Waislamu, kuanzia zama za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), walikuwa ni Ummah mmoja peke yake. Amesema (Ta´ala):

إِنَّ هَـٰذِهِ أُمَّتُكُمْ أُمَّةً وَاحِدَةً وَأَنَا رَبُّكُمْ فَاعْبُدُونِ

“Hakika huu ummah wenu ni ummah mmoja – Nami ni Mola wenu, hivyo basi niabuduni.”[1]

Mayahudi na wanafiki walijaribu mara nyingi kuwafarikisha waislamu kipindi cha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), lakini hata hivyo hawakuweza. Wanafiki walisema:

لَا تُنفِقُوا عَلَىٰ مَنْ عِندَ رَسُولِ اللَّـهِ حَتَّىٰ يَنفَضُّوا

“Msitoe [mali] kwa ajii ya walioko kwa Mtume wa Allaah mpaka watokomee.”

Allaah akawaraddi kwa kusema:

وَلِلَّـهِ خَزَائِنُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَلَـٰكِنَّ الْمُنَافِقِينَ لَا يَفْقَهُونَ

“Na ni za Allaah pekee hazina za mbingu na ardhi, lakini wanafiki hawafahamu.”[2]

Mayahudi pia walijaribu kuwafarikisha na kuwaritadisha waislamu kutoka nje ya dini yao:

وَقَالَت طَّائِفَةٌ مِّنْ أَهْلِ الْكِتَابِ آمِنُوا بِالَّذِي أُنزِلَ عَلَى الَّذِينَ آمَنُوا وَجْهَ النَّهَارِ وَاكْفُرُوا آخِرَهُ لَعَلَّهُمْ يَرْجِعُونَ

“Kundi miongoni mwa Ahl-ul-Kitaab likasema: “Aminini yale ambayo yameteremshwa kwa wale walioamini mwanzo wa mchana na kanusheni mwisho wake wapate kurejea.”[3]

Lakini mikakati yote hii haikufanikiwa kwa sababu Allaah aliifichua na kuifedhehesha. Wakajaribu tena kwa mara nyingine kwa kuwatajia Answaaar uadui, vita na mashairi ya kejeli yaliyopitika kati yao kabla ya Uislamu. Allaah akafichua mikakati yao na kusema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِن تُطِيعُوا فَرِيقًا مِّنَ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ يَرُدُّوكُم بَعْدَ إِيمَانِكُمْ كَافِرِينَ

“Enyi mlioamini! Mkilitii kundi la waliopewa Kitabu watakurudisheni kuwa makafiri baada ya kuamini kwenu.”[4]

Mpaka alipofikia (Ta´ala) kusema:

يَوْمَ تَبْيَضُّ وُجُوهٌ وَتَسْوَدُّ وُجُوهٌ ۚ

“Siku [baadhi ya] nyuso zitakuwa nyeupe na zengine zitakuwa nyeusi.”[5]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwajia Answaar ambapo akawawaidhi na kuwakumbusha kuhusu neema ya Uislamu na namna walivyokuwa na umoja kupitia yeye baada ya kufarikiana ambapo wakapeana mikono na kukumbatiana. Matokeo yake zikafeli propaganda za mayahudi na waislamu wakabaki na umoja wao. Allaah (Ta´ala) amewaamrisha wawe na umoja juu ya haki na akawakataza tofauti na kufarikiana. Amesema (Ta´ala):

وَلَا تَكُونُوا كَالَّذِينَ تَفَرَّقُوا وَاخْتَلَفُوا مِن بَعْدِ مَا جَاءَهُمُ الْبَيِّنَاتُ

“Wala msiwe kama wale waliofarikiana na wakakhitilafiana baada ya kuwajia ubainifu.”[6]

وَاعْتَصِمُوا بِحَبْلِ اللَّـهِ جَمِيعًا وَلَا تَفَرَّقُوا

“Shikamaneni kwa kamba ya Allaah nyote pamoja na wala msifarikiane.”[7]

Hakika (Subhaanah) amewawekea Shari´ah ya kukusanyika katika kutekeleza ´ibaadah mbalimbali ikiwemo swalah, swawm, hajj na kujifunza elimu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akisisitiza kuwakusanya waislamu na wakati huohuo akiwakataza kufarikiana na kutofautiana. Isitoshe Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akieleza maelezo yaliyo na maana ya masisitizo juu ya kukusanyika na yakikataza kufarikiana. Alikuwa akieleza kuhusu namna ambavyo kutatokea mfarakano katika Ummah huu kama ulivyotokea katika nyumati zilizokuwepo kabla yake pindi aliposema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakika yeyote atakayeishi kipindi kirefu katika nyinyi basi atakuja kuona tofauti nyingi. Hivyo basi, jilazimieni na Sunnah zangu na Sunnah za makhaliyfah wangu waongofu na wenye kuongoza baada yangu.”[8]

