04. Uombezi wa Mtume siku ya Qiyaamah

Vilevile kuna Hadiyth zilizopokelewa kwa mapokezi mengi kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) zinazothibitisha maombezi mengi kwa watenda madhambi na wengineo. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ana maombezi mengi kukiwemo uombezi kwa watu pindi watapokuwa wamesimama mahali pa kukusanyikia. Watamwendea Aadam (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kumuomba uombezi ambapo ataomba udhuru na kustahi kwa Mola wake kwa kuwa alikosea kwa kula kwenye mti. Baada ya hapo atasema:

“Mola wangu hajapatapo kukasirika kama alivyokasirika leo na hatokasirika tena namna hiyo kamwe.”

Kisha atawaelekeza watu wamwendee Nuuh kwa kuwa yeye ndiye alikuwa Mtume wa kwanza kutumwa ardhini. Nuuh (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) atastahi kuombea mbele ya Mola wake kwa kuwa ataona kuwa alikosea pindi alipoomba du´aa dhidi ya watu wake na Allaah akawa amewaangamiza. Amejipa udhuru tu. Anaona haya kwa Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) kwa sababu ya dhambi moja ambayo ni bora kuliko matendo yetu. Hebu tumuonelee Allaah haya ukweli ipasavyo katika mambo yote ya maisha yetu.

Nuuh (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) atasema:

“Mola wangu hajapatapo kukasirika kama alivyokasirika leo na hatokasirika tena namna hiyo kamwe. Nenden kwa mwengine. Nendeni kwa Ibraahiym.”

Ibraahiym (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ataomba udhuru kwa sababu ya kitu anachoonelea kuwa ni uongo. Haikuwa uongo wa kihakika, ilikuwa ni tawriya. Atazingatia kuwa ni maasi ambapo atastahi kuombea mbele ya Allaah. Atasema:

“Mola wangu hajapatapo kukasirika kama alivyokasirika leo na hatokasirika tena namna hiyo kamwe. Nenden kwa mwengine. Mimi mwenyewe naiangalia nafsi yangu.”

Baada ya hapo atawaelekeza watu kwa Muusa. Muusa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimuua kafiri na mtu dhalimu na akaonelea kitendo chake kama dhambi duniani na Aakhirah. Pamoja na kuwa Allaah amewasamehe duniani, akawanyanyua daraja na akawateua kuwa Manabii na Mtume wanamuonelea Allaah haya kwa sababu ya makosa yao. Muusa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) atasema:

“Mola wangu hajapatapo kukasirika kama alivyokasirika leo na hatokasirika tena namna hiyo kamwe. Nendeni kwa mwengine. Mimi mwenyewe naiangalia nafsi yangu. Nendeni kwa mwengine. Nendeni kwa ´Iysaa.”

Watu wataenda kwa ´Iysaa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye atasema:

“Mola wangu hajapatapo kukasirika kama alivyokasirika leo na hatokasirika tena namna hiyo kamwe. Nendeni kwa mwengine. Mimi mwenyewe naiangalia nafsi yangu.”

Baada ya hapo akawaelekeza kwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye atasema:

“Mimi ndio mwenye haki nayo, mimi ndio mwenye haki nayo.

Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ataanguka na kusujudu mbele ya Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) na awaombee watu watolewe katika hali hiyo yenye kushtua ambapo jua litakuwa karibu na watu kiasi cha kwamba kuna ambao majasho yatafika kwenye miguu yao, magoti, kiunoni, kifuani na wengine vinywani[1]. Watu watakuwa katika hali ya kutisha ambayo hakuna aijuae isipokuwa tu Allaah (Tabaarak wa Ta´ala). Wote wote watakuwa namna hii, sawa waumini na makafiri, isipokuwa tu watu aina saba ambao Allaah atawafunika kwa kivuli chake siku ambayo hakuna kivuli isipokuwa Chake. Pindi watu wote watapokutana na matatizo na majanga haya watu aina saba watafunikwa na kivuli cha Allaah kwa sababu ya matendo yao. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Watu aina sababu watafunikwa na kivuli cha Allaah siku ambayo kutakuwa hakuna kivuli isipokuwa kivuli Chake.” al-Bukhaariy (659) na Muslim (1031).

[1] Muslim (194).

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Qurrat-ul-´Aynayn bi Tawdhwiyh Ma´aaniy ´Aqiydat-ir-Raaziyayn, uk. 11-14
  • Imechapishwa: 09/10/2016