Ina fadhilah kubwa na ina nafasi ya juu kwa Allaah. Mwenye kulitamka kikweli basi Allaah atamwingiza Peponi. Vilevile yule mwenye kulisema hali ya kuwa ni mwongo, damu na mali yake vitasalimishwa duniani na hesabu yake ataachiwa Allaah (´Azza wa Jall). Ni neno fupi kulitamka, herufi zake ni chache, jepesi kwenye ulimi lakini lenye uzito kwenye mizani. Ibn Hibbaan na al-Haakim, ambaye ameisahihisha pia, wamepokea kupitia kwa Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesimulia ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Muusa alisema: “Ee Mola Wangu! Nifunze kitu ambacho nitakukumbuka kwacho na kukuomba kwacho.” Akamwambia: “Ee Muusa! Sema: “Hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah.” Akasema: “Ee Mola! Waja Wako wote wanasema hivi.” Akasema: “Ee Muusa! Lau mbingu saba na vyote vilivyomo ndani yake mbali na Mimi na ardhi saba na vyote vilivyomo ndani yake vitawekwa kwenye kitanga kimoja cha mzani na “hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah” ikawekwa kwenye kitanga kingine, basi “hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah” ingevizidi uzito.”[1]

Hadiyth hii inafahamisha kwamba shahaadah ndio dhikr bora kabisa.

´Abdullaah bin ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesimulia kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliyesema:

”Du´aa bora ni ile ya ´Arafah na bora nilichosema mimi na Mitume wengine waliokuwa kabla yangu ni ´hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah hali ya kuwa yupekee hana mshirika. Ufalme wote ni Wake na himdi zote njema anastahiki Yeye – Naye juu ya kila kitu ni Muweza`.”

Ameipokea Ahmad na at-Tirmidhiy.

Miongoni mwa mambo yanayothibitisha namna lilivyo na uzito kwenye mizani ni yale yaliyopokelewa na at-Tirmidhiy na akayafanya kuwa ni mazuri, an-Nasaa´iy na al-Haakim ambaye amesema kuwa ni Swahiyh kwa mujibu wa masharti ya Muslim kupitia kwa ´Abdullaah bin ´Amr (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Siku ya Qiyaamah ataletwa mwanaume juu ya vichwa vya viumbe na aonyeshwe madaftari tisini na tisa [yaliyojaa madhambi]. Kila daftari [limejaa madhambi kwa] umbali wa kikomo cha macho. Aambiwe: “Unapinga chochote katika haya? Je, wahifadhi Wangu walikudhulumu?” Aseme: “Hapana, Mola wangu.” Kusemwe: “Hivi una udhuru au una tendo jema lolote?” Mtu huyo atanyamaza na aseme: “Hapana, Mola wangu.” Aambiwe: “Ndo, una tendo jema kwetu. Haudhulumiwi.” Halafu kutatolewa kadi iliyoandikwa ´hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni mja na Mtume Wake` iwekwe kwenye kitanga kimoja cha mzani. Atasema: “Ee Mola! Vipi kadi hii na madaftari yote haya?” Aambiwe: “Hutodhulumiwa.” Halafu kutawekwa yale madaftari kwenye kitanga kimoja cha mzani na ile kadi kwenye kitanga kingine cha mzani ambapo ile kadi itayashinda uzito yale madaftari.”

Neno hili lina fadhilah kubwa na nyingi ambazo jumla yazo zimetajwa na Haafidhw Ibn Rajab katika kijitabu chake “Kalimat-ul-Ikhlaasw” na akathibitisha kwa kila fadhilah aliyotaja, ikiwa ni pamoja na:

1 – Ndio thamani ya Pepo. Yule ambaye ndio yatakuwa maneno yake ya mwisho ataingia Peponi.

2 – Ndio yanayomuokoa mtu na Moto.

3 – Yanamuwajibishia mtu msamaha.

4 – Ndio wema mkubwa kabisa.

5 – Yanafuta madhambi na makosa ya mtu.

6 – Yanaifanya ile imani iliyomo moyoni kuwa mpya.

7 – Yanashinda uzito madaftari ya madhambi.

8 – Yanamwondoshea mtu vikwazo mpaka anafika kwa Allaah (´Azza wa Jall).

9 – Ndio maneno ambayo Allaah anamsadikisha nayo yule mwenye kuyatamka.

10 – Ndio tendo bora kabisa na lililo na thawabu nyingi ambalo ni sawa na kuacha watumwa huru.

11 – Ni kinga dhidi ya shaytwaan.

12 – Ndio neno la salama kutokamana na vitisho vya ndani ya kaburi na hali za kutisha za siku ya mkusanyiko.

13 – Ndio nembo ya waumini pindi wataposimama kutoka ndani ya makaburi yao.

14 – Miongoni mwa fadhilah zake vilevile ni kuwa linamfungulia yule mwenye kulitamka milango minane ya Peponi aingie kupitia mlango anaotaka.

15 – Miongoni mwa fadhilah zake vilevile ni kwamba wale wenye kulitamka, hata kama wataingia Motoni kwa sababu ya kufanyia upungufu zile haki zake, ni lazima tu watatoka.

Hivi ndio vichwa vya khabari vya fadhilah zake ambazo zimetajwa na Ibn Rajab katika kijitabu chake na akajengea dalili kwa kila fadhilah moja kaitka hizo[2].

[1] Ahmad (06/170).

[2] Kalimat-ul-Ikhlaasw, uk. 54-66

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ma´naa laa ilaaha illa Allaah, uk. 9-15
  • Imechapishwa: 23/09/2023