06. Mke mwema anatakiwa kumtii mume na mwenye maafikiano na mchangamfu


Katika sifa za mke mwema ni yale yaliyopokelewa katika “as-Sunan” ya al-Bayhaqiy[1] kupitia kwa Abu Udhaynah ambaye amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Wabora wa wanawake wenu ni wale wenye mahaba na wenye rutuba walio na maafikiano na wanausia juu ya kumcha Allaah. Waovu wa wanawake wenu ni wale wenye kuonyesha mapambo yao na wenye kiburi na ni wanafiki. Hakuna yeyote katika wao atakayeingia Peponi isipokuwa watakuwa ni mfano wa kiasi cha jogoo walio na madoa meupe kwenye mbawa na kucha zao.”

Zitazame hizi sifa alizo nazo mke mwema.

“…wenye mahaba… “ Hii ni sifa ambayo ni tukufu na yenye kusifiwa kwa yule mwanamke mwema na yule mke aliyebarikiwa. Bi maana kwamba anapenda na kufanya aweze kupendwa. Hakuna mwingine anayestahiki mapenzi haya kama mume. Anatakiwa kuhakikisha anajipendekeza kwake na kuamsha hisia na huruma yake kwa maneno mazuri ya kupendeza. Anatakiwa kuhakikisha ampende kwa kutaamiliana naye vizuri na kuonekana vizuri. Mke anatakiwa kuhakikisha ameshinda kuweza kuyapata mapenzi ya mume kwa maneno yake, muonekano, matendo na tabia.

“…wenye rutuba… “ Bi maana azae watoto wengi. Ni sifa yenye kusifika kwa mwanamke. Mwanamke huyu ni katika wanawake bora. Ikiwa mwanamke yuko na ila yoyote au maradhi ni jambo ambalo halitomdhuru kwa kuwa sio jambo ambalo amezembea yeye au amefanya kwa khiyari yake. Allaah hatomhesabu kwa hilo. Hili halimdhuru na wala haliathiri chochote katika wema wake.

Ama ikiwa mwanamke ni mwenye rutuba lakini hata hivyo akawa ni mwenye kuzuia ujauzito na watoto, anadhurika kwa hili. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Oeni wanawake wenye mahaba na rutuba. Kwani hakika mimi nitajifakhari wingi wenu kwa Ummah zingine siku ya Qiyaamah.”[2]

Linalotakikana kwa mwanamke ni kujitahidi kupata watoto na kutilia uzito katika kuwalea watoto na kuwaangalia. Vilevile ahesabu thawabu kutoka kwa Allaah kwa kupatikana katika jamii watoto wema na walinganiaji wanaotengeneza. Ahesabu hilo tokea ile siku ya kwanza anapoolewa. Azungumze baina yake yeye na Allaah amkirimu wavulana watakaokuja kuwa maimamu wa uongofu, wanachuoni wa waislamu na walinganiaji katika kheri. Kwa hili aandikiwe thawabu kubwa kwa nia yake nzuri na kila kinachofanya hilo.

“… walio na maafikiano… “ Bi maana asiwe ni mkali na msusuwavu. Anatakiwa kuwa msikivu na mtiifu. Hatakiwi kuwa ni mwenye kiburi na majivuno. Hatakiwi kumdharau mume. Hatakiwi kuwa muasi na mpekutevu.

“…wanausia… “ Bi maana mwenye kumuusia na kumliwaza mume wake na kusimama karibu naye. Anatakiwa awe ni mwenye kumsaidia katika kheri na katika kumtii Allaah na kila kinachofanya kuleta furaha na mafanikio.

“… juu ya kumcha Allaah… “ Bi maana sifa hizi zinakuwa ni zenye kunufaisha kwanza pindi mwanamke atakapomcha Allaah (´Azza wa Jall). Lau atakuwa ni mwenye mahaba, rutuba, maafikiano na mwenye kuusia kwa kutafuta mambo ya kidunia na sio kwa ajili ya kumcha Allaah, sifa hizi hazitoleta manufaa yoyote wala hazitomfaa. Sifa hizi zitamnufaisha tu ikiwa anazifanya kwa kutafuta kupata Radhi za Allaah (´Azza wa Jall) na akaishi juu ya uchaji Allaah.

“Waovu wa wanawake wenu ni wale wenye kuonyesha mapambo yao… “ Bi maana wale wenye kuonyesha mapambo yao na kutoka nje kwa kujipodoa, kujipamba, mzuri, kwa kujiweka manukato na kujipodoa ili Shetani aweze kumfuata nyuma yake na kuharibu jamii. Mwanamke mwenye kutoka kwa sifa hizi anafanya hivyo ili apate kuwa mmoja katika askari wa Iblisi na kumsaidia kuiharibu jamii. Malengo ni kueneza fitina na kueneza machafu kwa wale waumini.

