Swali: Wanazuoni katika nchi hii wametofautiana kuhusu hukumu ya kusikiliza Anaashiyd za Kiislamu. Wapo wanaosema haziruhusiwi na hazifai kusikilizwa kwa sababu zinafanana na nyimbo za Suufiyyah na wengine wakasema inajuzu kuzisikiliza na hakuna ubaya. Ni ipi kauli sahihi katika suala hili, khaswa kwa kuwa zimeenea kwa vijana wema waliotulia katika dini? Na pia kuhusu maigizo na michezo ya jukwaani ya Kiislamu, je, yanajuzu?

Jibu: Anaashiyd za Kiislamu ni kama mashairi. Ikiwa ni salama, basi ni salama, na ikiwa ndani yake kuna maovu, basi ni maovu. Mashairi kwa ujumla ni kama alivyosema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakika baadhi ya mashairi yana hekima.”

Lakini wengi wa washairi wako kama alivyosema Allaah:

وَالشُّعَرَاءُ يَتَّبِعُهُمُ الْغَاوُونَ

“Washairi wanafuatwa na wapotofu.”[1]

Hivyo mashairi ndani yake kuna mazuri na mabaya kama maneno mengine yote. Mazuri yake ni mazuri na mabaya yake ni mabaya. Ikiwa shairi lina maneno mazuri ya kusifu tabia njema na kuonya dhidi ya tabia mbaya, yakiwa juu ya ´Aqiydah sahihi na kukemea ´Aqiydah potofu na kubainisha ubatilifu wake na mfano wa hayo yanayojulikana katika Shari´ah, basi hilo ni shairi jema.

Vivyo hivyo inapokuja katika Anaashiyd. Ikiwa ndani yake kuna wito wa kheri, kuhamasisha kufanya mema, kushikamana na Uislamu, kulinda nchi dhidi ya maadui na mfano wa hayo, basi hakuna ubaya. Ama ikiwa ndani yake kuna wito wa batili, kupendezesha batili au kuhimiza tabia mbaya, basi yanakatazwa, kama ilivyo kwa mashairi mengine mabaya.

Kwa kumalizia ni kwamba kutoa hukumu ya jumla bila kuchunguza si sahihi. Kila aina ya Anaashiyd ichunguzwe. Yale yaliyo salama hayana tatizo, na yale yenye maovu yakemewe. Haiwezekani kutoa hukumu sahihi isipokuwa kwa kuyawasilisha kwa wanazuoni ili wabainishe hukumu yake.

[1] 2:224

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/3192/التفصيل-في-حكم-استماع-الاناشيد-الاسلامية
  • Imechapishwa: 04/11/2026