01. Kinga ya kwanza ya janga la corona: Du´aa kabla ya janga

Himdi zote njema ni stahiki ya Allaah ambaye anamwitikia mwenye kudhikika anapomuomba, anamsaidia aliyepatwa na majanga anapomuomba, anaondosha dhara na kuyasahilisha matatizo. Nyoyo hazipati uhai isipokuwa kwa kumtaja, halitokei jambo isipokuwa kwa idhini Yake, hakiishi chenye kuchukiza isipokuwa kwa huruma Yake, hakulindwi kitu isipokuwa kwa ulinzi Wake, hakufikiwi chenye kutarajiwa isipokuwa kwa wepesi Wake na wala furaha haifikiwi isipokuwa kwa kumtii Yeye.

Nashuhudia ya kwamba hapana mungu wa kweli isipokuwa Allaah, hali ya kuwa yupekee hana mshirika, Mola wa walimwengu, Mungu wa wamwanzo na wa wamwisho, ambaye anazisimamisha mbingu na ardhi. Na nashuhudia ya kwamba Muhammad ni mja na Mtume Wake ambaye ametumilizwa kwa Kitabu kinachobainisha na njia ilionyooka. Swalah na salamu zimwendee yeye, kizazi chake na Maswahabah zake wote.

Hizi ni nyasia zenye kunufaisha ambazo napenda kukumbusha kwa mnasaba wa khofu za watu katika masiku haya juu ya janga la corona. Tunamuomba Allaah (´Azza wa Jall) atuondoshee sisi na waislamu wote kila dhara, balaa na shida na matatizo pamoja na kutuhifadhi sote kama anavyowahifadhi waja Wake wema. Kwani hakika Yeye ni muweza wa kila jambo.

1- Du´aa ya kuomba kabla ya kufikwa na janga

´Uthmaan bin ´Affaan (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Mwenye kusema mara tatu:

بِسْمِ اللهِ الَّذِي لاَ يَضُرُّ مَعَ اسْمِهِ شَيء في الأرْضِ وَلاَ في السَّمَاءِ وَهُوَ السَّمِيعُ العَلِيمُ

“Kwa jina la Allaah ambaye hakidhuru pamoja na jina Lake chochote katika ardhi na katika mbingu Naye ni Mwenye kusikia, mjuzi.”

basi hatofikwa na janga lenye kushtukiza mpaka apambazukiwe. Na yule mwenye kusema hivo wakati anapopambazukiwa mara tatu basi na janga lenye kushtukiza mpaka aingiliwe na jioni.”[1]

[1] Abu Daawuud na wengineo.

  • Mhusika: Shaykh ´Abdur-Razzaaq bin ´Abdil-Muhsin al-´Abbaad
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Ashru Waswaayaa lil-Wiqaayah min-al-Wabaa’, uk. 3-5
  • Imechapishwa: 29/03/2020