04. Abu Bakr al-Khatwiyb al-Baghdaadiy anaweka wazi madhehebu ya Salaf kuhusu sifa

15- al-Mubaarak bin ´Aliy as-Swayrafiy ametukhabarisha: Abul-Hasan Muhammad bin Marzuuq bin ´Abdir-Razzaaq az-Za´faraaniy ametuhadithia: Haafidhw Abu Bakr Ahmad bin ´Aliy bin Thaabit al-Khatwiyb ametuhadithia na kusema:

“Kuhusu sifa zilizipokelewa kutoka katika Sunnah Swahiyh, madhehebu ya Salaf (Radhiya Allaahu ´anhum) ilikuwa ni kuzithibitisha na kuzipitisha juu ya udhahiri wake na kuzikanushia namna na ushabihisho. Maudhui haya yamejengwa juu ya kwamba maneno kuhusu sifa ni kama maneno kuhusu dhati, mia kwa mia.

Ikiwa ni jambo lenye kutambulika ya kwamba kumthibitisha Mola (´Azza wa Jall) ni kuthibitisha uwepo Wake, na si kuthibitisha ukomo wala namna, kadhalika kuthibitisha sifa Zake ni kuthibitisha uwepo Wake, na si kuthibitisha ukomo wala namna.

Tukisema kuwa Allaah (Ta´ala) ana mkono, usikizi na uoni, basi huko ni kuzithibitisha sifa ambazo Yeye mwenyewe amejithibitishia. Hatusemi kuwa maana ya mkono ni uwezo wala kwamba maana ya kusikia na kuona ni elimu. Hatusemi kuwa ni viungo vya mwili na wala hatuzifananizi na mikono, usikizi wala maono ambavyo ni viungo vya mwili na nyenzo za matendo. Wahy umeyataja kwa njia ya kuzithibitisha. Vilevile ni wajibu kuzitakasia ushabihisho, kwa sababu Amesema (Tabaarak wa Ta´ala):

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖوَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.”[1]

وَلَمْ يَكُن لَّهُ كُفُوًا أَحَدٌ

”Wala hakuna yeyote anayefanana na kulingana Naye.”[2]

[1] 42:11

[2] 112:04

  • Mhusika: Imaam Muwaffaq-ud-Diyn bin Qudaamah al-Maqdisiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Dhamm-ut-Ta’wiyl, uk. 13