Huenda mtu akauliza ni kwa nini hakuanza kitabu chake kwa kumhimidi Allaah na kumtakia swalah na salamu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Jambo la kwanza ni kwamba ameanza kwa jina la Allaah. Inatosha kwa kumswalia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kuandika utangulizi. Jambo la pili ni yale yaliyosemwa na mshereheshaji ´Allaamah na Shaykh ´Abdur-Rahmaan bin Hasan (Rahimahu Allaah):

“Nina nuskha kwa hati ya mkono ya Shaykh ambapo ameanza kitabu kwa:

“Himdi zote njema anastahiki Allaah. Swalah na salamu zimwendee Mtume wetu Muhammad.”

Maana ya Tawhiyd kilugha ni “kukipwekesha kitu juu ya kingine”. Maana yake Kishari´ah ni “kumpwekesha Allaah kwa ´ibaadah”.Maana ya Kishari´ah inaweza kugawanywa mafungu matatu kwa njia ya upambanuzi:

1-  Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah. Maana yake ni kumpwekesha Allaah (Subhaanah) katika matendo Yake. Bi maana kwamba Yeye Mwenyewe ndiye Mwenye kuumba, kuruzuku, kuhuisha, kufisha, kunufaisha na kudhuru. Kukiri aina hii peke yake hakumfanyi mtu akawa muislamu. Hata makafiri waliikiri. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

وَلَئِن سَأَلْتَهُم مَّنْ خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ لَيَقُولُنَّ اللَّـهُ ۚ قُلِ الْحَمْدُ لِلَّـهِ ۚ بَلْ أَكْثَرُهُمْ لَا يَعْلَمُونَ

“Na ukiwauliza: Ni nani aliyeumba mbingu na ardhi? Bila shaka watasema: Allaah. Sema: AlhamduliLLaah (Himidi Anastahiki Allaah). Bali wengi wao hawajui.”[1]

قُلْ مَن يَرْزُقُكُم مِّنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ أَمَّن يَمْلِكُ السَّمْعَ وَالْأَبْصَارَ وَمَن يُخْرِجُ الْحَيَّ مِنَ الْمَيِّتِ وَيُخْرِجُ الْمَيِّتَ مِنَ الْحَيِّ وَمَن يُدَبِّرُ الْأَمْرَ ۚ فَسَيَقُولُونَ اللَّـهُ ۚ فَقُلْ أَفَلَا تَتَّقُونَ

”Sema: “Nani anayekuruzukuni kutoka mbinguni na ardhini au nani anayemiliki kusikia na kuona na nani anayemtoa aliye hai kutoka mfu na anayemtoa mfu kutoka aliye hai na nani anayeendesha mambo?”  Watasema: “Ni Allaah”, basi sema: “Je, basi kwa nini hamchi?”[2]

أَمَّن يَبْدَأُ الْخَلْقَ ثُمَّ يُعِيدُهُ وَمَن يَرْزُقُكُم مِّنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ ۗ أَإِلَـٰهٌ مَّعَ اللَّـهِ ۚ قُلْ هَاتُوا بُرْهَانَكُمْ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ

”Au nani Anayeanzisha uumbaji, kisha Anaurejesha; na nani anayekuruzukuni kutoka mbinguni na kwenye ardhi? Je, yuko mwabudiwa pamoja na Allaah? Sema: Leteni ushahidi wenu wa wazi mkiwa ni wakweli.”[3]

Allaah anaeleza kwamba washirikina walikuwa wakiamini kwamba Allaah ndiye Mwenye kuumba na Mwenye kuruzuku ambaye anahuisha na anafisha. Pamoja na haya hawakuwa waislamu. Kwa nini? Kwa sababu hawakuhakikisha aina ya pili ambayo ndio lengo la kila kitu.

[1] 31:25

[2] 10:31

[3] 27:64

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: I´aanat-ul-Mustafiyd bi Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 21-22
  • Imechapishwa: 18/07/2019