Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Suala la nne: Kusubiri juu ya maudhi yatakayompata mtu ndani yake.

MAELEZO

Subira ni kuichunga nafsi iweze kumtii Allaah, kuiweka mbali na kumuasi Allaah na kutokukasirikia Qadar za Allaah. Kwa njia ya kwamba mtu akaizuia nafsi kutokamana na kukasirika, kukereka na kuchoka na badala yake siku zote akawa ni mchangamfu katika kulingania katika Uislamu hata kama atakumbwa na maudhi. Kwa sababu kuwaudhi wale wanaolingania katika kheri ni katika maumbile ya watu isipokuwa yule aliyeongozwa na Allaah. Allaah (Ta´ala) amesema akimwambia Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

وَلَقَدْ كُذِّبَتْ رُسُلٌ مِّن قَبْلِكَ فَصَبَرُوا عَلَىٰ مَا كُذِّبُوا وَأُوذُوا حَتَّىٰ أَتَاهُمْ نَصْرُنَا

“Kwa hakika walikadhibishwa Mitume kabla yako wakasubiri juu ya yale waliyokadhibishwa na wakaudhiwa mpaka ilipowafikia nusura Yetu.” (al-An´aam 06 : 34)

Kila pale ambapo maudhi yatakuwa na nguvu zaidi, basi nusura inakurubia. Hata hivyo nusura haikuwekewa kikomo kwa mtu kunusuriwa katika maisha yake na akaona athari ya Da´wah yake imetimia, bali nusura inaweza kuja hata baada ya kufa. Hili linapatikana kwa njia ya kwamba Allaah akafanya watu kukubali yale ambayo siku moja alikuwa akiwalingania kwayo ambapo baadaye wakayapokea na kushikamana nayo barabara. Hili pia huzingatiwa kuwa ni nusura kwa mlinganizi huyu hata kama atakuwa ameshakufa.

Kwa ajili hiyo ni lazima kwa mlinganizi awe ni mvumilivu juu ya Da´wah yake na mwenye kuendelea kulingania katika dini ya Allaah (´Azza wa Jall). Pia anapaswa awe mwenye subira kwa vile vipingamizi ambavyo vitajitokeza na maudhi yatakayompata. Hawa hapa Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) walifanyiwa maudhi kwa maneno na kwa matendo. Allaah (Ta´ala) amesema:

كَذَٰلِكَ مَا أَتَى الَّذِينَ مِن قَبْلِهِم مِّن رَّسُولٍ إِلَّا قَالُوا سَاحِرٌ أَوْ مَجْنُونٌ

“Ndio kama hivyo, hawakuwafikia wale wa kabla yao Mtume yeyote yule isipokuwa walisema: “Mchawi au mwendawazimu.” (adh-Dhaariyaat 51 : 52)

وَكَذَٰلِكَ جَعَلْنَا لِكُلِّ نَبِيٍّ عَدُوًّا مِّنَ الْمُجْرِمِينَ

“Na hivyo ndivyo Tumemfanyia kila Nabii adui miongoni mwa wahalifu.” (al-Furqaan 25 : 31)

Lakini hata hivyo mlinganizi anatakiwa akabiliane nayo kwa subira. Tazama maneno ya Allaah (´Azza wa Jall) akimwambia Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

إِنَّا نَحْنُ نَزَّلْنَا عَلَيْكَ الْقُرْآنَ تَنزِيلًا

“Hakika Sisi tumekuteremshia Qur-aan uteremsho wa hatua kwa hatua.” (al-Insaan 76 : 23)

Pengine jambo lililokuwa linatarajiwa hapa aambiwe kushukuru neema ya Mola Wake, lakini badala yake Allaah (´Azza wa Jall) akasema:

فَاصْبِرْ لِحُكْمِ رَبِّكَ

“Hivyo basi, subiri hukumu ya Mola wako.” (al-Insaan 76 : 24)

Hapa kuna ishara ya kuwa kila atakayesimama kidete kwa Qur-aan, basi ni lazima yampate yeye yale yanayohitajia subira. Tazama hali ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati walipompiga watu wake na wakamtoa damu na huku anafuta damu usoni mwake na wakati huohuo anasema:

“Ee Allaah, wasamehe watu wangu! Kwani hakika hawajui.”[1]

Kwa ajili hiyo ni lazima kwa mlinganizi awe ni mwenye subira na mwenye kutarajia malipo.

Subira imegawanyika sehemu tatu:

1- Subira katika kumtii Allaah.

2- Subira kwa kujitenga na yale aliyoharamisha Allaah.

3- Subira juu ya Qadar ya Allaah ambayo inapitika ima pasi na chumo na taathira ya mja, au ambayo Allaah anayafanya kupitia kwa baadhi ya waja katika maudhi na mashambulizi.

[1] al-Bukhaariy (3477), Muslim (1792), Ibn Maajah (4025), Ahmad (1/380), Ibn Hibbaan (969) na Abu ´Awaanah (4/313).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 24-25
  • Imechapishwa: 16/05/2020