02. Kushikamana na mfumo wa Salafiyyah ndio suluhu


Ni lazima mgawanyiko utokee na umeshatokea, kama alivyotujuza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Njia ya uokovu ni kushikamana na yale aliyokuwa akifuata Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah wake. Hili kundi ndio kundi lililookoka na Moto, Firqat-un-Naajiyah. Makundi mengine yote yataingia Motoni. Hivyo ndio maana likaitwa kundi lililookoka, Firqat-un-Naajiyah; ambao ni Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Hili ndio kundi linalotofautiana na mengine kwa kufuata kwao Qur-aan na Sunnah. Makundi mengine yote yanayoenda kinyume nalo, basi ni makundi potofu hata kama yatajinasibisha na Ummah huu. Mfumo wa makundi hayo yanakwenda kinyume na mfumo wa Mtume (swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah wake. Haya ni katika ukamilifu wa kuwapendea kwake kheri (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) watu. Njia iko wazi; inahusiana na kufuata Qur-aan na Sunnah na yale waliyokuwemo Salaf wahenga wa Ummah huu; ambao ni Maswahabah, Taabi´uun na waliokuja baada ya Taabi´uun mpaka mwisho wa karne bora. Mwisho wake ni katika karne ya tatu au ya nne. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Karne bora ni yangu, kisha itayofuatia kisha itayofuatia.. .”

Mpokezi wa Hadiyth hii amesema:

“Sikumbuki baada ya karne yake alitaja karne mbili au tatu.”

“… halafu watajitokeza watu ambao wenye kuapa na hawakuombwa kufanya hivo, wenye kutoa ushahidi na hawakuombwa kufanya hivo, watafanya khiyana na hawatoaminiwa na itadhihiri kwao kupenda sana dunia.”

Baada ya karne bora ndio kutapitika mambo haya. Lakini yule mwenye kufuata mfumo wa karne bora, hata kama atakuwa katika siku ile ya mwisho ya kumalizika kwa dunia, ataokoka na kusalimika na Moto. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

وَالسَّابِقُونَ الأَوَّلُونَ مِنَ الْمُهَاجِرِينَ وَالأَنصَارِ وَالَّذِينَ اتَّبَعُوهُم بِإِحْسَانٍ رَّضِيَ اللّهُ عَنْهُمْ وَرَضُواْ عَنْهُ وَأَعَدَّ لَهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي تَحْتَهَا الأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا ذَلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ

Na wale waliotangulia awali miongoni mwa al-Muhaajiriyn na al-Answaar na wale waliowafuata kwa wema Allaah Ameridhika nao nao wameridhika Naye. Na Amewaandalia Mabustani yapitayo chini yake mito, watadumu humo milele. Huko ndiko kufuzu kukuu.” (09:100)