03. Washirikina wa sasa ni wabaya zaidi kuliko wa kale kwa sababu mbili

Washirikina waliokuja nyuma wanawashinda wale washirikina wa mwanzo. Kwa sababu shirki zao zinakuwa siku zote wakati wa raha na wakati wa shida. Wale wa kale walikuwa wakishirikisha kipindi cha raha peke yake. Ama wakati wa matatizo walikuwa ni wenye kumtakasia Allaah dini na maombi. Amesema (Ta´ala):

فَإِذَا رَكِبُوا فِي الْفُلْكِ دَعَوُا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ فَلَمَّا نَجَّاهُمْ إِلَى الْبَرِّ إِذَا هُمْ يُشْرِكُونَ

“Wanapopanda merikebu basi humwomba Allaah hali ya kumtakasia Yeye dini, lakini anapowaokoa katika nchikavu, tahamaki hao wanamshirikisha.”[1]

Ama kuhusu washirikina hawa wa leo ambao wanamwabudu al-Badawiy, wanaomwabudu al-Husayn, wanaomwabudu ´Abdul-Qaadir al-Jaylaaniy na wengineo shirki zao zinakuwa siku zote. Ni mamoja wakati wa raha na wakati wa shida. Wao shirki zao zinakuwa mbaya zaidi kuliko wale wa kale, zenye dhambi zaidi na mbaya zaidi. Baadhi yao wanafikia kushikirisha mpaka katika utendakazi wa Allaah. Baadhi yao wanawafanya wale waungu wao ni wenye kushirikiana na Allaah katika kuendesha ulimwengu. Hii ni shirki nyingine. Huku ni kushirikisha katika utendakazi wa Allaah.

Tunacholenga ni kwamba shirki za waliokuja nyuma ni mbaya zaidi kuliko shirki za wale waliotangulia na ni mbaya zaidi kwa sababu mbili:

Ya kwanza: Wanashirikisha nyakati zote; wakati wa raha na wakati wa shida. Hivo ni tofauti na wale wa kale.

Ya pili: Wengi wao wamefikia mpaka kuwashirikisha waungu wao katika kuyaendesha mambo; katika kuumba viumbe na kuruzuku ulimwengu. Jambo hili ni baya zaidi kuliko shirki za wale wa kale, khatari zaidi, upotevu zaidi na liko mbali zaidi na uongofu.

[1] 29:65

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 10-11
  • Imechapishwa: 10/08/2020