04. Qur-aan na Sunnah ni vitu viwili vyenye kulazimiana

Misingi hiyo miwili ni yenye kulazimiana. Anayepinga msingi mmoja basi amekanusha na kuukadhibisha msingi mwingine. Hiyo ni kufuru na ni upotevu na vilevile ni kutoka katika Uislamu kwa maafikiano ya wanachuoni wote na watu wa imani.

Kumepokelewa Hadiyth tele kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu ya uwajibu wa kumtii, kufuata yale aliyokuja nayo na uharamu wa kumuasi. Hilo linawahusu wale waliokuwa wakati wake na wataokuja baada yake mpaka siku ya Qiyaamah. al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kunitii basi amemtii Allaah na mwenye kuniasi amemuasi Allaah.”

al-Bukhaariy amepokea kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ummah wangu wote utaingia Peponi isipokuwa atayekataa.” Kukasemwa: “Ee Mtume wa Allaah! Nani atayekataa?” Akasema: “Atayenitii ataingia Peponi na atayeniasi atakuwa amekataa.”

Ahmad, Abu Daawuud na al-Haakim wamepokea kwa mlolongo wa wapokezi Swahiyh kupitia kwa Miqdaam bin Ma´diy Karb aliyesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Tanabahini! Hakika mimi nimepewa Kitabu na kingine mfano wake. Tanabahini! Anakaribia kujitokeza mwanaume aliyeshiba juu ya kitanda chake na kusema: “Shikamaneni na Qur-aan hii. Yale ya halali mtayoyakuta ndani yake, basi yahalalisheni na yale ya haramu mtayoyakuta ndani yake, basi yaharamisheni.”

Abu Daawuud na Ibn Maajah wamepokea kwa mlolongo wa wapokezi Swahiyh kupitia kwa Ibn Abiy Raafiy´ ambaye amepokea kutoka kwa baba yake aliyesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Asiwepo yeyote mwenye kushegama juu ya kitanda chake akajiwa na amri katika niliyoamrishwa au niliyokatazwa akasema: “Hatuyajui [hayo]. Tutachopata katika Kitabu cha Allaah ndio tutachokifuata.””

al-Hasan bin Jaabir amesema kuwa amemsikia Miqdaam bin Ma´diy Karb (Radhiya Allaahu ´anh) akisema: “Mtume wa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) siku ya Khaybar alikataza mambo kadhaa halafu akasema:

“Anakaribia mmoja wenu kunikadhibisha ambapo ameshegama akajiwa na maneno yangu kisha aseme: “Baina yangu mimi na nyinyi ni Kitabu cha Allaah. Kutachopata ndani yake cha halali tutakihalalisha na tutachopata ndani yake cha haramu tutakiharamisha. Tanabahini! Yale aliyoharamisha Mtume wa Allaah ndio mfano wa yale aliyoharamisha Allaah.””

Ameipokea al-Haakim, at-Tirmidhiy na Ibn Maajah kwa mlolongo wa wapokezi Swahiyh.

Kumepokelewa mapokezi chungumzima kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba alikuwa akiwausia Maswahabah wake katika Khutbah zake waliyopo wawafikishie wasiokuwepo na kusema:

“Huenda mfikishiwaji akaelewa zaidi kuliko mfikishaji.”

Katika hayo ni yale aliyopokea al-Bukhaariy na Muslim ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pindi alipowakhutubia watu katika hajj ya kuaga siku ya ´Arafah na siku ya kuchinja aliwaambia:

“Aliyepo amfikishie asiyekuwepo. Huenda mfikishiwaji akaelewa zaidi kuliko mfikishaji.”

Iwapo Sunnah yake ingelikuwa sio hoja kwa yule mwenye kuisikia na yule mfikishiwaji na endpao ingelikuwa sio yenye kubaki mpaka siku ya Qiyaamah, basi asingeliwaamrisha kuifikisha. Kwa hayo ikapata kutambulika kuwa hoja ni yenye kumsimamia yule mwenye kuisikia aliyepo wakati wake na yule mwenye kufikishiwa kwa mlolongo wa wapokezi Swahiyh.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ujuwb-ul-´Amal bis-Sunnah
  • Imechapishwa: 23/10/2016