Udanganyifu kutoka katika msikiti wa Qiblatayn

Swali: Wakati tulipoenda Madiynah tukaingia msikiti wa Qiblatayn tukaambiwa kuwa tuswali kwanza Rak´ah mbili kuelekea Yerusalemu na Rak´ah mbili kuelekea Ka´bah. Ni upi sahihi wa kitendo hichi? Ni kwa nini msikiti huo umeitwa jina hilo la msikiti wa Qiblatayn? Je, ndio msikiti ulio hii leo?

Jibu: Hilo ni katika ghushi ya wenye kufanya ghushi. Wanawaongopea watu wazembe na kuwaambia kuwaambia hapa ni mahali pa hivi na vile. Wakati mwingine wanawaambia kuwa maeneo fulani kuna baraka kwa sababu ndipo ilipopiga goti ngamia yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati ilipofika Madiynah.

Mosi ni kwamba maeneo hayo yanahitaji kuthibitishwa. Na jengine ikiwa pamethibiti kweli – je, tunatakiwa kupatembelea? Hapana. Kwa sababu Maswahabah, ambao ndio viumbe watukufu zaidi, hawakutembelea sehemu hizo. Kutokana na ninavojua hakuna Swahabah yeyote aliyeenda kuswali katika kile kinachoitwa kuwa ndio msikiti wa Qiblatayn. Hata mimi sijui kama kweli msikiti huo ndio hapo kuliposwaliwa viblah viwili au hapana. Lakini hata kama itasihi kweli kuwa ndio huo, haijuzu kwa yeyote kuswali kwa kuelekea Shaam.

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (12/410)
  • Imechapishwa: 08/04/2026