05. Sharti sita za ulazima kufunga Ramadhaan


Suala la tano: Sharti za ulazima wa kufunga Ramadhaan

Ni lazima kufunga Ramadhaan kwa yule ambaye ametimiza sharti zifuatazo:

1- Uislamu. Swawm haimlazimu kafiri na wala haisihi. Kwa sababu swawm ni ´ibaadah. ´Ibaadah haisihi kutoka kwa kafiri. Akisilimu halazimiki kulipa zile siku zilizompita.

2- Kubaleghe. Swawm haimlazimu yule ambaye hajafikia kiwango cha kukalifishwa. Hilo ni kutokana na maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa salalm):

“Kalamu imenyanyuliwa kutoka kwa watu watatu.”[1]

Miongoni mwao akataja mtoto mpaka abaleghe. Swawm ya ambaye bado hajabaleghe inasihi endapo atafunga na akiwa ni mwenye kupambanua mambo.

Mlezi wake anatakikana kumwamrisha kufunga ili azoee.

3- Akili. Mwendawazimu na ambaye ametokwa na akili si lazima kwao kufunga. Hilo ni kutokana na maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa salalm):

“Kalamu imenyanyuliwa kutoka kwa watu watatu.”[2]

Miongoni mwao akataja mwendawazimu mpaka apate fahamu.

4- Afya njema. Yule ambaye ni mgonjwa hawezi kufunga haimlazimikii. Iwapo atafunga basi funga yake inasihi. Amesema (Ta´ala):

 وَمَن كَانَ مَرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ

“Atakayekuwa mgonjwa au safarini basi atimize idadi katika siku nyinginezo.”[3]

Maradhi yakimwondoka basi atalazimika kulipa zile siku alizokula.

5- Ukazi. Si lazima kwa msafiri kufunga. Amesema (Ta´ala):

 وَمَن كَانَ مَرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ

“Atakayekuwa mgonjwa au safarini basi atimize idadi katika siku nyinginezo.”

Endapo msafiri atafunga basi swawm yake ni sahihi. Lakini ni lazima kwake kulipa zile siku alizofungua akiwa safarini.

6- Kutakasika na hedhi na damu ya uzazi. Ni lazima kwa wawili hao kufunga. Bali ni haramu juu yao. Hilo ni kutokana na maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa salalm):

“Je, anapoingia hedhini si haswali wala hafungi? Basi huo ndio upungufu wa dini yao.”[4]

Baadaye ni lazima kwao kulipa. ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ameeleza:

“Lilikuwa likitupata jambo hilo na tunaamrishwa kulipa funga na hatuamrishwi kulipa swalah.”[5]

[1] Ahmad (06/100) na Abu Daawuud (04/558). Ni Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”al-Irwaa´” (297).

[2] Ahmad (06/100) na Abu Daawuud (04/558). Ni Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”al-Irwaa´” (297).

[3] 02:185

[4] al-Bukhaariy (304).

[5] Muslim (335).

  • Mhusika: Nukhbatin minal-´Ulamaa´
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fiqh-ul-Muyassar, uk. 151-152
  • Imechapishwa: 14/04/2020