“… wenye kiburi… “ Bi maana walio na kiburi. Kuna mafungamano baina ya kuonyesha mapambo na kiburi. Mwanamke anayetoka nje barabarani na kwenye masoko na ni mwenye kuonyesha mapambo, kajipodoa, kajitia manukato na kujipendezesha hawezi kwenda hivyo wakati huohuo akawa ni mwenye haya na mnyenyekevu kwa Allaah (Ta´ala). Anatoka hali ya kuwa ni mwenye kiburi, kujiweka juu na mwenye jeuri. Anakuwa ni mwenye kuzowea, katika muonekano wake na sura yake. Hivyo kuna mafungamano baina ya kuonyesha mapambo na kuwa na kiburi kama jinsi kuna mafungamano baina ya kuwa na heshima na haya.

Mwanamke mwenye heshima anakuwa na haya kamilifu. Moyo wake unakuwa ni wenye kujaa haya. Mwanamke mwenye kuonyesha mapambo yake anakuwa amevua Jilbaab ya haya na badala yake anavaa Jilbaab ya kiburi, kujiona na kiburi. Linamdhuru yeye, maisha yake ya ndoa na maisha yake yote. Ndio maana mwenye kuwa namna hiyo akasifiwa kuwa ni muovu katika wanawake. Kasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

Waovu wa wanawake wenu ni wale wenye kuonyesha mapambo yao na wenye kiburi na ni wanafiki. Hakuna yeyote katika wao atakayeingia Peponi isipokuwa watakuwa ni mfano wa kiasi cha jogoo walio na madoa meupe kwenye mbawa na kucha zao.”

Lini unawaona jogoo walio na madoa meupe kwenye mbawa zake na kucha zake? Ni zaidi ya mara chache sana kupata jogoo wa namna hiyo. Mara nyingi utamuona jogoo wote huwa mweusi. Anasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakuna yeyote katika wao atakayeingia Peponi isipokuwa watakuwa ni mfano wa kiasi cha jogoo walio na madoa meupe kwenye mbawa na kucha zao.”

bi maana ni idadi ndogo sana ya wanawake kama hawa watakaoingia Peponi. Kwa kuwa aina hii ya jogoo ni chache sana.

Hadiyth hii inafanana na maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Enyi wanawake! Toeni Swadaqah kwa wingi na mumuombe Allaah msamaha. Nimeona Moto nyinyi ndio wakazi wengi wa Motoni.”[3]

Kwa nini ameona wakazi wengi wa Motoni ni wanawake? Utakaposoma katika Sunnah kuhusu sifa hizi za wakazi wabaya wa Motoni utaona kuwa wanawake wengi wanapuuza na hawajali kabisa. Kana kwamba hatosimama mbele ya Allaah siku ya Qiyaamah na kumhesabu kwa hilo. Anaweza kufikiwa na Hadiyth na ujuzi juu ya suala hili, lakini anachojali tu yeye ni matamanio yake na utashi wake.

Kuna Hadiyth nyingi zimekuja kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambazo zimetaja sifa za mwanamke anayelaumika. Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) anasema:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amemlaani mwanamke anayerefusha nywele na mwenye kurefushwa, mwanamke anayepiga chale (tattoo) na mwenye kupigwa chale.”[4]

Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewalaani wanaume wanaojifananisha na wanawake na wanawake wanaojifananisha na wanaume.”[5]

Mbali na Hadiyth hizi na zingine zinazomlaani mwanamke kwa sifa mbalimbali  utaona ni wanawake wangapi wanaosikia laana na kuwekwa mbali na huruma ya Allaah hata hivyo hawajali kabisa. Kana kwamba hawatosimama mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) na kuulizwa juu ya hayo. Kana kwamba haitokuja siku ambapo atawekwa ndani ya shimo na kufunikwa na udongo na kusimama mbele ya Mola Wake kwa matendo yake. Anapuuza yote haya. Hafikirii lolote. Hamu yake kubwa anachojali ni kujipodoa na kujipamba hata kama kile anachokifanya ni kumuasi Allaah, kwenda kinyume na maamrisho ya Allaah na kujiweka mwenyewe katika ghadhabu na hasira za Allaah (Tabaarak wa Ta´ala).

Kuna sifa zenye kulaumika ubainifu wake umekuja katika Sunnah kwa wanawake ili mwanamke mwema aweze kuwa katika hadhari. Lengo la mwanamke kuzijua sifa hizi ni ili aweze kujiepusha nazo. Mshairi amesema:

Nimejifunza shari sio kwa ajili [ya kuitaka hiyo] shari, kwa ajili nijitenge nayo

Yule asiyetofautisha kati ya jema na shari hutumbukia ndani yake

[1]  7/82. Imaam al-Albaaniy amesema kuwa ni Swahiyh katika ”as-Swahiyhah” (3380).

[2] Ahmad (12613), kupitia Anas (Radhiya Allaahu ´anh). Imaam al-Albaaniy amesema kuwa ni Swahiyh katika “Irwaa´-ul-Ghaliyl” (1784).

[3] al-Bukhaariy (304) kupitia kwa Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh) na Muslim (79) kupitia kwa Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa).

[4] al-Bukhaariy (5947) na Muslim (2124).

[5] al-Bukhaariy (5885).

  • Mhusika: Shaykh ´Abdur-Razzaaq bin ´Abdil-Muhsin al-´Abbaad
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifaat-uz-Zawjah as-Swaalihah, uk. 27-34
  • Imechapishwa: 13/08/2017