Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

1- Allaah (Ta´ala) amesema:

مَا أَصَابَ مِن مُّصِيبَةٍ إِلَّا بِإِذْنِ اللَّـهِ ۗ وَمَن يُؤْمِن بِاللَّـهِ يَهْدِ قَلْبَهُ ۚ وَاللَّـهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ

“Hausibu msiba wowote [kukupateni] isipokuwa kwa idhini ya Allaah. Yeyote   anayemuamini Allaah, basi huuongoza moyo wake. – Allaah kwa kila kitu ni mjuzi.”

Aayah inamaanisha kwamba misiba yote inayowafika watu imekadiriwa na Allaah. Hakuna msiba wowote ulimwenguni unaowafika watu isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ameukadiria. Amesema:

إِلَّا بِإِذْنِ اللَّـهِ

“… isipokuwa kwa idhini ya Allaah.”

Bi maana ameupanga na kuukadiria. Kwa sababu idhini ya Allaah imegawanyika aina mbili:

1- Idhini ya kilimwengu. Mfano wake ni pale Allaah (Ta´ala) aliposema:

وَمَا هُم بِضَارِّينَ بِهِ مِنْ أَحَدٍ إِلَّا بِإِذْنِ اللَّـهِ

“Wao hawawezi kumdhuru yeyote kwayo isipokuwa kwa idhini ya Allaah.”[1]

Bi maana kwa makadirio na matakwa Yake.

2- Idhini ya Kishari´ah. Mfano wake ni pale Allaah (Ta´ala) aliposema:

فَهَدَى اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا لِمَا اخْتَلَفُوا فِيهِ مِنَ الْحَقِّ بِإِذْنِهِ

“Allaah akawaongoza wale walioamini kuendea haki katika yale waliyotofautiana kwa idhini Yake.”[2]

Bi maana kwa Shari´ah Yake.

´Alqamah amesema:

“Huyo ni yule mtu ambaye anapofikwa na msiba anajua kuwa umetoka kwa Allaah, basi akaridhika na akajisalimisha.”

´Alqamah an-Nakha´iy ni mmoja katika Taabi´uun wakubwa. Ni mmoja katika Nakhaa´iyyah watatu wakubwa; ´Alqamah, al-Aswad na Ibraahiym. Walikuwa ni wanafunzi wa Ibn Mas´uud.

Maneno yake kwamba ni yule mtu ambaye anafikwa na msiba ima juu ya nafsi yake, mali yake, mtoto wake, familia yake au ndugu yake. Hata hivyo havunjiki moyo. Anatambua kwamba Allaah ndiye kaukadiria na kuupanga. Yale yaliyokadiriwa na Allaah ni lazima yatokee. Hasemi kwamba lau angelifanya hivi na vile, basi msiba usingelimtokea. Muumini anayajua haya na hivyo jambo linakuwa lepesi kwake. Anajua kuwa msiba unatoka kwa Allaah na hivyo anaridhia makadirio Yake. Kwa hiyo havunjiki moyo na wala hakasiriki. Anajisalimisha na makadirio na mipango ya Allaah (´Azza wa Jall).

Kujisalimisha na kuridhia huku Allaah amekuita kuwa ni imani. Amesema:

وَمَن يُؤْمِن بِاللَّـهِ يَهْدِ قَلْبَهُ

“Yeyote   anayemuamini Allaah, basi huuongoza moyo wake.”

Bi maana mtu anaridhia na kujisalimisha na makadirio ya Allaah. Hiki ndicho kinachokusudiwa; kusubiri juu ya msiba na kuridhia makadirio Allaah ameita kwamba ni imani. Matunda ya mtu kuridhia mipango ya Allaah, kuwa na subira na kutarajia malipo kutoka kwa Allaah ni kwamba moyo unahidiwa. Allaah kuweka ndani ya moyo imani, uoni wa mbali na nuru ni matunda ya kuwa na subira juu ya makadirio na mipango ya Allaah.

Kuhusu mtu ambaye anavunjika moyo, basi mambo hayo yanasababisha kinyume chake. Moyo wake unapofoka. Kunakuwa vurugu moyoni mwake. Daima anahisi vurugu na wasiwasi na dhiki. Ama kuhusu muumini ni mwenye kuhisi utulivu juu ya hayo yote. Aayah imefahamisha juu ya mambo makubwa ikiwa ni pamoja na:

1-  Misiba yote inatokea kwa mipango na makadirio ya Allaah.

2- Kuridhia na kuivumilia ni katika imani, kwa sababu Allaah ameita kuwa ni imani.

3- Sifa mbili hizo zinapelekea moyo kuongozwa katika kheri na imani yenye nguvu na yakini.

[1] 02:102

[2] 02:213

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: I´aanat-ul-Mustafiyd bi Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 431
  • Imechapishwa: 14/08/2019