Allaah (´Azza wa Jall) ametuamrisha kufunga Ramadhaan ili kushukuru neema ya Qur-aan. Neema ya Qur-aan haiwezi kulinganishwa na neema nyenginezo. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ameteremsha Qur-aan kwa lugha ya kiarabu ya wazi. Ameifanya ni yenye kubaki katika Ummah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mpaka siku ya Qiyaamah. Waislamu wanairejelea wanapofikwa na jambo. Wanachukua hukumu kutoka humo. Wanachukua mafunzo kutoka humo. Wanahukumiwa nayo wakati wa tofauti. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

وَمَا اخْتَلَفْتُمْ فِيهِ مِن شَيْءٍ فَحُكْمُهُ إِلَى اللَّـهِ

“Katika lolote lile mlilokhitilafiana, basi hukumu yake ni kwa Allaah.”[1]

Allaah ameufadhilisha mwezi huu kwa sababu ya fadhila za Qur-aan. Ameiteremsha ndani yake. Ameamrisha kufunga mchana na nyusiku zake  na kuutumia usiku kwa ajili ya swalah. Mchana wake unatakiwa kufungwa na nyusiku zake zinatakiwa kutumiwa katika swalah.

Katika Aayah hiyo hiyo Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ameeleza kuwa anataka kuwasahilishia Ummah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na hataki kuwafanyia uzito. Swawm inakuwa nyepesi kwa [kukusanyika] pamoja. Kwa ajili hiyo wanatakiwa wajiandae kwayo. Mwezi uwafikie ilihali wamejiandaa. Kunakuwa wepesi wa kufunga pindi wanapokuwa pamoja. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atayefunga Ramadhaan kwa imani na kutaraji malipo, atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia. Atayesimama [nyusiku za] Ramadhaan kwa imani na kutaraji malipo, atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia.”[2]

“Atayesimama [nyusiku za] Ramadhaan kwa imani na kutaraji malipo, atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia.”[3]

Imani na matarajio maana yake ni kusadikisha ahadi ya Allaah ya kwamba atawapa wafungaji malipo makubwa. Imepokelewa katika Hadiyth Swahiyh ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kila tendo jema la mwanaadamu linalipwa mara kumi mpaka mara mia saba. Allaah akasema: “Isipokuwa swawm. Hiyo ni Yangu na mimi Ndiye nitayeilipa. Ameacha matamanio Yake na chakula Chake na kinywaji Chake kwa ajili Yangu.” Mfungaji ana furaha mbili; furaha ya kwanza ni pale anapokata swawm yake na furaha nyingine ni pale atapokutana na Mola Wake. Harufu ya mfungaji inapendwa zaidi na Allaah kuliko harufu ya miski.”[4]

[1] 42:10

[2] al-Bukhaariy (1901) na (2014) na Muslim (760).

[3] al-Bukhaariy (37) na Muslim (759).

[4] al-Bukhaariy (5927) na Muslim (1151).

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Istiqbaal Shahri Ramadhwaan, uk. 23-26
  • Imechapishwa: 09/06/2017