2- Mwenye kumwingilia mke wake mchana wa Ramadhaan ilihali amefunga inaharibika swawm yake. Hapa ni pale ambapo atakuwa ni mwenye kukusudia na mwenye kujua. Ni lazima kwake kuilipa siku hiyo na kufanya tawbah ya kweli ilioambatana na majuto na kujivua [na dhambi hiyo]. Ni wajibu pamoja na hivo kutoa kafara ambayo ni kuacha mtumwa huru, asipopata asifunge miezi miwili mfululizo, asipoweza alishe masikini sitini. Hayo ni kutokana na yale yaliyothibiti kwa al-Bukhaariy na Muslim kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesimulia:

“Wakati tulipokuwa tumekaa kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuja mtu akisema: “Ee Mtume wa Allaah! Nimeangamia!” Akasema: “Una nini?”

Katika upokezi wa Muslim imekuja:

“Ni kipi kilichokuangamiza?” Akajibu: “Nimemwingilia mke wangu ilihali nimefunga.”

Katika upokezi wa Muslim imekuja:

“Nimemsibu mke wangu katika Ramadhaan.

Mtume wa Allaah akasema: “Unaweza kupata mtumwa ukamwacha huru?” Akajibu: “Hapana.” Akasema: “Unaweza kufunga miezi miwili mfululizo?” Akajibu: “Hapana.” Akasema: “Unaweza kupata chakula cha kuwalisha masikini sitini?” Akajibu: “Hapana.” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akanyamaza. Tulipokuwa katika hali hiyo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaja na chombo kilicho na tende ambapo akauliza: “Yuko wapi muulizaji?” Akajibu: “Ni mimi hapa.” Akamwambia: “Chukua ukatoe swadaqah.” Akasema: “Hivi kuna ambaye ni fakiri kuliko mimi, ee Mtume wa Allaah? Ninaapa kwa Allaah hakuna kati ya milima miwili hii watu wa nyumba ambao ni mafukara kuliko watu wa nyumbani kwangu.” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akacheka mpaka yakaonekana magego yake. Kisha akasema: “Walishe watu wa nyumbani kwako.”[1]

Katika Hadiyth hii kuna dalili inayofahamisha kwamba mfungaji, ambaye ´ibaadah ni yenye kumuwajibikia, mkazi, mwenye afya njema, aliyekusudia kufanya jimaa hali ya kuwa anakumbuka ni dhambi kubwa miongoni mwa madhambi makubwa. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliyakubali maneno ya mwanaume yule aliposema:

“Nimeangamia.”

Katika Hadiyth ya ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) katika “as-Swahiyh” ya Muslim imekuja:

“Nimeangua.”[2]

Ama akifanya jimaa hali ya kusahau, basi swawm yake ni sahihi kwa mujibu wa maoni ya wanachuoni yaliyo na nguvu zaidi. Vilevile hailazimu kulipa wala kutoa kafara.

[1] al-Bukhaariy (1936) na Muslim (1111).

[2] Muslim (1112).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mukhtaswaru fiy Ahkaam-is-Swiyaam, uk. 12-13
  • Imechapishwa: 17/04/2019