04. Sura ya tatu: Miongoni mwa sababu zinazopelekea kupinda katika ´Aqiydah sahihi

Kuna sababu mbalimbali zinazopelekea kupinda kutoka katika ´Aqiydah sahihi. Ni wajibu kuzitambua. Miongoni mwazo ni zifuatazo:

1- Mtu kutoijua ´Aqiydah sahihi kwa sababu ya kupuuza kujifunza na kuifunza au mtu akawa anaiwekea umuhimu mdogo mpaka kunazalika kizazi kisichoijua ´Aqiydah hiyo na kisichojua yale yenye kwenda kinyume nayo na yenye kuivunja. Matokeo yake kikaamini haki kuwa batili na batili kuwa ndio haki. ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Kamba ya Uislamu inamegolewa sehemu baada ya sehemu pale atapokulia katika Uislamu yule asiyejua kipindi cha kikafiri.”

2- Kufuata kichwa mchungu yale waliyokuwemo mababa na mababu, watu wakashikamana nayo japokuwa ni batili na wakaacha yenye kwenda kinyume nayo japokuwa ndio haki. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَإِذَا قِيلَ لَهُمُ اتَّبِعُوا مَا أَنزَلَ اللَّـهُ قَالُوا بَلْ نَتَّبِعُ مَا أَلْفَيْنَا عَلَيْهِ آبَاءَنَا ۗ أَوَلَوْ كَانَ آبَاؤُهُمْ لَا يَعْقِلُونَ شَيْئًا وَلَا يَهْتَدُونَ

“Wanapoambiwa: “Fuateni yale aliyoyateremsha Allaah husema: “Bali tunafuata yale tuliyowakuta nayo baba zetu.” Je, japokuwa baba zao walikuwa hawaelewi kitu chochote na wala hawakuongoka?”[1]

3- Kufuata kibubusa kwa kuchukua maoni ya watu katika ´Aqiydah pasi na kujua dalili zake na usahihi wake. Hivo ndivyo ulivo uhalisia kutoka katika mapote yaliyopinda kama vile Jahmiyyah, Mu´tazilah, Ashaa´irah, Suufiyyah na mengineyo. Wamewafuata kichwa mchunga maimamu wa upotevu na matokeo yake wakapinda kutoka katika ´Aqiydah sahihi.

4- Kuchupa mpaka kwa mawalii na waja wema na kuwapandisha zaidi ya nafasi zao kwa njia ya kwamba watu wakaamini kuwa na mambo ambayo hakuna mwengine ayawezayo isipokuwa Allaah kama kuleta manufaa, kuzuia madhara, kuwafanya kuwa ni wakati na kati baina ya Allaah na viumbe Wake katika kutatua haja mbalimbali na kuitikia maombi kiasi cha kwamba hali hiyo ikawapelekea kuwaabudu badala ya Allaah na kujikurubisha kwenye makaburi yao kwa kuwachinjia, kuwawekea nadhiri,  kuwaomba, kuwataka uokozi na msaada. Hivo ndivyo ilivyotokea juu ya watu wa Nuuh kwa wale watu wema pale waliposema:

وَقَالُوا لَا تَذَرُنَّ آلِهَتَكُمْ وَلَا تَذَرُنَّ وَدًّا وَلَا سُوَاعًا وَلَا يَغُوثَ وَيَعُوقَ وَنَسْرًا

“Wakasema: “Msiwaache waungu wenu na wala msimwache Wadd na wala Suwaa´ na wala Yaghuuth na Ya’uuq na Nasr!”[2]

Kadhalika hivo ndivyo ilivyo hali leo kwa waabudu makaburi wengi katika miji mingi.

5- Kughafilika kuzizingatia alama za Allaah za kilimwengu na za Qur-aan na kudanganyika na maendeleo ya kuichumi ya hivi sasa kiasi cha kwamba mpaka wakafikiria kuwa ni katika uwezo wa binaadamu peke yake. Matokeo yake wakawa wanamuadhimisha mtu na kuyaegemeza mambo haya katika ijitihadi zake na uvumbuzi wake peke yake. Qaaruun alisema hapo kabla:

إِنَّمَا أُوتِيتُهُ عَلَىٰ عِلْمٍ عِندِي

“Hakika nimepewa haya kwa sababu ya elimu yangu.”[3]

Kama anavosema mtu:

هَذَا لِي

“Haya nayastahiki mimi.”[4]

إِنَّمَا أُوتِيتُهُ عَلَىٰ عِلْمٍ

“Hakika nimepewa hayo kwa sababu ya elimu yangu.”[5]

Hawakufikiri na kuzingatia ukumbwa wa Yule aliyeumba viumbe hawa, akamuumba binaadamu, akampa uwezo wa kuweza kutengeneza vitu hivi na kunufaika navyo:

وَاللَّـهُ خَلَقَكُمْ وَمَا تَعْمَلُونَ

“Ilihali Allaah amekuumbeni pamoja na vile mnayoyafanya.”[6]

أَوَلَمْ يَنظُرُوا فِي مَلَكُوتِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَا خَلَقَ اللَّـهُ مِن شَيْءٍ

“Je, hawatazami ufalme wa mbingu na ardhi na vitu alivyoviumba Allaah?”[7]

أَوَلَمْ يَرَوْا أَنَّ اللَّـهَ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ قَادِرٌ عَلَىٰ أَن يَخْلُقَ مِثْلَهُمْ وَجَعَلَ لَهُمْ أَجَلًا لَّا رَيْبَ فِيهِ فَأَبَى الظَّالِمُونَ إِلَّا كُفُورًا

”Je, hawajaona kwamba Allaah ambaye ameumba mbingu na ardhi ni mweza wa kuumba mfano wa na amewawekea muda maalum usio na shaka, lakini madhalimu wamekataa kabisa [hawataki jengine] isipokuwa kukufuru tu.”[8]

6- Mara nyingi nyumba inakuwa haina maelekezo yaliyo salama. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kila mtoto anazaliwa katika maumbile [ya Uislamu]; baba yake ndiye humfanya akawa myahudi, mnaswara au mwabudu moto.”[9]

 Wazazi wawili wana jukumu kubwa katika kutengeneza mwelekeo wa mtoto.

7- Sehemu kubwa ya vyombo vya kuelimisha na vyombo vya khabari katika ulimwengu wa Kiislamu kuacha kutekeleza majukumu yake. Mara nyingi mfumo wa kufunza umekuwa hauweki umuhimu mkubwa au hauweki kabisa katika suala la dini. Upande mwingine vyombo vya khabari vyenye kuonekana, kusikilizwa na kusomwa mara nyingi vimekuwa ni vyenye kubomoa na kuharibu na huku vinatilia umuhimu mambo ya kiuchumi na burudani. Havitilii umuhimu mambo yenye kutengeneza tabia, kupanda ´Aqiydah sahihi, kukabiliana na mawimbi yaliyopinda mpaka kuzalike kizazi ambacho kitakuja kukabiliana na jeshi la kikafiri.

[1] 02:170

[2] 71:23

[3] 28:78

[4] 41:50

[5] 39:49

[6] 37:96

[7] 07:185

[8] 17:99

[9] al-Bukhaariy (03/312) na Muslim (08/423).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-ut-Tawhiyd, uk. 11-14
  • Imechapishwa: 22/01/2020