04. Dalili nyingine kwenye Injili ya kwamba ´Iysaa ni mwanadamu

“25Wakati ule Yesu akasema: “Nakushukuru, Baba, Mungu wa mbingu na ardhi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wasomi na wenye akili na ukawafunulia nayo watoto wachanga.”[1]

“23Naye pindi alipowaaga tu makutano alipanda mlimani kujiweka faraghani na kusali. Kulipokuwa jioni alikuwa huko peke yake.”[2]

Ni vipi atasali iwapo yeye ni Allaah au sehemu ya Allaah? Sala haiwi isipokuwa kutoka kwa mja fakiri ambaye anahitajia huruma wa Allaah. Allaah (Ta´ala) amesema:

يَا أَيُّهَا النَّاسُ أَنتُمُ الْفُقَرَاءُ إِلَى اللَّـهِ ۖ وَاللَّـهُ هُوَ الْغَنِيُّ الْحَمِيدُ

“Enyi watu! Nyinyi ni mafakiri kwa Allaah! Allaah ndiye mkwasi, mwenye kuhimidiwa.”[3]

إِن كُلُّ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ إِلَّا آتِي الرَّحْمَـٰنِ عَبْدًا

“Hakuna yeyote [katika viumbe] aliyeko mbinguni na ardhini isipokuwa atamjia Mwingi wa Rahmah kama mja.”[4]

“21Yesu akaondoka mahali huko akaenda pande za Tiro na Sidoni. 22Mwanamke mmoja mkanaani aliyeishi huko akakutana nae na akampazia sauti akisema: “Nirehemu, Bwana, Mwana wa Daudi! Binti yangu amepagawa sana na pepo.” 23Wala yeye hakumjibu kitu. Ndipo wanafunzi wake wakamuendea, wakamuomba hali ya kusema: “Mwambie aende zake, kwa maana anatupigia kelele nyuma yetu.” 24Akajibu: “Sikutumwa isipokuwa kwa kondoo waliopotea wa watu wa Israeli.” 25Lakini yule mwanamke akaja akamsujudia na kusema: “Bwana, nisaidie.” 26Akajibu: “Si sawa kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.” – 27″Yule mwanamke akajibu: “Ndiyo, Bwana”, lakini hata mbwa hula makombo yaangukayo mezani pa bwana zao.” 28Ndipo Yesu akamwambia yule mwanamke: “Mama, imani yako ina nguvu, itakuwa kama utakavyo.” Na tangu saa ile binti yake akapona.”[5]

Katika kisa hiki kuna makosa mengi:

1- ´Iysaa hana huruma na mapenzi – iwapo kisa kitakuwa ni sahihi.

2- Kasumba zenye chuki kwa vile anawaponya watoto wa mji wake na si wengine, pamoja na kuwa hakuhasirika kitu katika hayo.

3- ´Iysaa anaonyesha kiburi cha uzalendo, kuwadharau wengine na kuwachukulia kama mijibwa.

4- Mwanamke wa kishirikina mjinga alijadiliana naye na akamshinda.

“16Ndipo mtu mmoja akamuendea na kumuuliza: “Mwalimu, nitende jambo gani jema ili nipate maisha ya milele?” 17Yesu akasema: “Kwa nini waniuliza kuhusu habari njema? Hakuna aliye mwema isipokuwa mmoja tu. Lakini ukitaka kuingia katika uzima, shikamana na maamrisho.”[6]

Hapa kuna dalili nyingine ya kwamba ´Iysaa ni mwanadamu.

“45Pindi wakuu wa makuhani na mafarisayo waliposikia mifano yake walitambua ya kuwa anawazungumzia wao. 46Walitaka kumkamata lakini waliwaogopa watu, ambao walikuwa wakimuona kuwa Nabii.”[7]

Pindi walipotaka kumkamata waliwaogopa watu ambao walikuwa wakiitakidi kuwa ni Nabii. Ni dalili inayothibitisha kuwa watu katika zama za ´Iysaa walikuwa hawaonelei kuwa ni Allaah, mwana wa Allaah wala mmoja katika utatu. Bali walikuwa wakiamini ya kwamba ni Nabii tu. Hii ni moja ya dalili zenye nguvu dhidi yao wanaosema kuwa alikuwa mungu, lau wangelikuwa wanazingatia.

