Wakati muadhini anaposema swalah ni bora kuliko usingizi

Swali: Nini anachosema mtu wakati muadhini anaposema:

الصلاة خير من النوم

“Swalah ni bora kuliko usingizi.”?

Jibu: Aseme kama alivosema muadhini:

الصلاة خير من النوم

“Swalah ni bora kuliko usingizi.”

Kwa sababu pindi muadhini anaposema:

الله أكبر

“Allaah ni mkubwa.”,

 mwitikiaji atasema vivyo hivyo. Anaposema:

أَشْهَدُ أَنْ لا إِله إِلا الله الله

“Nashuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah.”,

 mwitikiaji atasema vivyo hivyo. Anaposema:

أَشْهَدُ أَنَّ مُحَمَّداً رَسُولُ الله

“Nashuhudia ya kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah.”

mwitikiaji atasema vivyo hivyo. Kisha mwitikiaji ataongezea kwa kusema:

رضيتُ باللَّهِ ربًّا وبالإسلامِ دينًا وبمحمَّدٍ رسولا

“Nimeridhia Allaah kuwa ndiye Mola, Uislamu ndio dini na Muhammad ndio Mtume.”

Anaposema:

حَيَّ عَلى الصلاةِ

“Njooni katika swalah.”,

mwitikiaji atasema:

لا حول ولا قوة إلا بالله

“Hapana kutikisika wala nguvu isipokuwa kwa msaada wa Allaah.”

Atasema vivyo hivyo wakati muadhini anaposema:

حَيَّ عَلى الْفَلاَحِ

“Njooni katika mafanikio.”

Akisema:

الله أكبر

“Allaah ni mkubwa.”,

mwitikiaji atasema vivyo hivyo. Anaposema:

لا إِله إِلا الله

“Hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah.”,

mwitikiaji atasema vivyo hivyo. Na pindi muadhini anaposema:

الصلاة خير من النوم

“Swalah ni bora kuliko usingizi.”,

Mwitikiaji atasema vivyo hivyo. Imesemekana vilevile kwamba ni sawa akisema:

صَدَقْتَ وَبَرِرْتَ

“Umesema kweli na kufanya wema.”

Imesemekana vilevile kwamba ni sawa akisema:

لا حول ولا قوة إلا بالله

“Hapana kutikisika wala nguvu isipokuwa kwa msaada wa Allaah.”

Hata hivyo kile cha kwanza ndio sahihi zaidi. Dalili ya hilo ni maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliposema:

“Mnapomsikia muadhini, basi semeni kama anavosema muadhini.”[1]

Hakuna jumla iliyobaguliwa katika Sunnah, isipokuwa tu “Njooni katika swalah” na “Njooni katika mafanikio” ambapo mwitikiaji anatakiwa kusema:

لا حول ولا قوة إلا بالله

“Hapana kutikisika wala nguvu isipokuwa kwa msaada wa Allaah.”

Pengine mtu akahoji kwamba si ni kweli kusema kwamba swalah ni bora kuliko usingizi. Ndio, lakini pia kusema Allaah ni mkubwa ni kweli na kusema hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah ni haki; je, utamwambia ambaye anatoa adhaana kuwa amesema kweli na kufanya wema? Hausemi hivo. Kwa hivyo sema kama anavosema muadhini wakati anaposema kuwa swalah ni  bora kuliko usingizi. Namna hii juu ya yale mambo mengine yote ambayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameyasema kwa njia ya kuenea.

[1] Ameipokea al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuud, at-Tirmidhiy, an-Nasaa’iy na Ibn Maajah.

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (12/195-196)
  • Imechapishwa: 02/04/2026