Zakaah juu ya miradi ya ufugaji wa wanyama, uzalishaji wa maziwa na miradi ya kilimo

Swali: Kuhusu miradi ya kisasa ambayo imekuwa ikionekana siku hizi, kama miradi ya ufugaji wa wanyama, uzalishaji wa maziwa, miradi ya kilimo na miradi mikubwa ya mali zisizohamishika kama majeng – Je, miradi hii inawajibika kulipiwa zakaah? Zakaah yake hutolewaje?

Jibu: Zakaah ya miradi hii ni kama ilivyotangulia kuelezwa. Ikiwa miradi hii imeandaliwa kwa ajili ya kuuzwa na kufanya biashara ili kutafuta riziki, basi itatolewa zakaah kila bidinapokamilika mwaka wa Hijriyyah. Kila kitu kilichoandaliwa kuuzwa – kama jengo, ardhi, duka au wanyama katika shamba – kinatolewa zakaah kulingana na thamani yake mwishoni mwa mwaka. Lakini vifaa vinavyotumika katika kazi yenyewe, hivyo havitozwi zakaah. Vivyo hivyo ardhi ambayo imeandaliwa kwa ajili ya kilimo si ya biashara, hiyo haitozwi zakaah kwa sababu haikuandaliwa kuuzwa, bali kwa kufugia wanyama, kulima au shughuli kama hizo. Kwa hiyo zakaah inahusu bidhaa za biashara. Kuhusu ardhi yenyewe, jengo lisilo la biashara, vifaa vya fundi seremala au fundi chuma – kama misumeno, nyundo na mengineyo – hivyo havina zakaah. Zakaah ipo tu katika mali na bidhaa zilizoandaliwa kuuzwa, kama vile vifaa, bidhaa au vyuma vinavyouzwa.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/1074/كيف-تزكى-المشاريع-الحديثة-كالانتاج-الحيواني-وغيره
  • Imechapishwa: 23/01/2026