Himdi zote njema anastahiki Allaah, Mola wa walimwengu. Swalah na salamu zimwendee Mtume Wake – mkweli na mwenye kusadikishwa – Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah zake wote.

Amma ba´d:

Kitabu hichi ni kuhusu mafunzo ya Tawhiyd. Nimeona nikifupize pamoja na kutumia ibara nyepesi. Nimenukuu kutoka katika vyanzo vingi kutoka katika vitabu vya maimamu wa ulimwenguni na khaswa vitabu vya Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah, vitabu vya ´Allaamah Ibn-ul-Qayyim, vitabu vya Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab na wanafunzi zake katika maimamu wa Da´wah hii iliyobarikiwa.

Miongoni mwa mambo yasiyokuwa na shaka yoyote ndani yake ni kwamba mafunzo ya ´Aqiydah ya Kiislamu ndio mafunzo ya msingi ambayo yanastahili kutiliwa umuhimu hali ya kujifunza, kuifunza na kutendea kazi yale yanayopelekea huko. Lengo ni ili matendo mema yaweze kukubaliwa kwa Allaah na pia yamnufaishe yule mtendaji. Hilo khaswa kwa kuzingatia kwamba hii leo mirengo iliyopinda imekuwa mingi, mirengo ya ukafiri, mirengo ya Taswawwuf na utawa, mirengo ya uabudiaji makaburi na masanamu na mirengo ya Bid´ah zinazokwenda kinyume na mwongozo wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Yote hii ni mirengo khatari muda wa kuwa muislamu hakujipamba kwa silaha ya ´Aqiydah sahihi iliyochotwa kutoka katika Qur-aan, Sunnah na matendo ya Salaf wa Ummah. Muislamu kama huyu ni rahisi sana kupitiliwa na mirengo hiyo iliyopinda. Mambo haya yanapelekea kutilia umuhimu mkubwa wa kuwafunza ´Aqiydah sahihi watoto wa Kiislamu kutoka katika vyanzo vyake vya asili.

Swalah na salamu zimwendee Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah zake.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-ut-Tawhiyd wa Bayaan maa yudhwaadduhaa, uk. 05-06
  • Imechapishwa: 17/12/2019