1- Ubainifu wa mfumo wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah katika majina na sifa za Allaah (Ta´ala) pamoja na baadhi ya mifano inayoweka wazi mfumo huo:

Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah mfumo wao katika majina na sifa za Allaah ni kwamba wanazingatia yale majina na sifa zilizothibitisha kwa Allaah katika Qur-aan au yaliyosihi kupokelewa kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Nayo ni haki juu ya uhakika wake na kikusudiwacho ni udhahiri wake. Hayahitajii upotoshaji wa wapotoshaji. Kwa sababu upotoshaji wa wapotoshaji umejengeka juu ya kufahamu vibaya au lengo baya. Kwani wamedhania kwamba wakithibitisha maandiko hayo au majina na sifa hizo juu ya udhahiri wake basi kufanya hivo ni kuthibitisha ufanano. Matokeo yake ndipo wakawa ni wenye kuyakengeusha maneno kuyaondosha mahala pake stahiki. Kuna uwezekano wasiwe miongoni mwa wale waliofahamu hivo. Lakini wana ufahamu mbaya katika kuufarikisha Ummah huu wa Kiislamu makundimakundi na hivyo kila pote likawa ni lenye kufurahikia yale waliyomo.

Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wanaamini yale majina aliyojiita Allaah Mwenyewe na zile sifa alizojisifu nazo Mwenyewe ndani ya Qur-aan na kupitia kwa Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba ni haki juu ya uhakika na udhahiri wake. Hayahitajii upotoshaji wa wapotoshaji. Bali yamesalimika kabisa kutokamana na hayo. Isitoshe haiyumkiniki yakafahamika kwa mambo yasiyolingana na Allaah (´Azza wa Jall) katika sifa za upungufu au zinazofanana na viumbe. Kwa mfumo huu bora wanasalimika kutokamana na upindaji na kufuru juu ya majina na sifa za Allaah. Hawamthibitishii Allaah isipokuwa kile alichojithibitishia Mwenyewe au alichomthibitishia Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pasi na kuongeza wala kupunguza katika hayo. Kwa hiyo mfumo wao ni kwamba majina na sifa za Allaah ni kwa mujibu wa dalili kutoka katika Qur-aan na Sunnah. Haiwezekani kwa yeyote kumwita Allaah kwa yale ambayo hakujiita Mwenyewe au kumsifu Allaah kwa yale ambayo hakujisifu Mwenyewe.

Mtu yeyote mwenye kusema kwamba Allaah ana jina au sifa fulani au hana jina au sifa fulani pasi na dalili, hapana shaka kwamba amezungumza juu ya Allaah bila ya elimu. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema:

قُلْ إِنَّمَا حَرَّمَ رَبِّيَ الْفَوَاحِشَ مَا ظَهَرَ مِنْهَا وَمَا بَطَنَ وَالْإِثْمَ وَالْبَغْيَ بِغَيْرِ الْحَقِّ وَأَن تُشْرِكُوا بِاللَّـهِ مَا لَمْ يُنَزِّلْ بِهِ سُلْطَانًا وَأَن تَقُولُوا عَلَى اللَّـهِ مَا لَا تَعْلَمُونَ

“Sema: “Hakika Mola wangu ameharamisha machafu, yaliyodhihirika na yaliyofichika na dhambi [aina zote] na ukandamizaji bila ya haki. Na [ameharamisha] kumshirikisha Allaah kwa ambayo hakukiteremshia mamlaka na kuzungumza juu ya Allaah yale ambayo hamyajui.”[1]

وَلَا تَقْفُ مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ ۚ إِنَّ السَّمْعَ وَالْبَصَرَ وَالْفُؤَادَ كُلُّ أُولَـٰئِكَ كَانَ عَنْهُ مَسْئُولًا

“Wala usifuatilie yale usiyo na elimu nayo. Kwani hakika masikio na macho na moyo vyote hivyo vitaulizwa.”[2]

[1] 07:33

[2] 17:36

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Manhaj Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah fiy-´Aqiydah wal-´Amal, uk. 08-10
  • Imechapishwa: 21/06/2019