Mwezi wa Ramadhaan unathibiti kwa kuonekana mwezi mwandamo. Hili ni kwa mujibu wa wanachuoni wote. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Fungeni pindi mtapouona na fungueni pindi mtapouona. Iwapo mtafunikwa na wingu kamilisheni idadi ya [siku] thelathini.”

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Fungeni pindi mtapouona na fungueni pindi mtapouona. Iwapo mtafunikwa na wingu fungeni [siku] thelathini.”

Katika upokezi mwingine imekuja:

“… kamilisheni hesabu ya Sha´baan siku thelathini.”[1]

Kinacholengwa ni kwamba kunafungwa na kufunguliwa kwa kuonekana mwezi mwandamo. Endapo hautoonekana basi ni wajibu kukamilisha Sha´baan siku thelathini kisha wafunge. Kadhalika iwapo mwezi hautoonekana ni wajibu kukamilisha Ramadhaan siku thelathini kisha wafungue. Ama endapo mwezi utaonekana inatakiwa kuufuata na himdi zote anastahiki Allaah.

Ni wajibu kwa waislamu kufunga pindi wanapoona mwezi mwandamo.  Mwezi mwandamo wa Ramadhaan unakuwa usiku wa tarehe 30 Sha´baan. Katika hali hii Sha´baan inakuwa ni yenye kupungua na watu wanafunga siku ya kufuata. Hali kadhalika wakiona mwezi mwandamo usiku wa tarehe 30 Ramadhaan. Katika hali hii watakata swawm 29 Sha´baan. Iwapo hawatoona mwezi mwandamo watakamilisha Sha´baan siku thelathini na Ramadhaan siku thelathini kutokamana na Hadiyth:

“Fungeni pindi mtapouona na fungueni pindi mtapouona. Iwapo mtafunikwa na wingu kamilisheni idadi ya [siku] thelathini.”

Inahusu Sha´baan na Ramadhaan. Katika upokezi mwingine imekuja:

“Fungeni pindi mtapouona na fungueni pindi mtapouona. Iwapo mtafunikwa na wingu fungeni [siku] thelathini.”

Mwezi mwandamo unathibiti kwa kuonekana na mtu mmoja mwadilifu kwa mujibu wa maoni ya wanachuoni wengi. Imethibiti ya kwamba Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

“Watu waliuona mwezi. Nikamweleza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba nimeuona. Kwa hivyo akafunga na akawaamrisha watu wafunge.”

Vilevile pindi ilipothibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba bedui alimweleza (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba ameona mwezi. Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Unashuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba mimi ni Mtume wa Allaah?” Mtu yule akasema: “Ndio.” Baada ya hapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawaamrisha watu wafunge.”[2]

Mtu mwadilifu akiuona mwezi ni wajibu kufunga. Kuhusu kuisha kwa Ramadhaan, kunahitajika ushahidi wa mashahidi wawili waadilifu. Hali kadhalika miezi mingine; inathibitishwa kwa mashahidi wawili waadilifu. Imethibiti ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Pindi mashahidi wawili wataposhuhudia basi fungeni na fungueni.”[3]

Imethibiti ya kwamba al-Haarith bin Haatwib (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitupa kazi ya kwenda nje kutazama  [mwezi mwandamo]. Usipoonekana na wakashuhudia mashahidi wawili waadilifu tutafuata ushahidi wao.”[4]

Kwa hiyo kunahitajika ushahidi wa mashahidi wawili waadilifu kuuona mwezi mwandamo juu ya kuisha kwa Ramadhaan na miezi mingine. Kuhusu kuanza kwa Ramadhaan ndio unatosheleza ushahidi wa mtu mmoja mwadilifu, kutokana na Hadiyth zilizotangulia.

Wanachuoni wametofautiana kama ushahidi wa mwanamke unakubaliwa kama wa mwanaume juu ya kuanza kufunga au haukubaliwi. Kuna maoni mawili juu ya hilo. Baadhi wameukubali kama wanavyokubali Hadiyth yake endapo atakuwa ni mwaminifu. Wengine hawakuukubali.

