04. Kuogopa shirki


Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

1- Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ

”Hakika Allaah hasamehi kushirikishwa na anasamehe yaliyo chini ya hayo kwa amtakae.”(04:48)

2- Ibraahiym (´alayhis-Salaam) amesema:

وَاجْنُبْنِي وَبَنِيَّ أَن نَّعْبُدَ الْأَصْنَامَ

“Uniepushe mimi na wanangu kuabudu masanamu.”(14:35)

3- Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kikubwa ninachokikhofieni juu yenu ni shirki ndogo.” Alipoulizwa juu yake akasema: “Kujionyesha.”[1]

4- Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Anayekufa ilihali ni mwenye kuomba wenza pamoja na Allaah ataingia Motoni.”[2]

Ameipokea al-Bukhaariy.

5- Muslim amepokea kuwa Jaabir (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mtu ambaye atakutana na Allaah ilihali hamshirikishi na chochote ataingia Peponi. Na atakayekutana Naye ilihali ni mwenye kumshirikisha na chochote ataingia Motoni.”[3]

MAELEZO

Mlango unahusiana na uwajibu wa kuogopa shirki. Ni wajibu kwa muumini kuiogopa shirki na maasi. Ajitenge nayo mbali na khaswa shirki. Asijiami nayo juu ya nafsi yake.

Shirki maana yake ni kumshirikisha Allaah na mwengine katika ´ibaadah pasi na kujali inahusiana na ´ibaadah ipi. Ndio maana ikaitwa kuwa ni shirki. ´Ibaadah ni haki ya Allaah Pekee. Baya zaidi kuliko hilo ni kumfanyia ´ibaadah aina zote asiyekuwa Allaah.

1-  Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ

”Hakika Allaah hasamehi kushirikishwa na anasamehe yaliyo chini ya hayo kwa amtakae.”(04:48)

Hapa kumebainishwa ukubwa na ukhatari wa shirki. Mtu akifa katika hali hiyo hasamehewi. Atadumishwa Motoni milele. Hilo ni tofauti na madhambi mengine. Ni jambo liko chini ya utashi wa Allaah akitaka atamuadhibu kisha baadae amwingize Peponi na akitaka atamsamehe. Lakini inapokuja katika shirki Allaah (Ta´ala) anasema:

إِنَّهُ مَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدْ حَرَّمَ اللَّـهُ عَلَيْهِ الْجَنَّةَ وَمَأْوَاهُ النَّارُ

“Hakika yule atakayemshirikisha Allaah, bila shaka Allaah atamharamishia Pepo na makazi yake yatakuwa ni motoni.”[4]

2- Ibraahiym (´alayhis-Salaam) amesema:

وَاجْنُبْنِي وَبَنِيَّ أَن نَّعْبُدَ الْأَصْنَامَ

“Na Uniepushe na wanangu kuabudu masanamu.” (14:35)

Hapa kuna ukhatari wa shirki. Bwana wa Mitume baada ya Mtume wetu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa ni mwenye kuiogopa shirki. Ni wajibu kuwaiga na kuiogopa shirki zaidi kuliko walivyokuwa.

Masanamu ni kitu kilicho kwa aina kama ya mtu na wanyama. Kulikuwepo aina mbalimbali za washirikina. Kuna ambao walikuwa wakiabudu masanamu. Wengine walikuwa wakiabudu yasiyokuwa masanamu kama mti, bahari, jua na mwezi. Wote kitu kimoja ndio kilikuwa chenye kuwakutanisha ambacho ni kumtekelezea ´ibaadah asiyekuwa Allaah (´Azza wa Jall). Sanamu inaweza kuitwa pia “mzimu”.

03- Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kikubwa ninachokikhofieni juu yenu ni shirki ndogo.” Alipoulizwa juu yake akasema: “Kujionyesha.”

Hadiyth hii imepokewa na Ahmad kwa mlolongo wa wapokezi mzuri kupitikia kwa Mahmuud bin Lubayd kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Imepokelewa vilevile kupitia njia zingine na milolongo ya wapokezi ilio na nguvu. Zote zinatolea dalili kuonesha kuwa ni wajibu kuwa na tahadhari na kujionyesha na kwamba ni jambo la khatari. Kuna watu wema wenye kutumbukia ndani yake. Wanaweza kutumbukia katika kujionyesha pindi wanaposwali, wanapota zakaah, wanapoamrisha mema na kukataza maovu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kutaka kusikika basi Allaah atamfichua na yule mwenye kutaka kuonekana na yeye Allaah atamfichukua.”[5]

Utimilifu wa Hadiyth ni:

“Allaah atawaambia wale wenye kujionyesha siku ya Qiyaamah: “Nendeni kwa wale mliokuwa mkijionyesha kwao duniani na mtazame kama watakupeni malipo yoyote.”[6]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah (Ta´ala) amesema: “Mimi ni Mwenye kujitosheleza ambaye sina haja ya washirika. Hivyo basi, yule mwenye kufanya kitendo na akanishirikisha Mimi pamoja na wengine nitamwacha yeye na shirki yake.”[7]

Imepokelewa na Muslim. Kwa ajili hiyo ni wajibu kwa mtu amtakasie ´ibaadah Allaah peke yake.

4- Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Anayekufa ilihali ni mwenye kuomba wenza pamoja na Allaah ataingia Motoni.”

Imepokelewa na al-Bukhaariy.

Mwenza ni mshirika anayeombwa msaada na kutakwa uokozi pamoja na Allaah. Mtu kama huyu atadumishwa Motoni milele. Katika upokezi mwingine imekuja ya kwamba Ibn Mas´uud amesema:

“Na anayekufa ilihali si mwenye kuomba wenza pamoja na Allaah ataingia Peponi.”

Bi maana yule mwenye kufa juu ya Tawhiyd ataingia Peponi. Ni dalili yenye kuonesha kuwa yule mwenye kujichukulia wenza katika watu wema, Mitume, miti na mawe akawaabudu pamoja na Allaah ataingia Motoni.

5- Muslim amepokea kuwa Jaabir (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mtu ambaye atakutana na Allaah ilihali hamshirikishi na chochote ataingia Peponi. Na atakayekutana Naye ilihali ni mwenye kumshirikisha na chochote ataingia Motoni.”

Hapa kuna ukhatari wa shirki na kwamba ni wajibu kuigopa na kutahadhari nayo.

Hadiyth ndani yake mna mambo mawili yanayopelekea:

1- Mwenye kukutana na Allaah pasi na kumshirikisha na chochote ataingia Peponi.

2- Mwenye kukutana na Allaah ilihali ni mshirikina ataingia Motoni. Kwa ajili hii ndio maana imetajwa katika upokezi mwingine ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Je, nisikujuzeni juu ya mambo mambo mawili yanayohitajika?” Wakasema: “Ndio.” Akasema: “Mtu ambaye atakutana na Allaah ilihali hamshirikishi na chochote ataingia Peponi. Na atakayekutana Naye ilihali ni mwenye kumshirikisha na chochote ataingia Motoni.”

[1] Ahmad (23680). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh-ul-Jaami´” (1555).

[2] al-Bukhaariy (4497).

[3] al-Bukhaariy (129) na Muslim (93).

[4] 05:72

[5] al-Bukhaariy (6499) na Muslim (93).

[6] Ahmad (23680). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh-ul-Jaami´” (1555).

[7] Muslim (2985).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 27-29
  • Imechapishwa: 19/03/2018