01. Sifa za mke mwema


Himidi zote anastahiki Allaah. Tunamhimidi Yeye na kumtaka msaada na kumuomba msamaha na kutubia Kwake. Tunajikinga Kwake kutokamana na shari ya nafsi zetu na uovu wa matendo yetu. Yule mwenye kuongozwa na Allaah, basi hakuna wa kumpoteza, na yule mwenye kupotezwa ba Allaah, hakuna wa kumwongoza. Nashuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah, hali ya kuwa ni Mmoja pekee asiyekuwa na mshirika. Nashuhudia ya kwamba Muhammad ni mja Wake na Mtume Wake.

Amma ba´d…

Maudhui ya kijitabu hiki kilicho na kichwa cha khabari ”Sifa za mke mwema” hayamuhusu tu msichana mdogo ambaye yuko njiani kutaka kuolewa ambaye anataka kuzijua sifa ambazo mke anatakiwa kuwa nazo ili aweze kujipamba nazo, kuishi nazo na kuzitimiza.

Vilevile hayamuhusu tu mwanamke ambaye ameolewa ambaye anataka kuwa na sifa za mke mwema ili aweze kuzidhibiti na kuishi nazo katika maisha yake.

Vilevile hayamuhusu tu mwanamke mwenye upungufu ili aweze kutibu upungufu wake na kujisahihisha mwenyewe na ndoa yake tukufu.

Bali ni wito na ukumbusho ulio jumla kuliko hivyo.

Ni ukumbusho kwa baba ambaye anataka wasichana wake na wanawake ambao wako katika usimamizi wake wapate kukuwa vizuri na malezi mazuri na ndoa ambayo inaafikiana na matakwa ya Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa kupitia kalima hii itakuwa ni usaidizi kwake kuweza kuwakumbusha vidhibiti vya Shari´ah na sifa ambazo inatakikana kwa msichana kukuwa juu yake.

Kadhalika ni ukumbusho kwa mama ambaye ni mchungaji katika nyumba yake na wasichana wake na kuwaelekeza. Wasichana wengi wanakuwa kwa tabia na sifa mbalimbali ambazo wamepata kutoka kwa mama zao.

Kadhalika ni ukumbusho kwa walinganizi ili waweze kulitilia uzito jambo hili, kulitilia umuhimu na kufanya juhudi katika kueneza sifa hizi tukufu, tabia zilizosifiwa na kazi iliyobarikiwa ili ziweze kupatikana kwa wasichana na wanawake katika jamii ya imani na majumbani. Hili na khaswa hii leo ambapo mwanamke ameshambuliwa kwa njia ambayo kamwe haijawahi kuonekana hapo kabla. Inafanyika kwa kutumia namna na njia mbalimbali. Malengo ni kutaka kumpotezea mwanamke usafi wake, utukufu wake, ukamilifu wake, fadhila zake, uzuri wake, imani yake, tabia yake na wema wake.

Hapo kabla ilikuwa ni vigumu sana kwa mwanamke kufikiwa na propaganda zinazoharibu, matamanio ya udanganyifu na maoni yaliyofungamana. Hilo lilikuwa likitendeka ima kwa kupitia rafiki mbaya au mfano wa hayo. Ama hii leo mwanamke anafikiwa na uchafu na uharibifu wote wa ulimwenguni nyumbani kwake. Hahitaji kutoka nje kwa ajili ya hilo. Sasa mwanamke anaweza kukaa chumbani mwake mbele ya TV, intaneti au magazeti machafu na akapata uchafu na shari zote katika moyo wake na fikra zake. Ili aweze kuwa mwema, mtwaharifu, mwenye dini na mwenye kumtii Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) analazimika kufunga madirisha, njia na vichochoro vyote vya shari na uharibifu.

Mwanamke ni jukumu kubwa kwa wale ambao Allaah amewabebesha usimamizi wake. Suala hili linahitajia kuliwekea umuhimi mkubwa kabisa.

Katika kivuli cha hali hii na upungufu wa ukumbusho wa imani, sifa njema na sifa nzuri ambazo mwanamke anatakiwa kujipamba nazo, wanawake wengi wamekuwa wadhaifu na wanyonge. Wametumbukia katika kuwa na upungufu wa haya na dini na kuanguka katika mapungufu na kasoro nyingi.

Kalima hii ni kama tulivyosema ni kuhusu sifa za mke mwema. Ninamuomba Allaah Mtukufu, Mola wa ´Arshi tukufu, aifanye iwe ya kheri na manufaa na afanye iwe ni ufunguo wa kheri na ufunge shari na uziongoze nyoyo, uzitengeneze nafsi na utengeneza mawasiliano na Mola wa walimwengu ili kuhakikisha radhi Zake na kuyafikia mapenzi Yake na kuyaepuka yale yanayomkasirisha na kumghadhibisha (Jalla wa ´Alaa).

  • Mhusika: Shaykh ´Abdur-Razzaaq bin ´Abdil-Muhsin al-´Abbaad
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifaat-uz-Zawjah as-Swaalihah, uk. 5-9
  • Imechapishwa: 04/06/2017