Watu kukusanyika kwa ajili ya kuwapa pole wafiwa

Swali: Ilitokea makaburini kwamba mtu mmoja aliwaamuru waliokuwa kwenye kaburi waondoke kwa ajili ya kutoa pole na kuacha kaburi wakati wa kuzika. Je, kitendo chake ni sahihi? Je, kubaki kwenye kaburi kwa ajili ya kumuombea maiti du´aa na kumuombea msamaha ni bora au kuelekea kuwapokea wanaokuja kutoa pole?

Jibu: Hili ni jambo batili. Hakuna sehemu maalum ya kutoa mkono wa pole. Bali haifai kuwe na mkusanyiko wa kutoa pole. Kutoa pole ni jambo pana; kunaweza kuwa kwa simu, msikitini au njiani. Jariyr bin ´Abdullaah al-Bajaliy (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

”Tulikuwa tukizingatia kukusanyika kwa watu kwa ajili ya maiti na kutengeneza chakula kuwa ni katika kuomboleza.”

Kwa hiyo hakuna kukusanyika wala kutengeneza chakula makaburini wala sehemu nyingine. Yote hayo hayana msingi. Kushughulika na kaburi kwa kulizika na kumuombea maiti du´aa, hilo ndilo linalotangulizwa. Kisha ndugu wa karibu huenda nyumbani. Hapana vibaya ikiwa mtu atakuja kutoa pole. Ama mkusanyiko unaokusudiwa, hauna msingi wowote. Bali inakhofiwa kuwa inaweza kuwa ni katika maombolezo.

  • Muhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Mutanawwi´ah (26)
  • Imechapishwa: 10/10/2026