (1594) na al-Haakim (1/171).

  • Mhusika: ´Allaamah Zayd bin Muhammad al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Latwiyfah ´alaa Usuwl-is-Sunnah al-Muniyfah, uk. 29-30
  • Imechapishwa: 01/10/2019