Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimhu Allaah) amesema:

Kwa jina la Allaah, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

MAELEZO

Kwa jina la Allaah – Mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) amekianza kitabu chake kwa Basmalah kwa ajili ya kuigiliza Kitabu cha Allaah (Subhanahu wa Ta´ala) ambacho kimeanzwa kwa Basmalah. Jengine ni kumwigiliza vilevile Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Yeye huanza vitabu na barua zake kwa Basmalah.

Allaah – Ni jina la Allaah (Jalla wa ´Alaa) pekee ambalo linafuatiwa na majina mengine yote. Allaah (Ta´ala) amesema:

الر كِتَابٌ أَنْزَلْنَاهُ إِلَيْكَ لِتُخْرِجَ النَّاسَ مِنَ الظُّلُمَاتِ إِلَى النُّورِ بِإِذْنِ رَبِّهِمْ إِلَى صِرَاطِ الْعَزِيزِ الْحَمِيدِ  اللَّهِ الَّذِي لَهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ وَوَيْلٌ لِلْكَافِرِينَ مِنْ عَذَابٍ شَدِيدٍ

 “Alif Laam Raa. Kitabu Tumekiteremsha kwako ili uwatoe watu katika viza kuwaingiza katika nuru kwa idhini ya Mola wao, waelekee katika njia ya Mwenye nguvu kabisa asiyeshindika, Mwenye kustahiki kuhimidiwa. Allaah ambaye ni Vyake pekee vyote viliyomo katika mbingu na katika ardhi. Na ole kwa makafiri kutokana na adhabu kali.”[1]

Hatusemi kuwa neno la kitukufu ”Allaah” ni sifa, isipokuwa hali ya kubainisha. Neno la kitukufu linakuwa na maana ya sifa yenye kufuata kwa kile kinachosifiwa.

Mwingi wa rehema [ar-Rahmaan] – Mwingi wa rehema ni katika majina maalum ya Allaah (´Azza wa Jall) na hivyo haliitwi mwingine. Mwingi wa rehema maana yake ni Yule mwenye kusifika na rehema kunjufu.

Mwenye kurehemu [ar-Rahiym] – Ni jina ambalo huitwa Allaah (´Azza wa Jall) na wengineo. Maana yake ni mwenye rehema zenye kuendelea. Mwingi wa rehema maana yake ni Mwenye rehema zenye kuenea, na Mwenye kurehemu, ambaye ni mwenye rehema zenye kuendelea, yakikusanywa, basi maana yake inakuwa “Mwingi wa rehema anayemfikishia rehema Zake kwa anayemtaka katika waja Wake”. Allaah (Ta´ala) amesema:

يُعَذِّبُ مَنْ يَشَاءُ وَيَرْحَمُ مَنْ يَشَاءُ وَإِلَيْهِ تُقْلَبُونَ

“Anamuadhibu amtakaye na anamrehemu amtakaye na Kwake mtarudishwa.”[2]

Makusudio ya Mwingi wa rehema ni ambaye rehema Zake ni zenye kuenea.

[1] 14:01-02

[2] 29:21

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sittah, uk. 03-04
  • Imechapishwa: 15/06/2021