Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Ukishajua kuwa Allaah amekuumba ili umwabudu Yeye, basi jua ya kwamba ´ibaadah haiitwi kuwa ni ´ibaadah, pasi na Tawhiyd. Kama jinsi kuswali hakuitwi kuswali, pasi na wudhuu´. Shirki ikichanganyika na ´ibaadah inabatilika kama jinsi wudhuu´ unavyobatilika unapoingiliwa na hadathi.

MAELEZO

Bi maana ukishaitambua Aayah:

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ

“Na Sikuumba majini na wanadamu isipokuwa waniabudu.” (51:56)

na wewe ni katika wanaadamu na hivyo inakugusa pia. Umejua kuwa Allaah hakukuumba pasi na malengo, kwa sababu ule na unywe, au kwa sababu uishi maisha haya na uburudike na kufurahika. Hakukuumba kwa sababu ya mambo haya. Amekuumba ili umwabudu. Amekuumbia viumbe hivi ili vikuwepesishie kumwabudu Yeye, kwa sababu huwezi kuishi bila vitu hivi. Vilevile huwezi kumwabudu isipokuwa kwa vitu hivi. Allaah amekuwepesishia navyo ili umwabudu, sio kwa ajili ufurahi navyo, wende huku na kule ukiwa na furaha, ufanye dhambi, ule na unywe kile unachotaka. Hivi ndivyo wanavyofanya wanyama. Mwanaadamu ameumbwa na Allaah (Jalla wa ´Alaa) kwa ajili ya lengo kubwa na hekima kubwa, nayo ni kumwabudu Allaah. Amesema (Ta´ala):

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ

“Na Sikuumba majini na wanadamu isipokuwa waniabudu.”

Allaah hakukuumba ili umruzuku au umkusanyie pesa. Hivi ndivyo wanavyofanyiana wanaadamu pindi wanapofanyiana kazi ili kukusanya mapato. Allaah ni mkwasi kwa haya. Allaah hawahitajii viumbe. Amesema:

مَا أُرِيدُ مِنْهُم مِّن رِّزْقٍ وَمَا أُرِيدُ أَن يُطْعِمُونِ

“Sitaki kutoka kwao riziki yoyote na wala sitaki wanilishe.” (51:57)

Allaah (Jalla wa ´Alaa) anawalisha wenye njaa na halishwi. Hahitajii chakula. Yeye (Jalla wa ´Alaa) ni mkwasi na wala hana haja ya ´ibaadah zako. Ufalme Wake haupungui kitu ukikufuru. Wewe ndiye unayemuhitaji. Wewe ndiye mwenye haja ya ´ibaadah. Katika rehema Zake ni kuwa amekuamrisha kumwabudu. Ni kwa ajili ya maslahi yako. Ukimwabudu, basi (Subhaanahu wa Ta´ala) atakukirimu kwa malipo na thawabu. ´Ibaadah ni sababu ya Allaah kukukirimu duniani na Aakhirah. Hivyo basi, ni nani anayefaidika kwa ´ibaadah? Ambaye anafaidika kwa ´ibaadah ni mja Mwenyewe. Kuhusu Allaah (Jalla wa ´Alaa), Yeye amejitosheleza na waja Wake.

“… basi jua ya kwamba ´ibaadah haiitwi kuwa ni ´ibaadah, pasi na Tawhiyd. Kama jinsi kuswali hakuitwi kuswali, pasi na wudhuu´.”

Ukishatambua kuwa Allaah amekuumba ili umwabudu, basi kadhalika unatakiwa kujua kuwa ´ibaadah ambayo Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) anairidhia haiwi sahihi yenye kuridhiwa na Allaah mpaka itimize sharti mbili. Kukikosekana sharti moja wapo, inabatilika.

1 – Kitendo hicho awe ametekelezewa Allaah peke yake na kiwe kimetakasika na aina zote za shirki. Kikichanganyika na shirki, kinabatilika. Kwa mfano wudhuu´ unachenguka iwapo utachanganyika na hadathi. Vivyo hivyo ´ibaadah yako inabatilika ukimwabudu Allaah na baada ya hapo ukatumbukia katika shirki.

2 – Kumfuata Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kila ´ibaadah ambayo hakuweka Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni batili na ni yenye kukataliwa na kwamba ni Bid´ah na ukhurafi. Kwa ajili hii amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Yeyote atakayefanya kitendo kisichoafikiana na amri yetu, basi atarudishiwa.”[1]

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Yeyote atakayezua katika amri yetu hii yasiyokuwemo, atarudishiwa.”[2]

´Ibaadah ni lazima iwe yenye kuafikiana na yale aliyokuja nayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), sio na yale ambayo watu wanaonelea kuwa ni mazuri na nia na makusudio yao mema. Muda wa kuwa hakisapotiwi na dalili kutoka katika Shari´ah, basi kitendo hicho ni Bid´ah isiyomfaa mwenye nayo. Uhakika wa mambo ni kuwa kinamdhuru kwa sababu ni maasi hata kama atadai kuwa anajikurubisha kwacho kwa Allaah (´Azza wa Jall).

Kwa hiyo ni lazima ´ibaadah itimize sharti mbili hizi ili iweze kuwa sahihi na yenye kumfaa mwenye nayo; kumtakasia nia Allaah na yenye kuafikiana na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ikichanganyika na shirki, inabatilika, na ikichanganyika na Bid´ah isiyokuwa na msingi, inabatilika pia. Hakuna faida ya ´ibaadah ikiwa haikutimiza sharti hizi mbili kwa sababu itakuwa inahusiana na kitu ambacho hakikuwekwa katika Shari´ah na Allaah (´Azza wa Jall). Allaah anakubali tu yale aliyoyaweka katika Kitabu Chake au kupitia Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Hakuna kiumbe yeyote ambaye ni wajibu kumfuata asiyekuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wengine wote wanafuatwa na kutiiwa kwa sababu tu wamemfuata na kumtii Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hata hivyo hawafuatwi ikiwa hawatomfuata Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Allaah (Ta´ala) amesema

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَأُولِي الْأَمْرِ مِنكُمْ

”Enyi mlioamini! Mtiini Allaah na mtiini Mtume na wenye madaraka katika nyinyi.” (04:59)

Wenye madaraka ni wale watawala na wanazuoni. Ni wajibu kuwatii na kuwafata endapo watamtii Allaah. Hata hivyo haitofaa kuwatii wala kuwafuata ikiwa wataenda kinyume na Allaah. Hakuna kiumbe yeyote ambaye anatakiwa kutiiwa yeye kama yeye isipokuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wengine wote wanatiiwa na kufuatwa wakimfuata na kumtii Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hii ndio ´ibaadah sahihi.

[1] Muslim (1718).

[2] al-Bukhaariy (2697) na Muslim (1718)

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Qawaa´id al-Arba´ah, uk. 14-16
  • Imechapishwa: 18/08/2022