05. Du´aa wakati wa kulala


24- Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipokuwa anataka kulala alikuwa akisema:

بِاسْمِكَ اللَّهُمَّ أَمُوتُ وَأَحْيَى

“Kwa jina Lako, Ee Allaah ninakufa na ninakuwa hai.”

Wakati anapoamka kutoka usingizini anasema:

الحَمْدُ للهِ الَّذِي أَحْيَانَا بَعْدَ مَا أَمَاتَنَا وَإِلَيْهِ النُّشُورُ

“Himdi zote ni Zake Allaah ambaye Ametupa uhai baada ya kutufisha na Kwako tutafufuliwa.”

25- Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipokuwa akilala kila usiku alikuwa akikusanya vitanga vyake, akivitemea cheche za mate na akisoma ndani yake: “Qul huwaAllaahu ahad”, Qul a´udhubi Rabbil-Falaq” na “Qul a´udhubi Rabbin-Naas”.” Kisha anajipangusa navyo mwili wake kadri na anavyoweza. Akianza kwa kichwa chake, uso wake na sehemu ya mbele ya mwili wake. Alikuwa akifanya hivyo mara tatu.”

26- Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anhu) ameeleza kwamba kuna mtu alimjia kila usiku na anataka Swadaqah ambayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa amemuachia aichunge. Usiku wa tatu akasema: “Nitakupeleka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).” Akasema: “Niache. Nitakufunza maneno ambayo Allaah Atakunufaisha nayo. Unapolala soma Aayah ya Kursiy yote:

اللّهُ لاَ إِلَهَ إِلاَّ هُوَ الْحَيُّ الْقَيُّومُ

“Hakuna mola anayeabudiwa kwa haki isipokuwa Yeye. Aliyehai daima, Msimamizi wa kila kitu… “

Allaah Ataendelea kukuhifadhi na hakukaribii Shaytwaan mpaka asubuhi.” Akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Amekwambia kweli na yeye ni muongo.”

27- Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kusoma usiku Aayah mbili za mwisho wa Suurat al-Baqarah zitamlinda.”

28- Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Pindi mmoja wenu anapoamka kutoka kitandani mwake kisha akarejea kisha akarudi basi akikukute kitanda kwa shuka yake mara tatu. Kwani hajui kilicho kuja baada yake. Na Akilala aseme:

بِاسْمِكَ رَبِّـي وَضَعْـتُ جَنْـبي ، وَبِكَ أَرْفَعُـه، فَإِن أَمْسَـكْتَ نَفْسـي فارْحَـمْها ، وَإِنْ أَرْسَلْتَـها فاحْفَظْـها بِمـا تَحْفَـظُ بِه عِبـادَكَ الصّـالِحـين

“Kwa jina Lako, Mola Wangu, nimeweka ubavu wangu na kwa ajili Yako nitaunyanyua. Ukiichukua nafsi yangu basi irehemu na ukiirudisha basi ihifadhi kwa kile unachowahifadhi nacho waja wako wema.”

Katika upokezi mwingine:

Anapoamka mmoja wenu basi na aseme:

الْحَمْدُ للهِ الَّذِي عَافَانِي في جَسَدِي وَرَدَّ عَلَيَّ رُوحِي وَأَذِنَ لِي بِذِكْرِهِ

“Himdi zote ni Zake Allaah ambaye Ameniafu katika mwili wangu, Amenirudishia roho yangu na kunifanya mimi kumdhukuru.”

29- Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumwambia ´Aliy na Faatwimah:

“Je, nisiwaeleze kilicho kheri kwenu kuliko mtumishi? Mnapolala kitandani mwenu semeni: “Subhaan Allaah” mara thelathini na tatu, “al-Hamdu lillaah” mara thelathini na tatu na “Allaahu Akbar” mara thelathini na nne.”

´Aliy amesema:

“Sikuacha kuisoma tangu nilipoisikia kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).” Aliambiwa: “Hata wakati wa usiku wa Swiffiyn?” Akasema: “Hata wakati wa usiku wa Swiffiyn.”

30- Wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipokuwa anataka kulala alikuwa akiweka mkono wake wa kulia chini ya shavu lake na anasema:

اللهُمَّ قِني عَذَابَكَ يَوْمَ تَبْعَثُ عِبَادَكَ

“Ee Allaah! Nikinge kutokana na adhabu Yako siku ambayo Utawafufua waja Wako.”

31- Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akisema pindi anapolala kitandani mwake:

الْحَمْدُ للهِ الَّذِي أَطْعَمَنَا وَسَقَانَا وَكَفَانَا، وَآوَانَا، فَكَمْ مِمَّنْ لا كَافِيَ لَهُ وَلا مُؤْوِيَ

“Himdi zote ni Zake Allaah ambaye ametulisha, ametunywesha, akatutosheleza na akatuhifadhi. Ni wangapi ambao hawana wa kuwatosheleza wala wa kuwahifadhi?”

32- Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimuamrisha mtu anapolala aseme:

اللَّهُمَّ أَنْتَ خَلَقْتَ نَفْسِي وأَنْتَ تَتَوَفَّاهَا لكَ مَمَاتُهَا وَمَحْيَاهَا إِنْ أَحْيَيْتَهَا فَاحْفَظْهَا وَإِنْ أَمَتَّهَا فَاغْفِرْ لَهَا اللَّهُمَّ إِنِّي أَسْأَلُكَ الْعَافِيَةَ

“Ee Allaah! Hakika Wewe umeiumba nafsi yangu nawe utaiua. Uhai wake na kufa kwake uko Kwako. Ukiipa uhai basi ihifadhi, na Ukiifisha (ukiiua) basi isamehe. Ee Allaah! Hakika mimi nakuomba afya njema.”

33- Alikuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema wakati anapolala kitandani mwake:

اللَّهُمَّ رَبَّ السَّمَواتِ وَرَبَّ الأَرْضِ وَرَبَّ الْعَرْشِ الْعَظِيمِ رَبَّنَا وَرَبَّ كُلِّ شَيءٍ فَالِقَ الْحَبِّ وَالنَّوَى وَمُنْزِلَ التَّوْرَاةِ والإِنْجِيلِ والْفُرْقَانِ أَعُوذُ بِكَ مِنْ شَرِّ كُلِّ ذِي شَرٍّ أَنْتَ آخِذٌ بِنَاصِيَتِهِ أَنْتَ الأَوَّلُ فَلَيْسَ قَبْلَكَ شَيءٌ وَأَنْتَ الآخِرُ فَلَيْسَ بَعْدَكَ شَيءٌ وأَنْتَ الْبَاطِن فليس دُونَكَ شَيءٌ اقْضِ عَنَّا الدَّيْنَ واغْنِنَا مِنَ الْفَقْرِ

“Ee Allaah! Mola wa mbingu saba na Mola wa ´Arshi tukufu! Mola Wetu na Mola wa kila kitu Mwenye kuichanua tembe ya mbegu na kokwa na Alieteremsha Tawrat, Injiyl na Furqaan. Najikinga Kwako kutokana na shari ya kila kitu ambacho Wewe ndiye mwenye kukamata utosi wake. Ee Allaah! Wewe ndiye wa Mwanzo; hakuna kabla yako kitu. Wewe ndiye wa Mwisho; hakuna baada yako kitu. Na Wewe ndiye adh-Dhwaahir; hakuna juu Yako kitu chochote. Na Wewe ndiye al-Baatwin; hakuna kilicho karibu zaidi kuliko Wewe. Tulipie madeni yetu na utuepushe na ufakiri.”

34- Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Unapokuja mahala pako pa kulala tawadha kama unavyotawadha kwa ajili ya Swalah. Kisha lalia upande wako wa kulia na useme:

اللهم أسلمت نفسي إليك و وجهت وجهي إليك و فوّضتُ أمري إليك و ألجأتُ ظهري إليك رغبةً و رهبةً إليك لا ملجأ و لا منجا منك إلا إليك. آمنت بكتابك الذي أنزلت و بنبيك الذي أرسلت

“Ee Allaah! Nimeisalimisha nafsi yangu Kwako. Nimeuelekeza uso wangu Kwako. Nimekuachia mambo yangu Wewe. Nimeutegemeza mgongo wangu Kwako. Nafanya hivyo kwa matarajio na kwa kukuogopa. Hapana sehemu ya kukimbilia wala ya kujiokoa ila Kwako. Nimekiamini kitabu Chako ulichokiteremsha na Mtume Wako Uliyemtuma.”

Ukifa usiku huo basi umekufa juu ya maumbile ya asli. Fanya ndio ya mwisho unayosema.”

  • Mhusika: Shaykh-ul-Islaam Ahmad bin Taymiyyah
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swahiyh-ul-Kalim at-Twayyib, uk. 34-39
  • Imechapishwa: 21/03/2017