“8Bali ninyi msiitwe Rabi, kwa kuwa mwalimu wenu ni mmoja nanyi nyote ni ndugu.”[8]

Ni dalili inayothibitisha kuwa watu katika zama za ´Iysaa walikuwa hawaonelei kuwa ni Allaah, mwana wa Allaah wala mmoja katika utatu. Bali walikuwa wakiamini ya kwamba ni Nabii tu. Hii ni moja ya dalili zenye nguvu dhidi yao wanaosema kuwa alikuwa mungu, lau wangelikuwa wanazingatia. Ni dalili inayothibitisha kuwa Masihi ni mwanadamu na kwamba Mola ni mmoja Naye si mwengine ni Allaah. Aya hii imepotoshwa kwa kusudi pindi ilipofasiriwa kwa kiarabu. Wamefanya ionekane kuwa Masihi ndiye Bwana, lakini tafsiri ya kingereza imesalimika na upotoshaji huu.

“9Wala msimuite yeyote baba hapa duniani, kwa maana Baba yenu ni mmoja, Naye ni yule aliye mbinguni.”[9]

Kwa hiyo utapata kujua kuwa neno “baba” na “mwana” kwenye Injili linalenga Mola na waja. Linahusu watu wote na sio maalum kwa Masihi.

“36Habari ya siku ile na saa ile hakuna yeyote aijuaye, hata Malaika walio mbinguni, wala Mwana, isipokuwa Baba peke yake.”[10]

Hii ni dalili ya kukata kabisa ya kwamba Saa hakuna yeyote aijuaye isipokuwa Allaah. Kuna dalili vilevile ya kwamba elimu ya Masihi ni yenye kukomeka kama watu wengine wote. Allaah peke yake ndiye mjuzi wa kila kitu.

“39Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifulifuli na kuomba: “Baba yangu, ikiwezekana kikombe hiki kiniepuke. Lakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe.”[11]

Ikiwa kweli haya yamethibiti, basi mtu aliyeyasema alikuwa ni mjinga juu ya uwezo wa Allaah. Vilevile amekiri ya kwamba ni mja wa Allaah ambaye anamwendesha.

“7Wakafanya shauri wakavitumia kwa kununua konde la mfinyanzi liwe mahali pa kuzika wageni. 8Kwa hiyo konde lile huitwa konde la damu mpaka hii leo.”[12]

Kuanzia hapa tunapata kufahamu kuwa Injili haikuandikwa wakati wa Masihi. Iliandikwa muda mrefu baada yake na imejengwa juu ya simbulizi kwenye midomo ya watu.

“46Karibu na saa tisa, Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu akisema: “Eloi, Eloi, lama sabakthani?” (Maana yake: Mungu wangu, Mungu wangu, kwa nini umeniacha?).”[13]

Hii ni moja katika dalili kubwa yenye kuonyesha kuwa aliyesema maneno haya alikuwa hamuamini Allaah, sembuse kuwa ni Nabii wa Allaah. Mosi ni kwamba Allaah havunji ahadi Yake na pili Mitume wa Allaah hawatilii shaka juu ya ahadi Yake.

[1] Matayo 11:25

[2] Matayo 14:23

[3] 35:15

[4] 19:93

[5] Matayo 15:21-28

[6] Matayo 19:16-17

[7] Matayo 21:45-46

[8] Matayo 23:08

[9] Matayo 28:09

[10] Matayo 24:36

[11] Matayo 26:39

[12] Matayo 27:07-08

[13] Matayo 27:46

  • Mhusika: ´Allaamah Muhammad Taqiyy-ud-Diyn al-Hilaaliy al-Maghribiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Baraahiyn al-Injiylyyah ´alaa anna ´Iysaa daakhil fiyl-´Ubuudiyyah wa la hadhdhwa lahu fiyl-Uluuhiyyah, uk. 14-16
  • Imechapishwa: 16/10/2016