06. Fadhilah za mke mwema


4 – Fadhilah za mke mwema. ´Abdullaah bin ´Amr (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika dunia yote ni starehe na hakuna starehe ya dunia ilio bora kama mwanamke mwema.”[1]

 Sa´d bin Abiy Waqqaas (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mambo manne ni katika furaha; mwanamke mwema, makazi mapana, jirani mwema na kipando chenye umakini. Mambo manne ni katika kukosa furaha; jirani mbaya, mwanamke mbaya, kipando kibaya na makazi ya kubana.”[2]

Thawbaan (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Wakati iliposhuka kuhusu fedha na dhahabu kile kilichoshuka[3] wakasema: ““Tuweke mali gani sasa?” ´Umar akasema: “Mimi nitakujuzeni jambo hilo.” Akaenda na ngamia wake haraka ambapo akamuwahi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na mimi nikiwa nyuma namfuata. Akasema: “Ee Mtume wa Allaah! Tuweke mali gani?” Akasema:

”Achukulie mmoja wenu moyo wenye kushukuru, ulimi wenye kumtaja na mke muumini anayemsaidia mmoja wenu katika jambo lake la Aakhirah.”[4]

 Mke mwema ni yule Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliusia kujinyakulia pale mwanzoni kabisa mwa kuoa. Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwanamke anaolewa kwa moja ya mambo manne; kwa mali yake, hasabu yake, uzuri wake na dini yake – jinyakulie mwenye dini mikono yako itashika mchanga.“[5]

Haafidhw amesema:

“Maana yake ni kwamba kinacholingana na mwanamme aliye na dini na muruwa ni kwamba dini ndio iwe kitu anachokitazama katika kila jambo na khaswa yule ambaye kutangamana naye kutachukua muda mrefu. Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwamrisha kumchagua mwanamke mwenye dini kwa sababu ndio malengo makubwa”[6]

[1] Muslim (1467), an-Nasaa´iy (06/69) na tamko ni lake na wengineo.

[2] Ibn Hibbaan katika ”as-Swahiyh” yake (1232) – Mawaarid) na wengineo. al-Albaaniy amesahihisha cheni ya wapokezi wake na ni kwa mujibu wa sharti za al-Bukhaariy na Muslim (01/509).

[3] Maneno Yake (Ta´ala):

وَالَّذِينَ يَكْنِزُونَ الذَّهَبَ وَالْفِضَّةَ وَلَا يُنفِقُونَهَا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ فَبَشِّرْهُم بِعَذَابٍ أَلِيمٍَ

“Na wale wanaolimbikiza dhahabu na fedha na wala hawazitoi katika njia ya Allaah, basi wape bishara ya adhabu iumizayo.” (09:34)

[4] at-Tirmidhiy (3094), Ibn Maajah (1856), Ahmad (05/282) na wengineo. Imekuja katika tamko la at-Tirmidhiy:

“Tuweke mali gani sasa?” Akasema: ”Bora yake ni ulimi wenye kushukuru, moyo wenye kushukuru, mke muumini ambaye anamsaidia katika imani yake.”

[5] al-Bukhaariy (09/132 – Fath), Muslim (1466) na wengineo.

[6] Fath (09/135).

  • Mhusika: Shaykh Muhammad Shuwmaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifaat-uz-Zawjah as-Swaalihah, uk. 18-22
  • Imechapishwa: 22/09/2022