Ni tangu kipindi kile mtu anapobaleghe mpaka mwishoni mwa ujana. Hii ndio hatua kubwa ambayo ina mapambano dhidi ya nasfi, matamanio na utawala wa shaytwaan. Anayechunga hatua hii basi humkaribia Allaah. Wakati hatua hii inapopuuzwa basi hutokea khasara kubwa. Hapa ndipo wanasifiwa wale wenye subira pindi wanaposubiri kutotumbukia katika makosa. Kama ambavyo Allaah (´Azza wa Jall) alivyomsifu Yuusuf (´alayhis-Swalaatu was-Salaam). Lau angeliteleza angelukuwa nani?

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mola wako anashangazwa na kijana asiyehadaika na mambo ya kipuuzi na matamanio.”[1]

Aliyebaleghe anatakiwa kujua kuwa pale tu anapobaleghe ni wajibu kwake kumtambua Allaah (Ta´ala) kwa dalili na isiwe kwa kufuata kichwa mchunga. Kama dalili inatosha kwake kuitazama nafsi yake na namna ulivyojengeka mwili wake. Hapa ndipo atajua kuwa ujenzi wa mwili huu ni lazima uwe na ambaye aliupangilia kama ambavyo ni lazima jengo liwe na aliyelijenga.

Anapaswa vilevile kutambua kuwa ameteremshiwa Malaika wawili wataokuwa pamoja naye katika maisha yote. Watayaandika matendo yake na kumuonyesha nayo Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Allaah (Ta´ala) amesema:

وَإِنَّ عَلَيْكُمْ لَحَافِظِينَ كِرَامًا كَاتِبِينَ يَعْلَمُونَ مَا تَفْعَلُونَ

“Hakika juu yenu kuna wenye kuhifadhi, waandishi watukufu, wanayajua yale mfanyayo.”[2]

Muhammad bin al-Fadhwl amesema:

“Kwa muda wa miaka ishirini sijawapa chochote wanaoandika madhambi yangu. Na lau ningefanya hivo basi ningeliwaonea haya.”

Kwa hivyo mja anatakiwa kuangalia ni kipi kinachopandishwa katika matendo yake. Endapo atakosea basi aliondoshe kosa hilo kwa kutubu na kujirekebisha.

Anatakiwa vilevile kuyateremsha macho yake. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

قُل لِّلْمُؤْمِنِينَ يَغُضُّوا مِنْ أَبْصَارِهِمْ

“Waambie waumini wanaume wainamishe macho yao.”[3]

Atosheke na mwanamke mmoja. Asitumie fursa ya kukithirisha kustarehe na wanawake. Hilo litamfanya tu kuutawanyisha moyo wake na kuzidhoofisha nguvu zake – na hilo halina mwisho.

Kuna watuwazima wengi ambao walikuwa wakisikitika juu ya ule muda wao wa ujana walioupoteza. Walikuwa wakilia juu ya ule muda walioutumia vibaya. Hebu yule ambaye itafikia siku akae chini asimame sana usiku aswali. Hebu yule ambaye itafikia siku ashikwe na udhaifu akithirishe kufunga.

Watu wako sampuli tatu. Kuna watu wanaoyatumia maisha yao katika kheri na kudumu juu yake. Hao ni wenye kufuzu. Kuna watu wanaochanganya mazuri na mabaya na kufanya mapungufu. Hao ni wenye kukhasirika. Kuna watu wenye kuzembea na kutendea maasi. Hao wameangamia.

Hivyo basi kijana atazame yuko mahala gani. Hakuna nafasi ambayo ni yake. Hebu atazame utukufu wa bidhaa yake na thamani yake. Subira! Subira! Mpambanaji anasubiri na kutokuoa pamoja na nguvu ya matamanio yake. Anasifiwa kwa hilo. Kwa ajili hiyo kijana anatakiwa kusubiri ili aje kuambiwa:

هَـٰذَا يَوْمُكُمُ الَّذِي كُنتُمْ تُوعَدُونَ

“Hii ni ile Siku yenu mlokuwa mkiahidiwa.”[4]

Anatakiwa kutahadhari na makosa ya vijana. Ni kama kasoro ilio kubwa katika bidhaa nzuri. Yule anayeteleza katika ujana wake basi atazame kule kustarehe kwake kuko wapi. Ni kipi kinachobaki kama si khasara tu yenye kudumu ambayo kila anapoikumbuka inamuumiza? Kuikumbuka inakuwa adhabu. Yule anayetoboa tundu katika vazi la uchaji Allaah inauzwa kwa vilivyochanika na kuraruka.

al-Junayd (Rahimahu Allaah) amesema:

“Lau mja atamuabudu Allaah kwa miaka elfumoja kisha akampa mgongo kwa muda mchache basi yale yatayokuwa yamempita yatakuwa mengi kuliko yale aliyoyafikia.”[5]

Baadhi ya Salaf wamesema:

“Natamani lau mikono yangu ingekatwa ili tu nisamehewe madhambi ya ujanani mwangu.”

Siku moja wakati wa mawaidha nilisema:

“Kijana! Wewe uko katika jangwa na uko na vyombo vya thamani unavyotaka kuvifikisha katika nchi ya malipo. Tahadhari usije kuviuza kwa matamanio kwa ajili ya thamani ya chini. Pindi unapofika katika mji huo unawaona watu waliopata faida kwa biashara zao ilihali wewe ni mwenye kusikitika na kulia kwa majuto.”

[1] Ahmad (1/151).

[2] 82:10-12

[3] 24:30

[4] 21:103

[5] Hilyat-ul-Awliyaa’ (10/278).

  • Mhusika: Imaam ´Abdur-Rahmaan bin al-Jawziy al-Hanbaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tanbiyh-un-Naa’im al-Ghamr ´alaa Mawswim-il-´Umr, uk. 55-64
  • Imechapishwa: 15/02/2017