Swali: Tunataraji kuwekewa wazi hukumu ya kuwategemea mawalii, kuwaabudia, kutahadharisha na kuzindua jambo hilo.

Jibu: Mawalii ni waumini na wanaingia Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) na wale wenye kuwafuata kwa wema. Ni wale wenye kumcha Allaah na wakawa na imani. Nao ni wale wenye kumtii Allaah na Mtume Wake. Wote hawa ni mawalii. Ni mamoja wakawa ni waarabu au wasiokuwa waarabu, weupe au weusi, matajiri au masikini, viongozi au raia, wanamme au wanawake. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema:

أَلَا إِنَّ أَوْلِيَاءَ اللَّـهِ لَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ الَّذِينَ آمَنُوا وَكَانُوا يَتَّقُونَ

“Tanabahi! Hakika mawalii wa Allaah hawana khofu juu yao na wala hawatohuzunika. Ambao wameamini na wakawa wanamcha.”[1]

Hawa ndio mawalii wa Allaah ambao wamemtii Allaah na Mtume Wake na wakaogopa ghadhabu Zake na hivyo wakatekeleza haki Yake na wakajiepusha na yale aliyokataza. Hawa ndio mawalii na ndio waliotajwa katika maneno Yake Allaah (Ta´ala):

وَمَا كَانُوا أَوْلِيَاءَهُ ۚ إِنْ أَوْلِيَاؤُهُ إِلَّا الْمُتَّقُونَ

“Na hawakuwa ni mawalii Wake. Hawakuwa mawalii Wake isipokuwa wenye kumcha Allaah.”[2]

Sio wale wachawi, wenye kudai kuwa na mambo yasiyokuwa ya kawaida na karama za uwongo. Si venginevyo ni wale wenye kumwamini Allaah na Mtume Wake na wenye kutii maamrisho ya Allaah na Mtume Wake kama ilivyotangulia. Haijalishi kitu wameyafikia makarama au hawakuyafikia.

Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndio wenye kumcha Allaah zaidi na ndio wabora zaidi wa watu baada ya Mitume. Wengi wao hawakufikia yale mambo yasiyokuwa ya kawaida ambayo yanaitwa ´makarama` licha ya ile imani, uchaji na elimu waliokuwa nayo juu ya Allaah na dini Yake. Allaah akawatosheleza kwa hayo kutokamana na makarama. Amesema (Subhaanah) kuhusu Malaika:

لَا يَسْبِقُونَهُ بِالْقَوْلِ وَهُم بِأَمْرِهِ يَعْمَلُونَ يَعْلَمُ مَا بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَمَا خَلْفَهُمْ وَلَا يَشْفَعُونَ إِلَّا لِمَنِ ارْتَضَىٰ وَهُم مِّنْ خَشْيَتِهِ مُشْفِقُونَ

”Hawamtangulii kwa maneno, nao kwa amri Yake wanatenda. Anayajua yale yaliyoko mbele yao na yale yaliyoko nyuma yao na wala hawataomba uombezi wowote isipokuwa kwa yule ambaye amemridhia, nao kwa ajili ya kumwogopa wananyenyekea.”[3]

Haijuzu kwa yeyote kuabudia Mitume, Malaika au mawalii wengineo. Wala haifai akawawekea nadhiri, akawachinjia, akawaomba kuwaponya wagonjwa, kuwaomba nusura dhidi ya maadui au aina nyenginezo za ´ibaadah. Amesema (Ta´ala):

وَأَنَّ الْمَسَاجِدَ لِلَّـهِ فَلَا تَدْعُوا مَعَ اللَّـهِ أَحَدًا

“Sehemu zote za kuswalia ni kwa ajili ya Allaah, hivyo basi msiombe yeyote pamoja na Allaah.”[4]

وَقَضَىٰ رَبُّكَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ

“Mola wako ameamuru kwamba: “Msiabudu isipokuwa Yeye pekee.”[5]

Maana yake ni kwamba ameamrisha na ameusia.

Vilevile amesema (Ta´ala):

وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ حُنَفَاءَ

“Hawakuamrishwa jengine isipokuwa wamwabudu Allaah hali ya kumtakasia Yeye dini kwa kujiengua na shirki na kuelemea Tawhiyd.”[6]

Zipo Aayah nyingi zenye maana kama hii.

Vivyo hivyo haijuzu kutufu makaburi ya mawalii wala ya wengineo. Twawaaf ni kitu maalum kwa Ka´bah tukufu. Vilevile haijuzu kuzunguka kitu kingine. Yeyote anayetufu kaburi akiwa ni mwenye kujikurubisha kwa yule mwenye nalo basi ameshirikisha. Ni kama ambavo ataswali kwa ajili yao, akawataka uokozi au akawachinjia. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

قُلْ إِنَّ صَلَاتِي وَنُسُكِي وَمَحْيَايَ وَمَمَاتِي لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ لَا شَرِيكَ لَهُ ۖ وَبِذَٰلِكَ أُمِرْتُ وَأَنَا أَوَّلُ الْمُسْلِمِينَ

”Sema: “Hakika swalah yangu na kichinjwa changu na uhai wangu na kufa kwangu ni kwa ajili ya Allaah pekee, Mola wa walimwengu, hali ya kuwa hana mshirika; na kwa hayo ndio nimeamrishwa, nami ni muislamu wa kwanza.”[7]

Kuhusu kuwaomba viumbe, waliohai, waweza na walioko mbele yako wakusaidie katika yale wanayoyaweza sio katika shirki. Bali hayo yanafaa. Kama vile alivosema Allaah (´Azza wa Jall) katika kisa cha Muusa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

فَاسْتَغَاثَهُ الَّذِي مِن شِيعَتِهِ عَلَى الَّذِي مِنْ عَدُوِّهِ

“Akamsaidia yule ambaye katika kundi lake dhidi ya yule ambaye ni katika adui wake.”[8]

وَتَعَاوَنُوا عَلَى الْبِرِّ وَالتَّقْوَىٰ ۖوَلَا تَعَاوَنُوا عَلَى الْإِثْمِ وَالْعُدْوَانِ

“Saidiane katika wema na kumcha Allaah na wala msisaidiane katika dhambi na uadui.”[9]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah yuko katika kumsaidia mja muda wa kuwa mja yuko katika kumsaidi nduguye.”[10]

Aayah na Hadiyth zenye maana kama hii ni nyingi. Ni jambo ambalo waislamu wameafikiana juu yake.

[1] 10:62-63

[2] 08:34

[3] 21:27

[4] 72:18

[5] 17:23

[6] 98:05

[7] 06:162-163

[8] 28:15

[9] 05:02

[10] Muslim (2699).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tahdhiyr min Fitnat-il-Qubuur, uk. 14-17
  • Imechapishwa: 06/04/2022