Maoni sahihi ni kwamba haukubaliwi. Uwanja huu ni wa wanaume na ni maalum kwa wanaume. Wanaume ndio wenye kushuhudia hilo. Isitoshe wao ndio wajuzi zaidi juu ya mada hii.

Ikiwa siku ya tarehe thelathini Sha´baan haukuthibitishwa kwa kuonekana mwezi mwandamano hiyo inaitwa ni “siku ya Shaka”. Haijuzu kuifunga kutokana na maoni sahihi ya wanachuoni. Ni mamoja siku hiyo ikawa nyeupe au na mawingu. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Fungeni pindi mtapouona na fungueni pindi mtapouona. Iwapo mtafunikwa na wingu kamilisheni hesabu ya Sha´baan siku thelathini.”

Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Msifunge siku moja au mbili kabla ya Ramadhaan, isipokuwa mtu aliyekuwa akifunga swawm. Na aendelee na swawm yake.”[5]

Ni wajibu kwa ambaye ataona mwezi mwandamo wa usiku wa tarehe thelathini Sha´baan, Ramadhaan, Shawwaal au Dhul-Qa´dah aieleze mahakama ya nchi yake. Isipokuwa ikiwa kama atajua kuwa kuna wengine ambao wameshafanya hivo. Hilo ni kutokamana na maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala):

وَتَعَاوَنُوا عَلَى الْبِرِّ وَالتَّقْوَىٰ

“Saidianeni katika wema na kumcha Allaah.”[6]

فَاتَّقُوا اللَّـهَ مَا اسْتَطَعْتُمْ

“Basi mcheni Allaah muwezavyo.”[7]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ni juu ya muislamu kusikiliza na kutii.”[8]

“Ninakuusieni juu ya kusikiliza na kutii hata kama mtatawaliwa na mja wa kihabeshi.”[9]

Ni jambo lenye kujulikana mtawala ameamrisha kupitia mahakama makuu kwa yule ambaye ataona mwezi mwandamo awajuze mahakama. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Fungeni pindi mtapouona… “

Bi maana mwezi mwandamo.

“… na fungueni pindi mtapouona. Iwapo mtafunikwa na wingu kamilisheni idadi ya [siku] thelathini.”[10]

Hakuna namna ya kuzitendea kazi Hadiyth hizi isipokuwa kwa mafanikio kutoka kwa Allaah kisha baada ya hapo waislamu kusaidiana baina yao kwa kujaribu kuutazama mwezi mwandamo na kuieleza mahakama kwa yule ambaye atakuwa ameuona. Kwa njia hiyo kunapatikana kutekeleza maamrisho ya Kishari´ah na kusaidizana katika wema na juu ya kumcha Allaah.

[1] al-Bukhaariy (1909) na Muslim (1081).

[2] Abu Daawuud (2340), at-Tirmidhiy (691), an-Nasaa’iy (2112), Ibn Maajah (1652) na ad-Daarimiy (1692). Dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Irwaa’-ul-Ghaliyl” (907).

[3] an-Nasaa’iy (2116). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Irwaa’-ul-Ghaliyl” (4/16).

[4] Abu Daawuud (2338) na ad-Daaraqutwniy (2/167). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh Abiy Daawuud” (2050).

[5] Muslim (1082).

[6] 05:02

[7] 64:16

[8] Muslim (1839).

[9] Abu Daawuud (4608), at-Tirmidhiy (2676), Ahmad (17184) na ad-Daarimiy (95). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”as-Silsilah as-Swahiyhah” (2735).

[10] al-Bukhaariy (1909) na Muslim (1081) bila ya “kwenda nje” ambayo imepokelewa na an-Nasaa’iy (2116). Swahiyh kwa mujibu al-Albaaniy katika ”Irwaa’-ul-Ghaliyl” (4/16).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Mufiyd fiy Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 5-7
  • Imechapishwa: 02/04/2022