“Mayahudi wamefarikiana katika mapote sabini na moja. Manaswara wamefarikiana katika mapote sabini na mbili. Ummah huu utafarikiana katika mapote sabini na tatu. Yote yataingia Motoni isipokuwa moja tu.” Tukasema: “Ni wepi hao, ee Mtume wa Allaah?” Akasema: “Ni wale wataofuata yale ninayofuata mimi hii leo na Maswahabah zangu.”[9]

Yametokea yale aliyoelezea Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ummah ulifarikiana mwishoni mwa wakati wa Maswahabah. Lakini hata hivyo tofauti hii haikuutikisa sana Ummah kwa muda ambapo karne bora – ambazo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amezisifu – bado zilikuwepo. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Wabora wenu ni karne yangu, kisha wataofuatia, kisha wataofuatia.”[10]

Mpokezi amesema:

“Sijui baada ya karne yake alitaja karne mbili au tatu.”

Hilo ni kwa sababu wanazuoni wa Hadiyth, wanazuoni wa tafsiri ya Qur-aan na wanazuoni wa Fiqh walikuwa wamejaa. Aidha wanazuoni wa Taabi´uun, waliokuja baada ya Taabi´uun, maimamu wanne, wanafunzi wao na nguvu ya nchi ya Kiislamu ilikuwepo katika karne zile. Kundi lililokuwa linakwenda kinyume lilikuwa linaraddiwa kwa dalili na kwa nguvu. Karne bora zilipoisha ndipo waislamu wakachanganyika na watu wa dini nyenginezo zinazoenda kinyume na elimu za watu wenye mila za kikafiri zikatafsiriwa kwa kiarabu na pia watawala wa Kiislamu wakawafanya marafiki zao wa karibu ni baadhi ya makafiri na wapotevu ambapo miongoni mwao wakawa ni mawaziri na washauri. Uongozi ukazidi kushika kasi na mapote na makundi yakawa mengi ambayo yalizalisha madhehebu mengi batili, jambo ambalo bado ni lenye kuendelea mpaka hii leo na mpaka pale Allaah atapotaka. Lakini himdi zote ni za Allaah kuona kundi lililookoka, Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah, bado ni wenye kuendelea kushikamana barabara na Uislamu sahihi ambapo wanapita juu yake, wanaita kwao na bado wanaendelea na hawatoacha kuendelea kuhakikisha ile hali aliyoielezea Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kuendelea kubaki na kusimama imara kikundi hiki. Hiyo ni fadhilah ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ili dini hii iweze kubaki na kuwasimamishia hoja wakaidi.

Hakika kundi hili lililobarikiwa linawakilisha yale maneno, matendo na ´Aqiydah aliokuwa nayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pamoja na Maswahabah zake (Radhiya Allaahu ´anhum). Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Ni wale wataofuata yale ninayofuata mimi hii leo na Maswahabah zangu.”

Wao ndio wale watu waledi na wema waliobakia ambao Allaah amesema juu yao:

فَلَوْلَا كَانَ مِنَ الْقُرُونِ مِن قَبْلِكُمْ أُولُو بَقِيَّةٍ يَنْهَوْنَ عَنِ الْفَسَادِ فِي الْأَرْضِ

“Basi kwa nini hawakuweko katika karne za kabla yenu watu weledi wanakataza ufisadi katika nchi, isipokuwa wachache tu.”[11]

[1] 21:92

[2] 63:07

[3] 03:72

[4] 03:100

[5] 03:106

[6] 03:10

[7] 03:103

[8] Abu Daawuud (4609), at-Tirmidhiy (2676), Ibn Maajah (46) na Ahmad (17184)

[9] at-Tirmidhiy (2641).

[10] al-Bukhaariy (6508), Muslim (2535), at-Tirmidhiy (2222), an-Nasaa´iy (3809), Abu Daawuud (4657), Ibn Maajah (2362) na Ahmad (04/427).

[11] 11:116

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Min Usuwl ´Aqiydah Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah, uk. 07-12
  • Imechapishwa: 12/05/2022