01. Mtu kufanya kitendo kwa ajili ya dunia ni katika shirki

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

1- Allaah (Ta´ala) amesema:

مَن كَانَ يُرِيدُ الْحَيَاةَ الدُّنْيَا وَزِينَتَهَا نُوَفِّ إِلَيْهِمْ أَعْمَالَهُمْ فِيهَا وَهُمْ فِيهَا لاَ يُبْخَسُونَ أُوْلَئِكَ الَّذِينَ لَيْسَ لَهُمْ فِي الآخِرَةِ إِلاَّ النَّارُ وَحَبِطَ مَا صَنَعُواْ فِيهَا وَبَاطِلٌ مَّا كَانُواْ يَعْمَلُونَ

”Anayetaka maisha ya dunia na mapambo yake, basi Tutawalipa kikamilifu matendo yao humo nao hawatopunjwa humo; [lakini] hao ndio wale ambao hawatokuwa na chochote katika Aakhirah isipokuwa Moto. Yataharibika yale yote waliyoyafanya humo [hapa duniani] na yatabatilika yale waliyokuwa wakiyatenda.”[1]

2- Imepokelewa kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ameangamia mja wa dinari! Ameangamia mja wa dirhamu! Ameangamia mja wa Khamiyswah! Ameangamia mja wa Khamiylah! Akipewa huridhia na kama hakupewa hukasirika. Ameangamia na amehiliki mtu huyo! Kama mwiba ukimchoma basi asipate mtu wa kumchomoa! Twuubaa kwa mja ambaye amechukua khitamu za farasi wake kwa ajili ya kupigana Jihaad katika njia ya Allaah; niywele zake ziko timtim na miguu yake imejaa vumbi. Anapowekwa kuchunga [kikosi cha jeshi] basi huchunga kikwelikweli na anapowekwa nyuma kuchunga basi anachunga kikwelikweli. Akiomba idhini asingeliidhinishwa na akiombea basi maombi yake yasingekubaliwa.”[2]

MAELEZO

Shirki inayokusudiwa hapa ni ile aina ndogo. Mtu kufanya kitendo kwa ajili ya dunia maana yake ni kwamba mtu anafanya kitendo cha kidini na huku hakuna anachokusudia isipokuwa lengo la kidunia. Kwa mfano mtu akapigana jihaad kwa ajili ya mateka. Au mtu akasoma kwa ajili ya uongozi na ajira. Au akahiji na kufanya ´Umrah kwa ajili ya pesa na kitu kingine.

Tofauti kati ya mlango uliotangulia na mlango uliotangulia ni kwamba mlango uliotangulia unazungumzia kujionyesha na mlango huu unazungumzia mtu kufanya kitendo kwa ajili ya dunia. Mafungamano yake ni kwamba yote miwili kitendo kinafanywa kwa ajili ya asiyekuwa Allaah na kwamba ni shirki iliojificha. Kwa sababu makusudio na matakwa ni miongoni mwa matendo ya kimoyo. Mafungamano yake ni katika hayo. Tofauti ni kwamba kujionyesha mtu anakusudia cheo na umashuhuri na kufanya kitendo cha kidini kwa ajili ya dunia mtu anakusudia tamaa na malipo ya haraka. Imesemekana kwamba yule anayefanya kitendo cha kidini kwa ajili ya dunia ni mwenye busara zaidi kuliko yule anayefanya kwa ajili ya kujionyesha kwa sababu anafanya kwa ajili ya kujionyesha hapati chochote. Ama kuhusu yule ambaye anafanya kitendo cha kidini kwa ajili ya pato la kidunia kuna uwezekano angalau kwa uchache akafikia tamaa na manufaa fulani ya kidunia. Lakini yote mawili ni khasara mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala), kwa sababu wote wawili wameshirikisha kwenye nia na makusudio yao. Kwa hivyo yote mawili yamekutana kwa upande fulani na yametofautiana kwa upande mwingine.

[1] 11:15-16

[2] al-Bukhaariy (2887).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: I´aanat-ul-Mustafiyd bi Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 448
  • Imechapishwa: 24/07/2019